25.2 C
Dar es Salaam
Monday, March 27, 2023

Contact us: [email protected]

Bunge liboreshe kanuni zake kuwalinda wabunge wanaopata majanga

Na LEONARD MANG’OHA

TUNDU Lissu ni mwanasiasa machachari aliyejizolea umaarufu kupitia majukwaa ya kisiasa na zaidi ni miongoni mwa wabunge ambao wamekuwa wakilichachafya Bunge kwa hoja.

Amekuwa akieleza kwa sauti kubwa wasiwasi wake kuhusu mwenendo wa mambo kadha wa kadha, ambayo yamekuwa yakiibua mijadala mizito miongoni mwa jamii.

Wakati mwingine kutokana na namna anavyoiwasilisha hoja zake kwa jamii, mara nyingi amekumbana na mkono wa dola kutokana na kauli zake tata ambazo zimekuwa zikitafsiriwa kuwa ni uchochezi.

Kutokana na kauli zake hizo, amelala katika vituo vya polisi na mahabusu, lakini hajawahi kutiwa hatiani kutokana na umahiri wake katika sheria jambo lililomsaidia mara zote kuukwepa mkono wa Mahakama.

Tangu Septemba 7, mwaka 2017 Lissu yu kitandani kutokana na shambulizi baya la kupigwa zaidi ya 30 na watu wasiojulikana wakati wa vikao vya Bunge jijini Dodoma.

Baada ya shambulizi hilo, Lissu alipatiwa huduma ya kwanza katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kisha akasafirishwa kwenda jijini Nairobi kwa matibabu zaidi.

Baada ya matibabu ya takribani miezi minne na operesheni kadhaa, Lissu alihamishiwa nchini Ubelgiji anakoendelea na matibabu mpaka sasa huku akiendelea na harakati zake za kisiasa akiwa hospitali.

Hivi karibuni Spika wa Bunge, Job Ndugai alitangaza uamuzi wa kumvua ubunge Lissu kutokana na kile alichodai kuwa ni utoro na kutojaza fomu ya mali na madeni ambazo hujazwa na wabunge kila mwaka.

Uamuzi huo ulifanywa chini ya kifungu cha 37 (iii) sura ya 343 ya Sheria ya Uchaguzi inayomtaka Spika kumpa taarifa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ikiwa kuna jimbo ambalo liko wazi kwa mujibu wa sheria.

Kutokana na hilo, Spika Ndugai alitangaza kuwa amemwandikia Mwenyekiti wa NEC barua kuwa jimbo hilo la Singida Mashariki lipo wazi.

“Nimemwandikia barua mwenyekiti wa tume aendelee na hatua za kulijaza jimbo hilo,”anasema Ndugai.

Tayari NEC imetangaza Julai 31 mwaka huu kuwa ni siku ya kufanyika uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi hiyo ya Lissu.

Katika taarifa yake kwa umma juzi, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage, anasema: “Tumezingatia  matakwa ya kifungu cha 37 (1) (b) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi sura ya 343, kutoa taarifa kwa umma kuhusu uwepo wa uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Singida Mashariki,”.

Pamoja na kwamba ni utekelezaji wa matakwa ya Katiba, sheria na kanuni hatua hii imezua gumzo kama si kizaazaa miongoni mwa wadau na wanasiasa aidha kwa mwanasiasa mmoja mmoja au chama ambao baadhi wamepaza sauti kuonyesha kuwa hawakubaliani na uamuzi uliotolewa na kiongozi huyo wa Bunge.

Pia wamo watetezi wa haki za binadamu ambao kwa pamoja wanaona uamuzi huu si sahihi kutolewa kwa mtu aina ya Lissu ambaye kwa aina ya tukio la kushambuliwa kwake asingeweza kuomba ruhusa ya Spika.

Chadema

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, anadai kuwa uamuzi huo hauwatikisi wala kuwakatisha tamaa bali unazidi kuimarisha dhamira yao ya kushika dola.

“Wanatupa sababu zaidi za kufanya kazi vitu kama hivi haviwezi kutukatisha tamaa, vinatuimarisha katika dhamira yetu, tunafanyiwa uonevu mwingi ndani ya Bunge, tunafanyiwa visa vingi. Hivi visa havituvunji moyo, zaidi vinatuimarisha.

“Hasira ya kufukuza wabunge wetu, hasira ya kutoheshimu mawazo yetu, hasira ya kuondoa michango yetu tutaimaliza kwa kupeleka wabunge wengi, kuondoa wingi wa CCM ndani ya Bunge na kuiongoza serikali ya nchi hii,”ananukuliwa Mbowe na gazeti moja la kila siku.

Hata hivyo inaelezwa kuwapo mipango ya kutumia njia nyingine za kisheria kuomba kurejeshwa kwa ubunge wa Lissu.

Kanuni za Bunge

Kupitia kanuni za Kudumu za Bunge toleo la mwaka 2016 zinaeleza kuwa, kuhudhuria vikao vya Bunge na kamati zake ni wajibu wa kwanza wa kila mbunge.  Mbunge yeyote atakayeshindwa kuhudhuria mikutano ya Bunge mitatu mfululizo bila ruhusa ya Spika iliyotolewa kwa maandishi, atapoteza ubunge wake kwa mujibu wa Ibara ya71 (1) (c) ya Katiba na Spika ataitaarifu Tume ya Uchaguzi. 

Pia kanuni hizo zinaeleza kuwa mbunge atakapokosa kuhudhuria nusu ya vikao vya mkutano mmoja bila ya sababu ya msingi atapewa onyo. 

Mbunge yeyote atakayeshindwa kuhudhuria vikao vya Bunge na zamati zake kwa sababu maalumu atatakiwa kupata kibali cha Spika, kwa madhumuni ya fasili ya (4) ya kanuni hii, kibali kitatolewa katika Ofisi za Bunge za Dodoma au Dar es Salaam au Zanzibar.

Kwa kuangalia kanuni hizi bila kuingiza masuala ya busara ambayo hata hivyo hayamlazimishi mtu kufanya jambo fulani si rahisi kumlaumu Spika Ndugai kwa uamuzi alioufanya kwa sababu alichokifanya ni kutekeleza matakwa ya kanuni hizo ambazo Bunge lenyewe limejiwekea ili kuhakikisha linasimamia hadhi na heshima yake kwa kuwadhibiti wabunge kutoenenda kinyume cha matakwa ya chombo hicho.

Lakini pamoja na usimamizi huo wa matakwa ya Katiba, sheria na kanuni bado upo mwanya katika kanuni, mwanya kwa maana ya kanuni kushindwa kuwalinda wabunge ambao wanapatwa na majanga makubwa ambayo si rahini kuomba ruhusa ya Spika kama tukio la Lissu.

Lissu wakati anaondoka nchini kwenda Nairobi hakuwa akijitambua kutokana na ukubwa wa majeraha aliyoyapata kwa kushambuliwa idadi kubwa ya risasi hakuwa katika hali ya kujitambua na hali hiyo iliendelea hivyo kwa muda mrefu hadi hapo alipozinduka akiwa Nairobi.

Kwa ufupi ni kwamba Lissu aliondoka akiwa nusu mfu. Je katika hali hiyo angeweza kuomba ruhusa ya Spika? Lakini hata baada ya operesheni nyingi na matibabu ya muda mrefu ameshindwa kurejea nchini, anaweza vipi kujaza fomu za mali na madeni ili hali hajaruhusiwa na madaktari kurejea nchini.

Kutokana na tukio la Lissu, Bunge linapaswa kurejea kanuni zake kuona kama kweli ni rafiki na zinafaa kuendelea kutumika kama zilivyo.

Bila shaka zinahitaji kuongezwa baadhi ya vifungu vya maneno ili kuondoa mapengo haya ya wazi, kwa sababu zikiendelea kuwa hivi kiongozi wa Bunge hawezi kuepuka lawama za kwamba anayo agenda ya siri ya kuwaondoa wabunge.

Na hili linaweza kuzua utata zaidi ikiwa itatokea mbunge wa chama chake, akapatwa na tukio la aina yoyote ambalo litamfanya ashindwe kuomba ruhusa ya Spika na kisha Spika akatumia busara ya kutokumwondoa kutokana na tatizo lililompata, hakuna mbunge wa upinzani atakayemwelewa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,211FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles