ANDREW MSECHU –dar es salaam
SERIKALI imetia saini mikataba ya utekelezaji wa miradi sita ya maji katika Jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani, huku Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa, akisema mradi mkubwa wa kupeleka maji katika miji 28 utakaogharimu zaidi ya Sh trilioni 1.2, utaanza mwishoni mwa mwaka huu.
Akizungumza wakati wa uwekaji saini miradi hiyo sita inayosimamiwa na Dawasco, Mbarawa alisema mradi huo ulioko chini ya Serikali unatarajiwa kuanza Septemba mwaka huu.
“Mradi huu utaanza rasmi Septemba, mwaka huu katika miji yote 28, ambapo tuna uhakika wakandarasi watakuwa tayari kwenye maeneo rasmi ya miradi katika mikoa iliyopangwa,” alisema.
Akizungumzia miradi sita iliyotiwa saini jana, Profesa Mbarawa aliagiza ianze kutekelezwa bila kuchelewa na wananchi waendelee kupatiwa maji kila eneo bila kusubiri kuzinduliwa kwa mradi.
Alisema katika miradi hiyo inayogharimu Sh bilioni 114.5, mmoja unatekelezwa kwa mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia (WB) na mingine mitano inatekelezwa kwa kutumia fedha za ndani.
Alisema awamu ya pili ya mradi wa usambazaji maji kuanzia matenki ya maji Chuo Kikuu hadi Bagamoyo uliolenga kuhudumia wateja 750,000, utakaounganisha wateja wapya 64,000, utagharamiwa na WB kwa gharama ya Sh bilioni 77.2, ukitarajiwa kukamilika miezi 18 kuanzia sasa.
Alieleza kuwa miradi mingine inayogharamiwa kwa fedha za ndani itagharimu Sh bilioni 40 ambazo zinatokana na vyanzo vya ndani ya Dawasco na uwezeshaji wa Serikali.
Aliitaja miradi mingine kuwa ni wa bomba la kusafirisha maji kutoka Jeti hadi Buza, visima 20 Kimbiji na Mpera wilayani Kigamboni, usambazaji maji Kisarawe-Pugu, mradi wa maji katika mji wa Mkuranga na bomba la kusafirisha maji kutoka Mlandizi hadi Kijiji cha Mboga (Chalinze).
Profesa Mbarawa alieleza kukerwa na kuchelewa kuanza kwa utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji kutoka Chuo Kikuu hadi Bagamoyo, ambao usanifu wake ulikamilika mwaka 2014 na makubaliano ya kifedha yaliyofikiwa wakati wa utiaji saini wa mradi wa daraja la Ubungo ambao kwa sasa uko karibu asilimia 40 ya utekelezaji.