30.2 C
Dar es Salaam
Sunday, March 26, 2023

Contact us: [email protected]

Wanafunzi 8,000 warejeshwa shuleni

Na Allan Vicent -Tabora

WANAFUNZI  8,250 waliokuwa wameacha shule kwa sababu mbalimbali, zikiwamo umaskini wa wazazi wao, kuhama makazi au kutumikishwa katika shughuli za kilimo na ufugaji mkoani Tabora, wamerejeshwa shuleni.

Hayo yalisemwa juzi mjini hapa na Ofisa Elimu Taaluma  Mkoa wa Tabora, Arone Vedastus wakati wa kikao kazi cha kujadili mpango mkakati wenye lengo la kutokomeza mimba na ndoa za utotoni katika jamii kilichoandaliwa na Shirika la Save The Children.

Alisema  watoto wengi, hasa wanaotoka familia zenye hali duni ya maisha au familia za wafugaji, wamekuwa wakiachishwa shule kwa sababu mbalimbali hali inayosababisha  hasa watoto wa  kike kuozeshwa mapema au kupata mimba za utotoni.

Alisema jitihada kubwa zilizofanywa na mkoa huo, chini ya Mkuu wa Mkoa huo, Aggrey Mwanri za kuhakikisha watoto wote wanalindwa na kupatiwa haki yao ya elimu, zimewezesha asilimia 75 ya watoto 11,000 walioacha shule katika kipindi cha miaka 5 iliyopita kurejea shuleni.

“Kila mtu ana wajibu wa kumlinda mtoto na kuhakikisha anapata haki zake za msingi ikiwemo elimu, serikali haitavumilia kuona vitendo vya unyanyasaji au ukandamizaji vinafanywa kwa mtoto wa shule ikiwemo kumwachisha shule,” alisema

Alisisitiza Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa wazazi, walezi, jamii na mashirika mbalimbali katika kuendesha mapambano dhidi ya unyanyasaji, ukandamizaji na ndoa za utotoni ili kuhakikisha watoto wote wanapata haki zao.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Emmanuel Nley alisema mashauri mengi ya vitendo vya unyanyaswaji wa watoto yanaharibiwa na wazazi au walezi kwa kutotoa ushirikiano kwa jeshi hilo ambapo wamekuwa wakitoa ushahidi wa uongo au kutojitokeza kabisa.

Aliitaka jamii, wazazi au walezi na waendesha mashitaka wa serikali kusimamia sheria katika kutetea watoto wote wanaonyanyaswa ili waweze kupata haki yao na kutokomeza vitendo hivyo.

Kwa upande wake Ofisa Maendeleo ya Jamii wa mkoa, Elias Mpangala,  alishauri kuwekwa mkazo na mkakati utakaosaidia kutokomeza mimba za utotoni na unyanyasaji watoto katika ngazi zote kuanzia vijiji, vitongoji, mitaa, kata, tarafa, wilaya hadi mkoa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,184FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles