Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
UONGOZI wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) umesema wakati wowote Kampuni ya Philips itazitengeza mashine za CT-Scan na MRI ziweze kutoa huduma kwa wagonjwa.
Umeyasema hayo siku moja baada ya Rais Dk. John Magufuli kutembelea hospitali hiyo na kumng’oa Kaimu Mkurugenzi wake, Dk. Hussein Kidanto
Kaimu Mkurugenzi mpya wa hospitali hiyo, Profesa Lawrence Mseru, pia amewahimiza wafanyakazi wa hospitali hiyo kuzingatia nidhamu ya kazi kila mmoja kulingana na maelezo aliyopewa katika mkataba wake wa kazi.
Ofisa Uhusiano Mkuu wa MNH, Aminiel Eligaesha, alikuwa akizungumza na MTANZANIA baada ya kumalizika kikao kati ya wafanyakazi na uongozi wa hospitali hiyo.
Alisema Profesa Mseru amekwisha kuanza mazungumzo na kampuni ya Philips kutengeneza mashine za CT Scan na MRI ambazo zimeharibika.
“Kaimu Mkurugenzi jana alikuja kujitambulisha ili kufahamiana lakini kikubwa ni amehimiza ushirikiano na nidhamu ya kazi kwa kila mfanyakazi,” alisema.
Awali akizungumza na MTANZANIA, mgonjwa mmoja Jackson Makenge alisema anamshukuru Mungu kwa kutembelewa na Rais na kumpatiwa msaada wa matibabu.
Makenge ni mmoja wa wagonjwa aliyepata bahati ya kuzungumza na Rais Dk. Magufuli ambaye amemgharamia kupatiwa vipimo nje ya hospitali hiyo.
“Namshukuru Rais Magufuli kwa ziara yake na kitendo cha kutukumbuka wagonjwa, lakini ni wakati sasa kwa kila mmoja kuwajibika bila kusubiri kusimamiwa,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI), Dk. Othman Kilolomo, alisema ziara ya Rais Dk. Magufuli itasaidia kutatuliwa changamoto zinazowakabili.