Janeth Mushi, Arusha
Mashindano ya Jumuiya ya Michezo jijini Arusha maarufu Arusha Ndondo Cup yamefunguliwa rasmi katika viwanja vya Jeshi kikosi cha 977 Tanganyika Packers Moshono, ambapo jumla ya timu 20 zitachuana.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mashindano hayo, leo Juni 30, Mhariri Mkuu wa Kampuni ya Tan Communication Media, wamiliki wa Redio 5 Arusha, Ashura Mohamed amewataka vijana watakaoshiriki mashindano hayo kuyachukulia kama chachu ya kuendeleza vipaji vyao.
Amesema mchezo wa soka hapa nchini na duniani ni mchezo unaoongioza kuwa na washabiki wengi hivyo waendelee kufanya mazoezi kwa bidii na kuwa na nidhamu ili kukuza vipaji na kutumia mashindano hayo vyema kujitangaza.
Ashura amewataka marefa ambao wanachezesha mechi hizo na waratibu wa mashindano hayo kuhakikisha kuwa wanatumia sheria 17 za mpira wa miguu ili kuhakikisha kuwa mshindi anapatikana kihalali.
“Nimeelezwa kuwa mashindano haya yameanza mwaka 2015, yakiwa na timu 12 leo tuna timu 20 ni hatua nzuri na inaonesha wazi kuwa mmejipanga vizuri nisisitize tu sheria za mpira zifuatwe, ” amesema.
Aidha amesema ili kuongeza nguvu katika mashindano hayo ataongeza zawadi ili kuongeza hamasa kwa timu zitakazoshiriki na kufanya vyema zaidi.
Naye Mratibu wa mashindano hayo ambaye ni mdau wa michezo kutoka wilaya ya Arumeru Benjamini Mathayo, alitaja moja ya changamoto kubwa ni kukosekana kwa vifaa vya kutosha na fedha.
Alisema mashindano hayo yatasaidia kupunguza idadi ya matukio ya kihalifu na utumiaji wa madawa ya kulevya huku yakienda sambamba na utunzaji wa mazingira ambapo kila jumapili timu zote zitapanda miti katika maeneo ya wazi.