25.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Mzozo wa Iran waibuka mchuano wa wagombea urais Democratic

WASHINGTON-MAREKANI

WAGOMBEA urais kupitia chama cha Democratic nchini Marekani wamefanya mdahalo wao wa kwanza jana huku hoja kuu sita zikionekana kutawala ikiwamo mzozo kati ya Marekani na Iran.

Hoja nyingine zilizoibuka ni  huduma ya afya, mabadiliko ya tabia nchi.

Katika sehemu ya kwanza ya mdahalo huo wa siku mbili, jana na leo pia mjadala unaonekana kutawala katika eneo la sera za kigeni, ukatili unaotokana na umiliki wa silaha, na uhamiaji haramu.

Seneta wa Marekani Elizabeth Warren, ambae ni miongoni mwa wagombea wanaoongoza katika kinyang’anyiro hicho amesema atapigania huduma ya afya inayofadhiliwa na serikali na kuwakosoa wale ambao wanapinga mfumo wa afya wa aina hiyo.

“Huduma ya afya ni huduma ya msingi kwa binadamu na mimi nitapigania haki za msingi za binadamu. “

Suala la huduma ya afya limekuwa muhimu katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2020, hasa baada ya Rais Donald Trump kusaini amri ya kufuta sehemu ya mpango wa afya wa rais aliyemtangulia Barack Obama, uliokuwa ukijulikana kama Obamacare.

Kuhusu suala la Iran, Seneta wa jimbo la New Jersey, Corey Booker ndiye mgombea pekee aliyesema haungi mkono makubaliano ya nyuklia na Iran na kwamba ulikuwa ni “uamuzi wenye makosa.”

Suala la Iran limechukua mjadala mkubwa miongoni mwa wapiga kura wa Marekani hasa katika wakati huu ambao ambao nchi hizo mbili zimeingia katika mzozo mkubwa na hata kutishia kuingia vitani.

Baadhi ya wagombea waliyapa kipaumbele zaidi masuala mengine ya usalama.

Gavana wa jimbo la Washington, Jay Inslee amesema amestaajabishwa na suala la kupambana na mabadiliko ya tabia nchi kutopewa kipaumbele na wagombea wengi katika mdahalo huo.

Inslee amesema kizazi cha sasa ndiyo cha kwanza kushuhudia uchungu wa athari za mabadiliko ya tabia nchi na ndiyo cha mwisho kinachojaribu kupambana na hali hiyo.

Makamu wa rais wa zamani, Joe Biden na Seneta Bernie Sanders, ambao wanaongoza katika utafiti wa maoni ya wapiga kura, watapambana katika sehemu ya pili ya mdahalo huo leo jioni.

IRAN YATOA WITO

Wakati huo huo, Iran imeitaka Marekani kuiondolea vikwazo

Rais wa Iran, Hassan Rouhani alisema jana kwamba Marekani lazima iiondolee Iran vikwazo ilivyoiwekea pamoja na kurudi katika makubaliano ya nyuklia yaliyoafikiwa mwaka 2015 ili kumaliza mvutano kati ya nchi hizo mbili.

Rouhani alisema Marekani kurudi katika makubaliano ya nyuklia ndiyo njia rahisi ya kuhakikisha maslahi ya pande zote mbili.

Rais Trump kwa mara nyingine tena juzi alisisitiza kuwa hataki vita na Iran, lakini ameonya iwapo vita vitatokea, basi havitachukua muda mrefu.

Trump amedokeza kwamba vita hivyo vikizuka basi Marekani itashambulia kwa njia ya anga.

Marekani iliamua kujitoa katika makubaliano hayo ya nyuklia mwaka jana na badala yake kuiwekea tena vikwazo vikali Iran. Makubalaino hayo ambayo pia yaliwekwa saini na nchi nyingine zenye nguvu duniani yalikuwa na lengo la kuiondolea vikwazo Iran ili nayo ipunguze shughuli zake za kinyuklia

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles