31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Kesi ya kina Kitilya: Shahidi wa Serikali adai hajui chochote

KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

KAIMU Kamishna wa Sera wa Wizara ya Fedha, Mgonya Benedict (52), amedai hajui lolote kuhusu kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake.

Shahidi huyo amedai pia hajui kama Benki ya Standard ya Uingereza iliilipa Serikali ya Tanzania Dola za Marekani milioni saba baada ya kuishtaki kwa kuongeza ada ya uwezeshaji kutoka asilimia 1.4 hadi 2.4. Benki ya Standard ilishindwa kesi hiyo.

Hayo yalidaiwa jana Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi wakati Benedict akitoa ushahidi wa upande wa Jamhuri kwa kuongozwa na Wakili wa Serikali, Osward Tibabyekomya na upande wa utetezi kuhoji maswali.

Akihojiwa na Wakili Dk. Masumbuko Lamwai, shahidi huyo alidai hakuhusika na hakuwepo katika kamati yoyote iliyokuwa inashughulikia mchakato wa mkopo wa Dola za Marekani milioni 550.

Alidai hajaona mkataba kati ya Serikali na Benki ya Uingereza ya Standard na hafahamu kama benki hiyo ilirejesha Dola za Marekani milioni saba kwa Serikali baada ya kuishtaki na kushinda kesi.

Dk. Lamwai alidai Serikali iliishtaki benki hiyo Uingereza kwa  madai kwamba waliongeza ada ya uwezeshaji kutoka asilimia 1.4 ya mkopo hadi asilimia 2.4, na ilishindwa kesi ikalipa Dola za Marekani milioni saba.

Shahidi alidai hajui kama ugomvi uliopo ni kati ya Serikali na Benki ya Standard kwa kuongeza hiyo ada ya uwezeshaji.

Alidai utaratibu ulikiukwa kwani awali mapendekezo yalikuwa ada ya uwezeshaji ni asilimia 1.4 lakini baadaye ikawa asilimia 2.4 na taarifa hiyo aliipata ofisini.

Akihojiwa na Wakili Jeremiah Mtobesya shahidi alidai ushahidi wote aliotoa ni kuhusiana na sheria na kanuni za mikopo.

Shahidi huyo akihojiwa na Wakili Charles Alex alidai hafahamu chochote kuhusiana na kesi iliyopo mahakamani dhidi ya washtakiwa waliopo mahakamani, alidai anayafahamu mashtaka baada ya kupitia faili ofisini.

Awali akihojiwa na Wakili Tibabyekomya alidai vitu vinavyosaidia kukidhi madhumuni ya mkopo ni mapendekezo, taarifa kuhusu hali ya soko la mitaji na fedha na mkakati wa deni.

Alidai Kamati ya Madeni baada ya kufanya uchambuzi huandaa taarifa na kuipeleka katika Kamati ya Taifa ya Madeni na kwamba taarifa hiyo inaelezea kwa ufupi taarifa ya ukopeshaji, riba, ada na uchambuzi wa awali wa sekretarieti.

Benedict alidai kunakuwa na maoni ya sekretarieti kwenda kwa Kamati ya Taifa ya Madeni kisha sekretarieti inaandaa kikao cha kamati hiyo ya taifa na wajumbe kutoka Wizara ya Fedha, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Benki Kuu.

Kwa upande wa Zanzibar alidai wajumbe wanatoka ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mhasibu Mkuu na Tume ya Mipango.

Alidai mwenyekiti wa kikao cha Kamati ya Taifa ya Madeni ni Kamishna wa Sera, Katibu Kamishna Msaidizi na lengo la kufanya uchambuzi wa Kamati ya Madeni ni kujiridhisha kama huo mkopo una masharti nafuu kwa Serikali ikiwemo ada na riba zisiwe kubwa.

Akijibu hoja ya malipo ya Dola za Marekani milioni saba alipoulizwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Tibabyekomya, alidai hajui kama Serikali ililipwa kiasi hicho cha fedha kwa sababu Idara ya Sera haihusiani na malipo kwani hufanyika kwa mhasibu mkuu.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo namba nne ya mwaka 2019 ni mshindi wa mashindano ya urembo (Miss Tanzania) mwaka 1996, Shose Sinare na Sioi Solomon, ambao walikuwa maofisa wa Benki ya Stanbic.

Wengine ni maofisa wawili wa zamani wa Wizara ya Fedha, Bedason Shallanda, ambaye kwa sasa yuko Ofisi ya Waziri Mkuu na Alfred Misana, ambaye kwa sasa yuko Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 58, yakiwemo ya kuisababishia Serikali hasara ya kiasi cha Dola za Marekani milioni sita, kujipatia fedha kiasi hicho kwa njia za udanganyifu na utakatishaji fedha kiasi hicho, kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo, kuongoza uhalifu na kumdanganya mwajiri.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Februari 2012 na Juni 2015 katika maeneo mbalimbali Dar es Salaam na nje ya nchi wakati wa mchakato kuiwezesha Serikali kupata mkopo wa Dola za Marekani milioni 550 kutoka Benki ya Standard ya nchini Uingereza.

Kaimu Kamishana huyo wa sera, anakuwa ni shahidi wa pili katika kesi hiyo kutoka upande wa Jamhuri baada ya aliyekuwa Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, kukamilisha ushahidi mahakamani hapo na kudai kuwa akiwa madarakani hadi anaondoka mkopo walioomba ulikuwa Dola za Marekani milioni 550 na ada ya uwezeshaji ilikuwa asilimia 1.4 na si asilimia 2.4 kama inavyodaiwa.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Pius Hillah mbele ya Jaji Immaculata Banzi, shahidi huyo alidai mkopo walioomba ulikuwa wapewe kwa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza ni Dola za Marekani milioni 250 na awamu ya pili dola milioni 300.

Alidai mkopo ulikuwa unatoka Benki ya Standard  kwa riba ya asilimia 6.5 na ada ya uwezeshaji ilikuwa asilimia 1.4 ya mkopo huo na ulitakiwa kupatikana mwaka 2012.

“Mchakato ulikuwa haukukamilika, mkopo haukuweza kupatikana, wataalamu walipopitia mapendekezo walishauri mkopo usubiri hadi mwaka mwingine 2012/13.

“Mei 2012 nilistaafu, mwaka 2016 nilikuwa nimeshaondoka Wizara ya Fedha, niliitwa Takukuru wakataka nieleze kuhusiana na mchakato wa mikopo, nikawaeleza.

“Nikiwa PCCB (Takukuru) niliulizwa maswali kama nafahamu mchakato wa kuomba mkopo, waliniambia mkopo ulitolewa wa Dola za Marekani milioni 600 kwa ada ya uwezeshaji ya asilimia 2.4.

“Mpaka naondoka wizarani, mchakato wa mkopo ulikuwa haujakamilika, sijajua chochote kilichoendelea, niliacha ada ya uwezeshaji ikiwa asilimia 1.4 ya mkopo wote wa Dola za Marekani milioni 550,” alidai.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles