Na Asha Bani -Dar es salaam
MADEREVA wa daladala na makondakta wao Mkoa wa Dar es Salaam, wako mbioni kubadilishiwa mwonekano mpya wa sare zao wanapokuwa kazini.
Hatua hiyo, imeelezwa kuwa ni uchakavu na kupauka kwa vitambaa wanavyotumia sasa
Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, Mratibu wa Kozi fupi wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) katika banda la maonesho yanayoendelea Viwanja Sabasaba, Mashaka Kasara, alisema hatua hiyo inatokana na malalamiko ya kuchakaa na kupauka kwa sare hizo.
Alisema katika kutekeleza mkakati hiyo, tayari wamefanya vikao kadhaa na wadu wengine, wakiwamo Chama cha Wamiliki wa Mabasi Dar es Salaam (DACOBOA), Umoja wa Wasafirishaji Abiria, Dar es Salaam (UWADAR) na kikosi cha usalama barabarani.
“Kweli zile nguo zinachakaa, ni changamoto tutabadili kitambaa cha kushona kabisa,tulipendekeza kuwa na rangi damu ya mzee nyeusi (dark maroon) kwa mujibu wa wataalamu wa aina ya vitambaa,” alisema
Alisema VETA watahusika na kutengeneza sare hizo mpya ambazo kila dereva na kondakta wake atatakiwa kuwa nayo.
“Hizo za mara kwanza za rangi ya blue zimepauka na kuchoka hivyo ni vymea kuwabadilishia nao wakaonekana wasafi machoni mwa wateja wao. Na maamuzi haya hatujakaa VETA pekee iliundwa kamati ambayo mpaka ilipendekeza aina ya vvitambaana sehemu ambayo itapatikana vitambaa hivyo,” alisema
Katika hatua nyingine, Kasara alisema chuo hicho kinatoa kozi fupifupi ikiwemo ya ushonaji nguo, maabara, ufundi wa magari na udereva.
“Kwa mahitaji ya kujua namna ya kushona ,kukata nguo, rangi ubunifu wa mitindo kwa kutumia kompyuta, batiki na ufumaji wa masweta,soksi hivyo chuo kinawakaribisha watu kufika na kujifunza kozi hiyo kwa kuwa ni ajira tosha,” alisema