26 C
Dar es Salaam
Friday, November 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mbaroni kwa kumbaka, kumlawiti mama yake

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

JESHI la Polisi mkoani Dodoma linamshikilia Mazengo Chilatu (28), mkazi wa Manchali wilayani Chamwino kwa tuhuma za kumbaka na  kumlawiti mama yake mzazi.

Pia linamshikilia Donard Justine (25), mkazi wa Nanenane mkoani hapa kwa tuhuma za kumbaka kikongwe mwenye miaka 95.

Aidha watu wenye hasira katika eneo la Mailimbili Mnadani, wamempiga hadi kumuua mtu mwenye miaka kati ya 25 na 30 kwa tuhuma za kubaka watu watatu, wakiwemo mtoto wa miaka minne na mwanafunzi wa darasa la pili.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Gilles Muroto, alisema Juni 28 katika Kijiji cha Manchali wilayani Chamwino, Jeshi hilo lilimkamata Chilatu kwa tuhuma za kumlawiti mama yake mzazi.

“Mbinu alizotumia ni kumvizia akiwa amelala. Chanzo ni sababu ya ulevi na imani za kishirikina. Mtuhumiwa amekamatwa na atafikishwa mahakamani upelelezi utakapokamilika,” alisema Kamanda Muroto.

Katika tukio jingine, alisema Juni 28 katika eneo la Nanenane, Kata ya  Nzuguni  mkoani hapa, bibi kizee wa miaka 95, mkazi wa Nanenane, anadaiwa alibakwa na Justine ambaye ni pia ni mkazi wa Nanenane ambaye alimvizia akiwa amelala.

“Alimkaba shingoni asiweze kupiga kelele na kumbaka kwa nguvu. Chanzo na sababu ni ulevi na mmomonyoko wa maadili. Mtuhumiwa amekamatwa na atafikishwa mahakamani upelelezi utakapokamilika,” alisema.

Muroto alisema mtu mmoja mwanaume anayekadiriwa kuwa na  miaka kati ya 25 na 30 ambaye majina yake hayakufahamika, anadaiwa alibaka watu watatu kwa nyakati tofauti katika eneo la Mailimbili jijini hapa.

Alisema mara baada ya matukio hayo wananchi walimkamata na kumshambulia kwa kipigo hadi kufariki dunia.

Kamanda Muroto alidai kuwa tukio la kwanza alitenda Juni 23 katika eneo la Mailimbili jijini hapa ambako alimbaka bibi kizee wa miaka 80 baada ya kumvizia akiwa chooni na kumkaba shingoni.

Alidai tukio la pili alitenda Julai 3 katika eneo la Mailimbili Mnadani ambako alimbaka mtoto wa miaka minne baada ya kumshika kwa nguvu na kumvutia kichakani.

“Tukio la tatu lilitokea tena Mei 3 huko Mailimbili, alimbaka mtoto wa miaka 8, mwanafunzi wa darasa la pili baada ya kumkamata kwa nguvu na kumvutia kwenye pagale la nyumba.

“Baada ya tukio hilo wananchi walimshambulia kwa kipigo hadi kufa mara baada ya kufikishwa hospitali,” alisema Kamanda Muroto.

Katika hatua nyingine, alisema ukatili wa kijinsia umeongezeka mkoani hapa ambapo takwimu zinaonesha kwa kipindi cha miezi sita – Januari hadi Juni mwaka huu, kesi zilizoripotiwa ni 517, ambapo kwa mwaka jana ziliripotiwa 174.

“Ukatili wa kijinsia upo kwa sababu mbalimbali zikiwemo msongo wa mawazo, hali duni ya maisha, ulevi, matumizi ya madawa ya kulevya, baadhi ya viongozi wa dini kuhubiri imani potofu kwa waumini wao na uvivu wa fikra,” alisema Kamanda Muroto.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles