33.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Vita ya namba Simba si mchezo

NA MOHAMED KASSARA

BAADA ya kuhitimisha usajili wao wa msimu ujao, sasa ni rasmi kuwa vita ya namba katika kikosi cha Simba itakuwa si ya kitoto kutokana na vifaa vilivyonaswa na Wekundu wa Msimbazi hao.

Takribani kila namba, kuna wachezaji zaidi ya wawili wenye viwango vya juu, hali itakayomfanya kila mmoja kupambana hasa ili kulishawishi benchi la ufundi kumpa namba kikosi cha kwanza.

Jumla ya wachezaji 10 wapya wametua Simba ili kukiimarisha kikosi cha timu hiyo, tayari kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya tatu mfululizo, lakini pia kufanya kweli katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kati ya wachezaji hao wapya, watano ni wa kimataifa ambao ni Francis Kahata (Kenya), Tairone Santos da Silva, Gerson Fraga Viera na Wilker Henrique da Silva (Brazil), Sharaf Eldin Shiboub (Sudan) na Deo Kanda (DR Congo).
Wazawa ni Ibrahim Ajib, Beno Kakolanya na Gadiel Michael (Yanga), Kennedy Juma (Singida United) na Miraji Athuman kutoka Lipuli FC.

Wachezaji hao wanaungana na nyota wa zamani wa timu hiyo kama John Bocco, Pascal Wawa, Meddie Kagere, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Aishi Manula, Clatous Chama, Jonas Mkude, Rashid Juma, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Hassan Dilunga, Said Ndemla, Yusuf Mlipili na Mzamiru Yassin.

Usajili wa Simba msimu huu umelenga kusuka kikosi imara kitakachowawezesha si tu kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara, lakini pia kufika zaidi ya hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika waliyoishia msimu uliopita.

Kwa kutinga robo fainali ya michuano hiyo, Simba ilivuna kitita cha zaidi ya shilingi bilioni tatu kama zawadi kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Fedha hizo zimeipa jeuri Simba ya kunasa wachezaji mahiri ambao imewaona wanaweza kukiongozea kasi kikosi chao na kutikisa vigogo wa soka la Afrika kama Al Ahly ya Misri, TP Mazembe ya DR Congo, Mamelody Sundowns ya Afrika Kusini na nyinginezo.

Na sasa wakati kikosi hicho kikitarajiwa kuanza mazoezi, Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems, atakuwa na shughuli pevu kupanga kikosi cha kwanza, lakini hilo likitegemea na jinsi wachezaji watakavyokuwa wakijituma mazoezini.

Katika nafasi ya mlinda mlango, Manula atatakiwa kutokubali kufanya kosa kwani akifanya hivyo, anaweza kujikuta akiporwa namba na Kakolanya ambaye tayari ameshaweka wazi shauku yake ya kupata nafasi kikosi cha kwanza.

Kwa upande wa beki wa kulia, Kapombe atalazimika kukaza msuli hasa, kwani iwapo hatamridhisha Aussems, anaweza kujikuta akisugua benchi na nafasi yake kuchukuliwa na kiraka, Nyoni kutokana na ukweli kwamba beki ya kati ina wachezaji wengi mahiri ambao ni Da Silva, Vieira, Wawa, Kennedy na Mlipili.

Beki ya kushoto nako kutakuwa na shughuli pevu, kwani baada ya Gadiel kutua Simba, Aussems atalazimika kumpima na Tshabalala kuona nani aanze kati ya wawili hao.

Kwenye kiungo, nako vita ya namba si mchezo kutokana na ukweli kwamba kuna wachezaji wengi wa viwango vya juu, wakiongozwa na ‘mkongwe’ Mkude, Viera na Shiboub, lakini pia Ndemla na Mzamiru ambao  wapo kando yao wakiisaka nafasi hiyo kwa udi na uvumba, hivyo haitakuwa rahisi kwa yeyote kujihakikisha kuanza katika kikosi cha Simba.

Ushindani mwingine, utakuwa kati Chama, Ajib, Kahata na Dilunga katika eneo la kiungo mshambuliaji.

Vita hiyo imenogeshwa na ujio wa Ajib aliyeng’ara na Yanga kwa misimu miwili iliyopita, lakini pia Kahata aliyetokea Gor Mahia ya Kenya.

Chama alizoeleka kucheza katika nafasi hiyo msimu uliopita, akiwabwaga Haruna Niyonzima na Dilunga, lakini safari hii atatakiwa kuthibitisha ubora wake mbele Ajib ambaye alikuwa katika kiwango msimu uliopita akiwa na Yanga.

Ajib aliibuka mchezaji aliyechangia upatikanaji wa mabao mengi zaidi msimu uliopita, akiicheza nafasi kama hiyo na kufunga mabao 10, akipiga pasi za mwisho 15.

Katika eneo hilo, pia kunategemea na maamuzi ya mfumo atakaoutumia Aussems kupunguza kiungo mmoja wa kati ili kuwaanzisha Ajib na Chama pamoja au mmoja aanze mwingine atokee benchi.

Licha ujio wa washambulaji Wilker na Kanda, lakini Kagere bado haonekani kama atakosekana kwenye kikosi cha kwanza kama atakuwa fiti kwa asilimia 100%.

Kinachompa jeuri Kagere ni kiwango kizuri alichokionesha msimu ulioipita, baada ya kuifungia timu hiyo mabao 23 na kuibuka kinara wa ufungaji wa Ligi Kuu Bara.

Msimu uliopita, Kagere alikuwa akicheza sambamba na Bocco na Emmanuel Okwi aliyeondoka Msimbazi hivyo vita kubaki kati ya wenzake hao wawili na wageni.

Mwisho wa siku, Aussems ndiye atakayekuwa mwamuzi wa mwisho kutegemea na viwango vya kila mchezaji katika nafasi, mfumo na mchezo husika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles