Bethsheba Wambura, Dar es Salaam
Rais John Magufuli, amezindua ghala kuu na mitambo ya gesi ya Kampuni ya Taifa Gas Ltd. inayomilikiwa na mfanyabiashara Rostam Aziz ambapo amewataka Watanzania wanaotumia mkaa kuanza kutumia gesi ili kupunguza gharama na kujilinda kiafya.
Aidha, amezipongeza sekta binafsi kwa kuamua kuungana na serikali kuwekeza katika gesi asilia.
“Nitoe wito kwa Watanzania ambao wamezoea kutumia mkaa waanze kutumia gesi kwa sababu kwanza wanapunguza gharama lakini pia wanajilinda kiafya kwani gesi ni salama na nafuu kutumia.
“Lakini pia nimefurahi kuona mmiliki na wengine wanaomiliki kampuni hii kwa asilimia 100 ni wazawa, nikupongeze sana Rostam na Watanzania wengine kwa uwekezaji na kuweza kutoa ajira zaidi ya 200 kwa Watanzania,” amesema Rais Magufuli.
Amesema ameambiwa kutokana na uwekezaji huo, kampuni hiyo imefanikiwa kulipa kodi hadi kufikia Sh bilioni moja, na kuwa matumaini yake kuwa kodi itaongezeka kadri uzalishaji wa gesi utakavyokuwa naendelea kuwapongeza ambapo ameahidi kuwa serikali iko pamoja nao.
“Naomba Serikali iache kuingilia sekta binafsi walishindwa kuleta hii gesi hapa leo wameona iko tayari wanakimbia kimbia kufanya nini, lazima mambo haya tushirikiane ili yaende.
“Kuna wakati fulami tuliwahi kuchukua uamuzi fulani mgumu, kulikuwa na kampuni inaitwa TIPA leo haipo naomba sana yasije kutokea kama yalivyotokea TIPA ikasambaratika,” amesema Rais Magufuli.
Pamoja na mambo mengine, Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Nishati kuhakikisha gesi asilia inafika katika maeneo ambayo haijafika japo wizara yenyewe ina nishati yake asilia lakini ihakikishe na hii nyingine inafika katika maeneno mengi.
“Lakini nawasihi na ninyi wasambazaji mpunguze bei ya mitungi, na nimefurahi kusikia kuwa Taifa Gas mtatengeneza mitungi yenu wenyewe na hiii itafanya bei ya gesi ipungue na kila Mtanzania atamudu kununua,” amesema.