24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Bashiru awashukia wanaogombea mali CCM

Na ANDREW MSECHU-DAR ES SALAAM

KATIBU Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, amekemea viongozi wenye uchu na mali za chama, akiagiza waondolewe ili kuepusha migogoro isiyokuwa na tija ndani ya chama hicho.

Akizungumza katika mkutano wa wanachama wa Wilaya ya Ubungo, Dar es Salaam jana, Dk. Bashiru alisema kuna taarifa za kuwepo migogoro ya viongozi kugombania mali za chama kama ilivyo katika Kata ya Sinza, hasa Sinza B, suala ambalo linatakiwa kushughulikiwa.

“Msiwavumilie hawa viongozi wenye uchu na mali za chama. Wafukuzeni wote. CCM haina uhaba wa wanachama na kila mwanachama ana haki ya kuongoza. Hizi tabia za kulindana na kukingiana vifua ndizo zilizotufikisha hapa,” alisema.

Aliwataka wanachama na viongozi kuhakikisha wanatunza mali za chama na kuzilinda, pia kufuata utaratibu mpya uliowekwa, ambao unahitaji malipo yote yatumie mfumo rasmi tofauti na ilivyokuwa zamani.

Alisema tabia hiyo ya viongozi kudokoa mali za chama haistahili kuvumiliwa kwa kuwa inawakatisha tamaa watu wenye moyo wa kujitolea.

Dk. Bashiru alisema katika suala la mali, chama hicho katika Mkoa wa Dar es Salaam kwa mwaka kina uwezo wa kupata zaidi ya Sh bilioni tano kwa upande wa miradi pekee, lakini wapo watu ambao bado wanaendelea kuvuruga mifumo ya malipo, suala ambalo halistahili kuvumiliwa.

“Kuna baadhi ya viongozi wanavuruga mfumo, hawalipi kwa kutumia ‘control number’, bado wanaendelea kupokea fedha taslimu na kuzipangia matumizi kiholela. Wengine wanasema mabanda hayana watu kumbe yana watu, wanafanya kama mali yao, hawa hawavumiliki,” alisema.

Alieleza kuwa kwa sasa hawatarajii kupokea fedha kutoka kwa matajiri, na kwamba chama kitaendelea kutumia rasilimali na miradi yake kujipatia kipato kujiendesha.

Dk. Bashiru alitoa maagizo hayo ikiwa ni takribani mwaka mmoja tangu alipokabidhi ripoti ya Tume ya Rais kuchunguza mali za chama kwa Rais Dk. John Magufuli iliyoonesha ubadhirifu na ufujaji mkubwa wa mali hizo.

Tume hiyo ya Rais ilibaini upotevu mkubwa wa mali za chama hicho na jumuiya zake, ikiwamo Umoja wa Vijana (UVCCM), Jumuiya ya Wazazi na Umoja wa Wanawake (UWT).

“Huwezi ukaanza kupiga vita rushwa na ufisadi ndani ya Serikali wakati chama kina rushwa na ufisadi, chama nacho tunataka tukisafishe, mambo ya rushwa na ufisadi yaishe ili Tanzania iende vizuri, ndio maana tumeunda tume,’’ alisema Rais Magufuli, mara baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo.

Alisema tume hiyo imefanya kazi nzuri na akaongeza kuwa ripoti hiyo itapelekwa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ndani ya mwezi huu ili ijadiliwe na viongozi watoe maelekezo.

Kadhalika, Rais Magufuli aliwaagiza wajumbe wa sekretarieti ya CCM waliohudhuria wakati wa uwasilishwaji wa ripoti hiyo kuanza kufanyia kazi baadhi ya mambo yaliyo ndani ya uwezo wao na kwamba masuala mengine yataamuliwa na vikao vikuu vya chama.

HALI YA CHAMA

Dk Bashiru alisema kuwa chama hicho kinaendelea kujiimarisha baada ya kulegalega kwa muda, ili kuendelea kuogoza kwa ridhaa ya wananchi.

“Hapa katikati tulilegalega na tumeumia kwa sababu ya kulegalega. Sasa tunaanza kufundishana kuhusu miiko ya uongozi na kujenga chama. Tunaagiza ziundwe kamati za itikadi na uenezi na ambao watakuwa wakisimamia hili ni makatibu uenezi wote kuanzia ngazi ya shina hadi taifa,” alisema.

Alisema matatizo yaliyojitokeza ni kwa kuwa walilala usingizi fofofo na hasa katika Jiji la Dar es Salaam ambako walijikuta wakipoteza majimbo mengi na kata nyingi.

Aliema Dar es Salaam ndio mkoa wenye wapigakura wengi kuliko mikoa yote, lakini walijikuta wakipata kura chache za urais kwa kuwa walilala na kupoteza pia majimbo ya Temeke, Kinondoni, Ubungo, Kawe, Kibamba na Ukonga.

Dk. Bashiru alikemea makundi na fitina huku akieleza kuwa wapinzani wamekuwa wenye wivu na kutafuta visingizio vingi, huku viongozi wao wakijitweza na kujisifu, sifa ambazo hazitakiwi kwa wasomi.

“Kwa wasomi ni vyema kuleta fikra na mawazo mbadala na msivumulie wanaosema uongo, sifa kuu ya wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ni kutokuwa mwongo,” alisema.

AJIBU MAPIGO KIAINA

Alisema kuna mtu mmoja (hakumtaja jina), anajiita kiongozi mkuu wa chama chake, hiyo tu inamnyima sifa ya kuthaminika kama mhitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Kauli hiyo ameitoa wiki chache tangu Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, kueleza kwamba hana muda wa kulumbana na Dk. Bashiru na kudai kwamba si saizi yake.

“Huyu eti anachaguliwa na wanachama halafu anajiita kiongozi mkuu wa chama, halafu ana mwenyekiti, sasa sijui huyo mwenyekiti kazi yake ni nini. Ninamweleza kuwa aache tabia ya kujitweza. Aache uongo uongo, hiyo siyo sifa ya mhitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

“Kuna wakati anasema eti hakuna ubeberu, ubeberu upo na ndio umesababisha vita zote duniani, ndio uliosababisha kuvurugika kwa mataifa kama Iraq, Libya na mengineyo. Halafu leo unakuja kusema kuwa ubeberu ulikuwepo kwenye miaka ya 1970, aache uongo,” alisema.

Dk. Bashiru alisema ni wazi kwamba umasikini wa nchi zinazoendelea kwa kiasi kikubwa umesababishwa na mabeberu.

Alisema ni vyema kiongozi huyo arudie sifa zake za zamani ambazo hata yeye anazijua, kwa kuwa alikuwa mstaarabu, muungwana na mjenga hoja mzuri.

UCHAGUZI

Dk. Bashiru alisema wanatarajia uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 utaandaliwa vizuri na utakuwa na wagombea safi wasiohusishwa na rushwa.

Alisema uchaguzi wa mwaka 2015 ulikuwa na fujo nyingi na hata yaliyotokea hayakutarajiwa, kwa kuwa chama hakikuwa kimejiandaa kukabiliana na misukosuko iliyojitokeza.

“Hatukuwa tumejiandaa kukabiliana na misukosuko iliyotokea katika uchaguzi huo na ndiyo maana yote yale yalitokea. Sasa hivi tunajiandaa ipasavyo kuwadhibiti wauza kura na wanunua kura, na wale wote wanaojihusisha na vitendo hivyo,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles