28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali Ujerumani yaficha siri za wanaobeba mimba zisizotarajiwa

 NA MWANDISHI WETU

WANAWAKE walio njia panda, ambao wana ujauzito na kutaka kujifungua lakini kwa kificho huwa wana machaguo machache ya kufanya ili kutimiza ndoto yao.

Kwamba, ni hali ngumu kwa mwanamke ambaye ni mjamzito na hataki mtu yeyote ajue linapokuja suala la kuzaliwa kwa mtoto wake hasa pale anapohitaji kuficha mimba kutoka kwa wazazi wanaowatesa au waume wao wakorofi.

Mara nyingi wanawake huwa na wakati mgumu wanapojikuta wamebeba mimba iwe kwa bahati mbaya au kinyume chake, hasa kama si ya kupangwa au mwanamke kuwa bado nje ya ndoa, au mimba ya mtu mwingine.

Katika hili, wanawake huogopa ghadhabu za wazazi au waume zao watakaofahamu fika kuwa mimba si zao, hivyo huamua kutenda dhambi ya kuzitoa.

Lakini iwapo watahitaji kuficha mimba zao, kuacha majina yao kamili na anuani za mawasiliano hospitalini kwa maandalizi mara nyingi ni jambo gumu kwao.

Huwa na hofu na hawataki majina yao au anwani ya hospitali wanayojiandaa kwenda kujifungua ijulikane.

Mei 2014, Serikali ya Ujerumani ilianzisha sheria inayotoa fursa ya uwezekano wa wanawake kuweza kujifungua kwa siri ili kuwasaidia wanawake wa aina hiyo.

Chini ya sheria hiyo, mwanamke anaweza kupiga simu bure, saa 24 katika siku saba za wiki bila ya kuwapo ulazima wa kujitambulisha na atakuwa na haki ya kupata msaada mara moja na wataalamu watahakikisha anapelekwa kwa mshauri wa karibu.

Tangu sheria hiyo ipitishwe miaka minne iliyopita, wanawake zaidi ya 300 wameitumia na wamejifungua watoto wao kulingana na sheria hiyo ya kujifungua bila kujulikana.

Iwapo mjamzito ataamua kujifungua mtoto wake kwa siri, anaweza pia kupata msaada wa kifedha anaohitaji na kujifungua katika hospitali au kwa mkunga bila ya kutoa kitambulisho chake.

Mtoto aliyezaliwa mara nyingi huwekwa katika huduma ya serikali na hutunzwa huku akisuburi mzazi au mlezi ajitokeze.

Miaka mitatu baadaye, tangu sheria hiyo ilipoanzishwa, kitengo cha huduma ya familia nchini Ujerumani kimewasilisha utafiti juu ya tathmini ya sheria hiyo.

Utafiti huo umeonesha tangu sheria hiyo ilipoanzishwa Mei 2014 zaidi ya watoto 100 wamezaliwa kila mwaka.

Daktari Jörn Sommer, aliyeongoza utafiti juu ya sheria iliyopitishwa na Serikali ya Ujerumani, anasema wengi kati ya wajawazito ambao wanataka kuweka siri mimba zao pamoja na wakati wa kujifungua, huchagua hatua hiyo ya kuzaa kwa siri kama njia mbadala.

Baada ya uzazi, mzazi anaweza kumwondoa na kumpeleka mtoto wake mahala popote bila kujulikana na mtu yeyote.

Kabla ya sheria hiyo kupitishwa, kulikuwa na idadi ya vituo vinavyojulikana kwa kuwapokea watoto, au vyumba vya kuwaacha watoto kwa siri nchini Ujerumani.

Hivi ni vyumba, ambavyo kwa kawaida huunganishwa na hospitali, ambapo mama aliye kata tamaa anaweza kumweka mtoto mchanga bila kuwasiliana na mtu yeyote.

Mara tu mtoto akiwekwa kwenye kitanda kidogo kengele hulia na wahudumu huenda kumchukua mtoto huyo aliyeachwa.

Kwa mujibu ya wanaharakati nchini humo, sheria hii ni muhimu kwa sababu inasaidia wanawake walio katika hali ngumu.

Katharina Jeschke, mjumbe wa Bodi ya Usimamizi wa Chama cha Wakunga Ujerumani, anasema chama chake kinahakikisha wanawake wanapokea msaada wa matibabu na kisaikolojia wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua.

Pia chama hicho kimezisaidia hospitali na wakunga katika masuala ya kisheria wakati mjamzito alipotaka kuhifadhi jina lake libakie siri kabla ya kujifungua.

Licha ya yote hayo, uzazi wa siri unahitaji wanawake kupitia mchakato maalumu ambao ni pamoja na kutumia vitambulisho vyao kwa ajili ya kujiandikisha kwa mnasihi.

Kuna tofauti ya watoto wanaoachwa katika vyumba vya siri na uzazi wa siri. Mvulana au msichana anayewekwa katika chumba cha siri kwa kawaida hukosa fursa ya kujifunza kitu kuhusu uzazi wao.

Serikali huiona staili hii kuwa ukiukwaji wa haki ya mtoto kufahamu asili yao.

Ndiyo maana chini ya sheria ya uzazi wa siri, mwanamke mwenye mimba hutakiwa kuanika jina lake halisi kwa mnasihi. Utambulisho wake hautafichuliwa kwa yeyote wakati wa ujauzito au baada ya uzazi.

Lakini mtoto anapofikisha umri wa miaka 16 hupewa mawasiliano ya mama.

“Huu ni ufumbuzi mzuri kwa mama na mtoto,” anasema Waziri wa Masuala ya familia na Wanawake Ujerumani, Katarina Barley.

Chama cha wakunga kinashukuru kwamba sheria hiyo inawapatia madaktari na wakunga mchakato unaokubalika kisheria, pia kuwapatia wanawake msaada wanaohitaji.

“Kwa ujumla, sheria hii ni muhimu kwa sababu inawasaidia wanawake wanaokuwa katika wakati mgumu,” anasema Jeschke na kuongeza:

“Inahakikisha wanawake wanapokea msaada wa kitabibu na kisaikojilia wakati wa ujauzito, uzazi wao na baada ya uzazi.

Lakini pia chama cha wakunga kimeeleza kwamba sheria ya uzazi wa siri haitakiwi moja kwa moja kufuta utaratibu wa kuwaacha watoto katika vyumba vya siri.

Wanasema katika hali ya dharura mwanamke anaweza asipitie hatua za uzazi wa siri na hivyo kuhitajika vyumba vya siri.

Kinasema baadhi ya wanawake wa Kiasia hasa asili ya Kihindi au Kiarabu, wana changamoto zaidi katika masuala kama hayo na suala la mauaji ya heshima.

Mara nyingi mauaji ya heshima, ndugu wa kiume au mzazi huua wa kike inapobainika kuwa mjamzito ilhali hajaolewa kwa kile wanachodai kulinda heshima ya familia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles