30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Walioghushi vyeti kujiunga JKT wakamatwa

*RC aagiza wakuu wa shule, maofisa elimu wahojiwe

Elizabeth Kilindi -Njombe

JESHI la Polisi Mkoa wa Njombe linawashikilia vijana sita wakidaiwa kughushi vyeti wakati wa usaili wa nafasi za kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher ole Sendeka, alisema kutokana na vitendo vya udanganyifu, ikiwamo kughushi uraia, wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wametengua nafasi za uteuzi za vijana walioteuliwa kujiunga na jeshi hilo, kusitisha usaili na kutangaza kupokea upya maombi ya kujiunga.

“Baada ya kupitia wilaya moja na nyingine, tumebaini kuwapo udanganyifu wa vyeti kuanzia vya kuzaliwa, elimu ya msingi na tumegundua wengine uraia wao una shaka, tumesitisha baada ya kujiridhisha taarifa zilizowasilishwa mbele yetu, baadhi yake zina udanganyifu mkubwa.

“Tumetangaza upya vijana hawa walete maombi upya kuanzia Juni 29 hadi Julai 8, mwaka huu, watapaswa kuwasilisha maombi yao kwa wakuu wa wilaya kila mmoja kwenye wilaya anakotoka,” alisema Sendeka.

Alisema licha ya vijana hao, pia watu wote wanaohisiwa kuhusika katika vitendo vya udanganyifu watakamatwa na kuhojiwa na wakigundulika hatua kali za kisheria zitachukuliwa.

“Baada ya kufanya uchunguzi, wapo vijana ambao tumeridhika wameghushi vyeti vyao, tumewaelekeza wakuu wa vyombo vya usalama kuchukua hatua kwa sababu tunawashikilia… wote waliotajwa hivi sasa wako katika mikono ya vyombo vyetu kwa mahojiano zaidi,” alisema Sendeka

Alisema wapo watuhumiwa waliodaiwa kuviandaa vyeti ambao wanafuatiliwa na baadhi yao wakiwa wamekamatwa.

 “Tumegundua kuna watu wanatengeneza vyeti feki, wanaghushi saini na mihuri. Katika ngazi ya wakuu wa shule za misingi, ngazi ya maofisa elimu wilaya, ngazi ya ofisa elimu mkoa kumekuwepo na mihuri bandia, sasa wale wote ambao wametajwa wanaendelea kuhojiwa na vyombo vya ulinzi na usalama,” alisema.

Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wamesema wamefikia uamuzi huo kwa kuzingatia misingi ya sheria na haki ili kutoa nafasi kwa watoto wa wanyonge, wakiwemo wa wakulima.

Wiki mbili zilizopita, mikoa yote ilianza kuandikisha vijana  na kupokea maombi kujiunga na JKT katika ngazi za wilaya, baadaye kufanyiwa usaili ngazi za mikoa ili kupata wanaostahili kujiunga na jeshi hilo.

JWTZ

Wiki iliyopita, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), lilisema litapitia upya vijana walioandikishwa kujiunga JKT katika mikoa yote, baada ya kubainika kuwapo upungufu katika uandikishaji.

Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa jeshi hilo, Luteni Kanali Gervas Ilonda, alisema watafanya ukaguzi kabambe kuhakiki vyeti na nyaraka husika kwa vijana walioandikishwa.

Alisema wamebaini kuwapo changamoto kadhaa, zikiwamo za vijana wengi kwenda kujiandikisha mikoa mingine na kusababisha wenyeji wa mikoa husika kukosa nafasi, kutoa taarifa za uongo, baadhi ya viongozi kuingilia mchakato kwa kuwaombea nafasi ndugu na jamaa zao, utapeli katika uandikishaji na taratibu zilizowekwa kutozingatiwa.

“Kimsingi mantiki ya kugawa nafasi katika mikoa na wilaya ni kuhakikisha vijana wanapatikana kutoka nchi nzima kwa uwiano ulio sawa.

“Tunasema kijana aandikishwe anakoishi kwa sababu anashirikishwa hadi kiongozi wa kijiji au mtaa, ndiyo anajua mwenendo wake ukoje, kama ni Mtanzania, ana tabia njema, kwa sababu ndiyo viongozi wa taifa la kesho.

“Tunapochukua kwa mapenzi ya wazazi au viongozi, tunaharibu taifa na hatutapata viongozi wa kesho,” alisema Luteni Kanali Ilonda.

Alisema pia vijana wengi wamefanya vitendo viovu vya kushawishi na kujaribu kutoa rushwa na hatimaye kughushi vyeti vya kuzaliwa na vile vya elimu.

“Kuna watu wanawasaidia kughushi vyeti na kuwapa mawazo ya jinsi gani ya kufanya ili waweze kujiunga, jeshi hili lina weledi, nidhamu, hatuwezi kubeza vitendo vinavyofanyika, lazima hatua zichukuliwe,” alisema.

Kuhusu viongozi, alisema baadhi yao wamekuwa wakishiriki kutoa kila aina ya msaada ili kuhakikisha vijana wanajiunga na jeshi hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles