25.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 30, 2024

Contact us: [email protected]

Biteko abaini waliouza dhahabu milioni 600/- bila kulipa kodi

MWANDISHI WETU-KAHAMA

WAZIRI wa Madini, Doto Biteko, amebaini wachimbaji wa madini wanaoendelea kuiibia Serikali ambapo kwa wiki moja, wilayani Kahama wafanyabiashara hao wameuza nje ya nchi madini ya takribani Sh milioni 600 bila kupitia masoko yaliyowekwa na hivyo kukwepa kodi.

Biteko alisema hayo jana alipofanya ziara mjini Kakola, Halmashauri ya Msalala Wilayani Kahama na kufanya mikutano na wananchi ambapo ametangaza kiama dhidi ya  watu hao wanaoiibia Serikali.

Alisema watu 12 wakazi wa Kakola wamebainika kununua madini kwa wachimbaji na kutorosha nje ya nchi bila kulipa kodi ya Serikali.

“Leo (jana),  tumetembelea baadhi ya watu tuliokuwa na taarifa zao na kukutana na mambo ya kusikitisha ambayo hayavumiliki.

Miongoni mwa hawa watu, ndani ya wiki mbili amenunua dhahabu Sh milioni 331 ameiuza bila kulipa kodi ya Serikali siku yake ya kunyakuliwa imefika.

“Aidha, mnunuzi mwingine ndani ya wiki tatu amenunua dhahabu yenye ya Shilingi milioni moja naye hajalipa kodi, ungekuwa wewe ndiyo Serikali watu hawa ungewafanya nini? mwingine madini ya milioni mbili,  mwingine ya Sh milioni 241 wote hawajalipa kodi.

“Yeyote anayeuhujumu uchumi wa nchi hii unyakuo umefika, yeyote anayenunua madini nje ya soko anavunja sheria, wiki hii  itakuwa ngumu kwenu ninyi mlionunua dhahabu kinyume cha sheria, haiwezekani watu wachache kuwa miungu watu,” alisema Biteko.

Pia Biteko amebainisha mpango wa Serikali katika kurahisisha usimamizi wa mialo nchi nzima na kubainisha kuwa mialo yote itawekwa sehemu moja na kuwa na uongozi maalumu ukishirikisha uongozi wa wizara na ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri na wa wachimbaji wadogo wa madini.

Alisema uamuzi huo umefikiwa ili kusaidia katika kutunza mazingira na kusaidia kupata taarifa sahihi za uzalishaji wa dhahabu katika mialo husika.

Pamoja na hayo alisema Serikali itaanzisha utaratibu wa kuchoma dhahabu katika eneo moja litakaloteuliwa ili kuondoa hali ya kila mmiliki wa mialo kuchoma dhahabu sehemu anapojua yeye jambo ambalo linawaondolea uwajibikaji wa kulipa kodi.

“Haiwezekani kuchenjua kwa mercury katikati ya makazi ya watu, kazi ya Serikali ni kuhakikisha inawapa mazingira ya kuchimba mbadiishe maisha yenu na mlipe kodi,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles