26.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, July 16, 2024

Contact us: [email protected]

Mbwa aumia, akimbilia duka la dawa

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

HAIJALISHI una shida zinazoweza kujaza mfuko mkubwa kiasi gani, linapokuja suala la uhai, acha kabisa. Kama hujui, hiyo si kwa binadamu tu, hakuna kiumbe kisichoujua utamu wa kuendelea kuvuta pumzi.

Kuliweka sawa hilo, ni tukio la hivi karibuni mjini Istanbul, Uturuki, ambapo mbwa amejikuta akiingia katika duka la dawa baada ya kuumia akiwa kwenye mihangaiko yake.

Wengi wameonekana kuvutiwa na kipande cha video kinachomuonesha mbwa akipata matibabu, lakini iliwashangaza zaidi baada ya kusikia kuwa alikwenda mwenyewe, tofauti na wengine ambao hupelekwa na wamiliki wao.

Aliyefichua kuwa aliingia bila usaidizi wa binadamu ni video iliyonaswa na kamera za duka hilo, ambayo inamuonesha mbwa huyo akiwa amesimama mlangoni, kana kwamba alikuwa akiomba msaada.

Akisimulia ilivyokuwa siku hiyo, mhudumu wa duka hilo, Banu Cengiz, anasema: “Alikuwa ananitazama. Nilimuuliza, ‘mtoto, kuna tatizo lolote?”

Cengiz anasema kwa kuwa yeye ni mpenzi wa wanyama, alimpa bakuli ya maji, akidhani alikuwa akisumbuliwa na kiu, lakini mbwa huyo alimpa mguu wake wa mbele.

Hapo ndipo Cengiz alipohisi mbwa huyo ameumia na alipomchunguza alibaini kuwa alikuwa na jeraha lililokuwa likivuja damu.

“Nilipompa kitanda, badala ya kwenda kulala, aliendelea kusisimama usawa niliokuwa, hadi pale nilipomaliza kumtibu,” anasema Cengiz.

Katika huduma yake, Banu, ambaye duka lake lina chumba maalumu kwa mapumziko ya mbwa wa mitaani, anasema alianza kwa kulisafisha jeraha kwa dawa, kabla ya kumpaka nyingine kwa ajili ya kuzuia wadudu.

“Nilipomaliza, alilala chini, ishara fulani hivi kama kushukuru, utadhani alikuwa akiniambia ‘nakuamini’,” anaeleza mwanamama Cengiz.

Baada ya matibabu, mbwa jike huyo alipumzika dukani hapo kwa muda, kabla ya kuondoka zake. Akizungumzia umuhimu wa kuwasaidia wanyama, Cengiz anasema:

“Huwa nafanya hivyo kwa sababu nao wana hisia. Tunapaswa kuwasaidia wale wenye uhitaji. Watu wanatakiwa kuwafundisha watoto wao juu ya kuwapenda na kuwaheshimu wanyama. Kwa kufanya hivyo, tunaweza kuishi pamoja katika ulimwengu mzuri kabisa.”

Aidha, video hiyo imewavutia walio wengi, huku baadhi wakielekeza shukurani na pongezi zao kwa Cengiz, wakisema alikuwa na utu kumsaidia mbwa huyo.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, mmoja kati ya walioitazama video hiyo, Shivam Kumar, anaandika: “Utu upo kwa sababu ya wewe mama. Shukurani kwa wema wako kwa ulimwengu huu.”

Wakati huo huo, huko mitandaoni wapo walioonekana kuwasifia wanyama aina ya mbwa, wakisema wana akili hata kuliko baadhi ya binadamu. Hao ni wale walioandika ‘Mbwa kiboko yao’, ‘Huwa napenda mbwa, wakati mwingine ndiyo navutiwa na binadamu’.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles