Anna Potinus – Dar es Saaam
Msanii wa muziki wa kizazi kipya Naseeb Abdul maarufu ‘Diamond Platnumz’, amesema haamini kuwa uhaba wa Kondomu za kike ni chanzo cha maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi kwakuwa sio wote wawili wanaotakiwa kuvaa bali akivaa mmoja inatosha.
Ametoa kauli hiyo leo Jumatano Julai 10, alipokua akizungumza na waandishi wa habari katika baada ya kutangaza kushirikiana na Tume yaKudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids), katika kutoa elimu ya maambukizi ya virusi vya ukimwi ambapo amesema wanaume ndio wanaowadanganya wanawake kuhusu matumizi ya kinga.
“Siamini kwamba kutopatikana kwa Kondomu za kike kunachangia maambukizi kwasababu sio lazima wavae wote wawili hivyo akivaa mmoja inatosha ni jambo la kueleweshana tu,” amesema.
“Sisi wanaume ndio tunaoongoza kulazimisha mtu asivae kinga sasa dada zangu mjiulize ni kwanini mtu afanye hivyo, maana yake hana nia nzuri na wewe itakua anataka upate ujauzito kwa lazima au nia nyingine mbaya na anakufanyia makusudi, ninaamini wanawake wakitusaidia kuweka misimamo kuwa haiwezekani basi haitawezekana,” amesema.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Tacaids, Jumanne Issango amesema kuna changamoto za upatikanaji wa Kondomu za kike na kuwataka vijana kutotumia nafasi hiyo kama sababu ya kutokuelewa na kutumia elimu zinazotolewa.
“Tunachokifanya ni kuwajengea uwezo wasichana kuweza kufanya maamuzi sahihi kuhusu afya zao, wasichana wengi wasio na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi wanawaachia mwanaume wamue iwapo watumie kinga au la jambo ambalo tunapingana nalo sana hivyo tunawajengwa uwezo wa kufanya maamuzi ya miili na afya zao kwa ujumla,” amesema Issango.
“Maeneo kama Temeke, Kinondoni na mikoa mingine kuna makundi ya vijana ambao tunawajengea uwezo tunaowaita wasichana balehe na wanawake vijana tunahakikisha wanapata elimu na kuwawezesha kiuchumi ili kuhakikisha wanapata elimu na kuwa na uwezo wa kujitegemea,” amesema Issango.
Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids), leo Jumatano Julai 10, wametangaza kushirikiana na kampuni ya Wasafi Ltd katika kupeleka ujumbe kwa jamii kuhusiana na suala la afya kupitia tamasha la Wasafi festival ambapo wasanii watapata fursa ya kutoa elimu kwa vijana juu ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi.