MOHAMED KASSARA-DAR ES SALAAM
TIMU ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars leo itashuka dimbani kumenyana na Kenya katika mchezo wa pili wa hatua ya makundi wa fainali za Mataifa Afrika (Afcon), utakaochezwa Uwanja wa June 30, Cairo, Misri.
Stars ilizindua kampeni zake za michuano hiyo, kwa kuchapwa mabao 2-0 na Senegal katika mchezo kwanza uliochezwa Jumapili iliyopita pia kwenye uwanja huo huo.
Kenya kwa upande mwingine , itaingia uwanjani ikiwa na machungu ya kupigwa mabao 2-0 ma Algeria, katika mchezo wake wa kwanza wa ufunguzi uliochezwa pia Jumapili kwenye uwanja huo.
Mchezo huo ni muhimu kwa timu zote kutokana na sababu kubwa mbili, moja utayakutanisha mataifa ambayo ni majirani, yakitoka Ukanda wa Afrika Mashariki, nyingine ni kitendo cha kila moja kupoteza mechi za kwanza, hivyo ushindi ni muhimu ili kufufua matumaini yakufuzu hatua ya 16 bora.
Stars na Kenya zimekutana mara 48 katika mechi za mashindano mbalimbali.
Katika kukutana huko, Kenya imeibuka mbabe mara nyingi, ikishinda michezo 20, Stars mara 14, huku mara sare 14 zikitoka sare. Pia Kenya imefunga mabao 62, huku Stars ikifunga mabao 43.
Mara ya mwisho timu hizo zilikutana mwaka 2017, katika mchezo wa nusu fainali ya michuano ya Chalenji ya Nchi za Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), ambapo Kenya iliibuka ushindi wa bao 1-0.
Akizungumzia mchezo huo, Kocha wa Stasrs Emmanuel Amunike alisema anaamini kikosi chake kitaingia uwanjani kivingine kusaka ushindi katika mchezo huo ,ili kutafuta nafasi ya kutinga hatua 16.
“ Nafahamu utakuwa mchezo mgumu kwa pande zote mbili, hasa kutokana na sisi wote tumetoka kupoteza michezo iliyopita, mchezo huo ni nafasi pekee kwetu ya kuamua hatma, nimewaanda vema vijana wangu kuhakikisha tunashinda ili kujipatia pointi tatu zitakazotuweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele.
“Kitu kikubwa na cha muhimu ambacho tunachokifanya kwasasa ni kuwajenga kiakili na kimbinu wachezaji , nina wachezaji bora na wenye uwezo wa kupambana, naamini wanasifa za kushindana na kupata matokeo bora,”alisema kocha huyo raia wa Nigeria.
Kwa upande wake, beki wa kushoto wa timu hiyo, Gadiel Michael alisema wao kama wachezaji wamejipanga kwa ajili ya kuhakikisha wanashinda mchezo huo ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele.
“Mechi na Kenya itakuwa ngumu kwakua wale ni majirani zetu kwahiyo tunafahamiana, hata hivyo hii ni vita ambayo tunatakiwa kupigana na kushinda, tupo tayari kwa hilo,”alisema beki huyo wa Yanga.
Tayari Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda yupo nchini Misri kwa ajili ya kuongeza hamasa katika kikosi cha Stars ili kuhakikisha inapata matokeo mazuri katika mchezo dhidi ya Kenya.
Hatua ya Makonda kwenda nchini Misri kuongeza amsha amsha inatokana na agizo alilopewa na Rais wa Jamhuri ya Muu ngano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli juzi, jijini Dar ee Salaam.
“Makonda umesema unataka kwenda Misri, nakutuma nenda hata leo na kawaambie wachezaji wasikate tamaa, kushinda kwao ndiyo ushindi wa Tanzania,” Rais Magufuli alimwambia Makonda.
Pia wa bunge 30 waliondoka nchini jana kwenda kuisapoti Stars itakapoumana na Kenya leo.