25.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

DC ashinda kura za maoni jimbo la Lissu

Nathaniel Limu-SINGIDA

WAJUMBE wa Mkutano Mkuu wa CCM Jimbo la Singida Mashariki, wamepiga kura kupata mwana CCM mmoja ambaye atapeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Julai 31.

Katika mkutano huo uliofanyika jana, wanachama 13 walichuana katika uchaguzi huo na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Miraji Mtaturu, ameongoza kura za maoni kwa kupata kura 396.

Uchaguzi huo unafanyika baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Tundu Lissu kupoteza sifa.

Mbali ya Mtaturu, wana-CCM wengine waliochuana katika kura hizo za maoni ni pamoja na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Luteni mstaafu Chiku Galawa aliyepata kura 40.

Wengine na kura zao katika nabano ni Thomasi Kitima (79), Martini Lissu (29), Lazaro Msaru (17), Hamisi Maulidi (12),  Mwanahamisi Mujori (7), Mariamu Nkumbi (7), Moris Mukhoty (4), Jeremia Ihonde (4), Sylivester Meda (3), Shilinde Kasure (1) na Emmanuel Hume (1).

Katika uchaguzi huo ambao ulikuwa na utulivu, kila mgombea aliweza kunadi sera zake mbele ya wapigakura na kisha kuulizwa maswali kwa mujibu wa utaratibu uliotangazwa na msimamizi wa uchaguzi huo, Katibu wa Sekreterieti CCM Taifa, Salum Leja.

Leja alisema kuwa wajumbe wa mkutano mkuu wamekamilisha kazi yao ya hatua ya kwanza na sasa kinachofuata majina ya wagombea watatu yatakwenda katika vikao vya ngazi ya juu ya chama.

Akizungumza baada ya kutangazwa kushinda kura za maoni, Mtaturu, alisema kuwa Jimbo la Singida Mashariki limekuwa nyuma kimaendeleo, hivyo pindi atakapoteuliwa na chama chake anaomba ushirikiano na wananchi wote wa Singida Mashariki na Wilaya ya Ikungi kwa ujumla.

“Ninawashukuru wana CCM wenzangu kwa kunipa ushindi mnono na sote tunaona namna jimbo letu lilivyo nyuma kwa maendeleo, na pindi chama kikinipa ridhaa na kuwa mgombea, ninaomba wote tushirikiane ili tuweze kuleta maendeleo,” alisema Mtaturu,

Naye mshindi wa tatu katika kura hizo za maoni, Luteni mstaafu Chiku Galawa, alisema ameridhika na matokeo ya uchaguzi huo na atashirikiana na mwana CCM yeyote ambaye atateuliwa na chama kuweza kusukuma gurudumu la maendeleo katika jimbo hilo.

“Sina kinyongo na nimeridhika kabisa na matokeo haya, kikubwa sasa tushirikiane kwa pamoja ili kuleta maendeleo,” alisema Galawa.

Kwa upande wake Katibu wa CCM Ikungi, Noverty Kibaji alisema wanachama hao baada ya kupigiwa kura za maoni za ndani ya chama, walioshinda nafasi tatu za juu, majina yao yatawasilishwa vikao vya juu kwa uamuzi.

 “Uchaguzi huu umefanyika kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za chama chetu na tunaamini vikao vya ngazi ya juu ndio vitakuwa na maamuzi nani atakayepeperusha bendera ya chama katika uchaguzi huu wa marudio,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles