CAIRO, MISRI
MLINDA mlango wa timu ya taifa ya Zimbabwe, George Chigova, ameweka wazi kuwa, kipigo walichokipata dhidi ya Misri katika mchezo wa ufunguzi wa Mataifa ya Afrika, hakikutokana na mgogoro wao na Chama cha soka (ZIFA).
Siku chache kabla ya kuanza kwa michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON), huko nchini Misri kulikuwa na taarifa kwamba, timu ya Zimbabwe imegoma kufanya mazoezi wakishinikiza kulipwa posho zao kutoka kwa Chama cha soka nchini Zimbabwe.
Mchezo huo wa ufunguzi ulimalizika kwa Zimbabwe kukubali kichapo cha bao 1-0, lililofungwa na Mahmoud Trezeguet, lakini Zimbabwe walionesha kiwango cha hali ya juu.
“Tunajua kwamba, tulikuwa kwenye matatizo, lakini baada ya kumalizika kwa matatizo hayo wachezaji tuliambiana kuyasahau yaliyotokea na kuangalia nini tunatakiwa kukifanya kwenye mchezo huo.
“Wote tulikuwa na furaha kubwa kushiriki mchezo huo wa kwanza, hivyo hatukuupoteza kwa sababu ya mgogoro wetu wa siku chache zilizopita kwa kuwa kila kitu kilikuwa kimekaa sawa.
“Tunaamini kila chama cha soka kila matatizo yao na timu zao, hivyo kwa upande wetu tuliweza kuyamaliza, tunachotaka sasa ni kuwafanya watu wa Zimbabwe kujivunia uwepo wetu kwenye michuano hii,” alisema kipa huyo.