25.6 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Papa Wemba: Karibu Music Festival ni tamasha la kipekee

Papa Wemba akifanya onyesho lake katika tamasha la Karibu Music Festival 2015. Picha kwa hisani ya Egdar NgelelaNa Hassan Bumbuli

TAMASHA la Karibu Music Festival lililomalizika hivi karibuni mjini Bagamoyo limeacha kumbukumbu ya mambo mengi kwa wapenzi wa sanaa ya muziki hapa nchini. Licha ya kwamba ni tamasha changa, lakini hakuna mtu anayeweza kufirikia kwamba ilikuwa ni mara ya pili kwa tamasha hilo kufanyika kutokana na jinsi lilivyoandaliwa kwa ufanisi mkubwa.

Mbali na maandalizi mazuri, lakini ubora wa kazi za sanaa zilizoonyeshwa jukwaani na wanamuziki mbalimbali ni sehemu ya mambo yaliyolifanya tamasha hilo kuonekana kama ni moja ya matamasha makubwa kabisa ya muziki katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.

Tamasha hilo lilishusha wasanii wengi waliomahiri kabisa katika fani ya muziki, lakini pia lilitoa nafasi kwa wasanii chipukizi kupanda jukwaani kufanya shoo na kilichovutia zaidi katika tamasha hilo ni kwamba ilikuwa ni 100% ‘live’.

Moja ya wanamuziki wakubwa waliotua kwenye tamasha hilo mwaka huu ni Jules Shungu Kikumba maarufu kwa jina la Papa Wemba ambaye pamoja na mambo mengine alishangaa sana kusikia kuwa hilo ni tamasha la pili kwani hakutarajia kutokana na hali aliyoiona kwenye tamasha hilo.

Katika mahojiano maalumu na mwandishi wa makala haya, Papa Wemba alisema ilikuwa ni mara yake ya kwanza kufika katika mji wa Bagamoyo, mji ambao aliusoma na kuusikia juu ya historia yake na amefika katika jambo kubwa kabisa katika maisha yake ya muziki.

“Kufika Bagamoyo ni jambo kubwa sana katika maisha yangu na ya muziki, pengine nimetembelea nchi nyingi na miji mikubwa duniani, leo hii nipo katika mji mdogo kijiografia, lakini wenye mambo makubwa sana katika historia na sanaa duniani.

“Kuna chuo cha sanaa cha kipekee, kuna tamasha la aina yake ambalo linanikutanisha katika jukwaa moja na wasanii wengine wengi tena wa aina mbalimbali za muziki, hii kwangu ni kitu kikubwa sana, nimezoea kufanya maonyesho ya peke yangu au kupanda kwenye matamasha ya muziki wa aina moja,” alisema.

Alisema Karibu Music Festival ni tamasha la aina yake na ushiriki wake umempa nafasi ya kuona vipaji vya vijana kutoka nchi mbalimbali za Afrika na jambo zuri ni kwamba wasanii hao vijana wanaonekana kuelewana jambo ambalo linawapa nafasi ya kupanua wigo katika kufanya kazi zao.

Anasema ni tamasha zuri ambalo linaweza kuimarisha mahusiano baina ya wanamuziki wa kanda mbalimbali barani Afrika na hata wale wa Ulaya na analiona kama ni jukwaa muhimu sana kwa wanamuziki chipukizi na wakongwe kukutana, kufahamiana na kufanya kazi pamoja katika siku za baadaye kama sehemu ya kubadilishana uzoefu.

“Ningependa labda kufanya muziki wa pamoja na wasanii chipukizi wa hapa Tanzania, siwezi kuangalia tu kwenye video nikajua huyu ananifaa, lakini ni kupitia tamasha kama hili ndiyo ninaweza kuona uwezo halisi na kuamua nini tunaweza kufanya.

“Mfano nimeona wanamuziki wenye vipaji vikubwa sana ambao ninaamini kama nitapata muda wa kufanya nao kazi tunaweza kutoka na kazi ambayo itakuwa bora zaidi, uzuri siku hizi si lazima tuandae muziki wa rhumba, bali tunaweza kufanya ‘fusion’ ya rhumba na aina nyingine ya muziki na kitu kikawa kizuri,” anasema.

Mkongwe huyo kutoka DRC anasema anaufahamu muziki wa Tanzania na anawafahamu wasanii chipukizi ambao wanafanya vizuri wakiwemo Nasib Abdul ‘Diamond Platinums’ na Ally Kiba ambao amekuwa akiwaona mara kadhaa kwenye televisheni.

“Muziki unapiga hatua, siangalii ni muziki gani lakini kuona wanamuziki chipukizi wa Tanzania  wanafanya vizuri katika aina fulani ya muziki hili ni jambo la kupendeza na la maendeleo,” alisema.

Licha ya hivyo, Papa Wemba anasema anaamini kupitia Karibu Music Festival wanamuziki wa Tanzania watapata fursa kubwa sana na kuendeleza muziki wao kwa kuwa analiona tamasha hilo kama ni kubwa na linaloweza kuleta mabadiliko makubwa kwa wanamuziki wa Tanzania kama watalitumia ipasavyo.

“Hata sisi tulianza kushiriki matamasha, tukajulikana naamini kupitia tamasha hili baada ya miaka kadhaa baadhi ya wanamuziki wa Tanzania watakuwa katika anga za kimataifa zaidi. Jambo kubwa ambalo wanatakiwa kufanya ni kujitahidi sana kufanya muziki na bendi kwani dunia ya sasa inahitaji muziki wa moja kwa moja maana huo wa kutoka kwenye CD watu wameshaununua na wanao majumbani mwao,” anasema.

Tamasha hilo lilishirikisha bendi na vikundi mbalimbali vya muziki kutoka Tanzania na nje ya Tanzania, takribani vikundi 28 walipanda katika Jukwaa la Karibu Music Festival mwaka huu zaidi ya nusu ya vikundi na bendi hizo zikiwa za hapa nyumbani.

Kutoka Tanzania kulikuwa na bendi za Duu Top Acoustic, Cheetah Theater, Inafrika Band, Jagwa Music, Jhikoman and Afrikabisa, Junior and Mankind, Misoji Nkwabi, Segere Original, The Spirit Band, Wika Band, Zawose Traveller, John Kitime & Ananias, Cocodo Band, Hardmad, Kadjanito & Band, Damian Soul, Juma Nature, Isha Mashauzi na Weusi.

Vikundi vilivyotoka nje ya nchi ni pamoja na H-Art The Band and Sarabi Band Kenya kutoka Kenya, Yuzzo & The Frontline Band kutoka Norway, Cie C’ArtDIC kutoka Togo. Wengine ni The Pakistan Experience kutoka Pakistan, Brian Mugenyi kutoka Uganda, Bo kutoka Afrika Kusini na Brina kutoka Jamaica.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles