NA MOHAMED KASSARA-DAR ES SALAAM
MLINDA mlango , Juma Kaseja amesaini mkataba mpya wa maika mitatu wa kuendelea kuitumikia KMC.
Kaseja alijiunga na KMC msimu uliopita kwa mkataba wa mwaka mmoja uliomalizika hivi karibuni, akitokea Kagera Sugar.
Kipa huyo aliisadia timu hiyo kumaliza nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kukata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika.
KMC ilidaka fursa hiyo, baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuipa ofa ya timu mbili Tanzania, baada ya timu ya Simba kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo ilifika hatua ya robo fainali.
Yanga ni timu nyingine iliyofaidika na ofa hiyo ya CAF, ambapo itaiwakilisha Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika, ikiungana na Simba iliyokata tiketi baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Wachezaji wengine walioongezwa mikataba katika kikosi hicho kinachomilikiwa na Manispaa ya Kinondoni Charles Ilanfya, Dennis Richard, Rehan Kibingu, Sadala Lipangile, Cliff Buyoya, Ismail Gambo, Omary Ramadhan, Abdul Hillary, Ally Ramadhan na Rayman Mgungila.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Ofisa Habari wa KMC, Anwari Binde, alisema wamemuongezea mkataba Kaseja, baada ya kuridhishwa na kiwango chake.
Alitaja kingine kilichowashawishi kuongezea mkataba wa kipa huyo nyota wa zamani wa Simba ni uzoefu wake katika michuano ya kimataifa.
“Ni kweli tumempa mkataba wa miaka mitatu Kaseja, huo nimuendelezo wa kuwabakiza wachezaji wetu muhimu, tumeamua kumsajili kutokana na uzoefu wake kwenye michuano ya kimataifa, tunajua ana uwezo mkubwa, tunaamini atatusaidia kutokana na ugeni wetu kwenye mikiki mikiki ya kimataifa.
“Kaseja ni mchezaji na kiongozi kwenye kikosi chetu,amecheza mpira kwa muda mrefu, hivyo hata wachezaji tulionao wamekuwa wakifuata mfano wake, bado tunaendelea kusajili na usajili wetu unalenga kusajili wachezaji vijana, uwepo wa mkongwe utasadia kuwapa hamasa ya kupambana kwa ajili ya kuisaidia timu kufikia malengo tuliyojiwekea,” alisema Binde.