KOCHA wa Manchester City, Manuel Pellegrini, amemtaka bosi wa klabu ya Chelsea, Roman Abramovich, kuwa na uvumilivu kutokana na matokeo wanayoyapata chini ya kocha wao, Jose Mourinho.
Mourinho kwa sasa yupo njia panda kufukuzwa katika klabu hiyo kutokana na matokeo mabaya, hivyo Pellegrini amemtaka bosi wa klabu hiyo kumpa muda Mourinho ili airudishe klabu hiyo katika ubora wake.
Hata hivyo, Pellegrini naye yupo katika wakati mgumu wa kuendelea kuifundisha klabu hiyo kama itashindwa kuchukua ubingwa, huku tayari klabu hiyo ikiwa mbioni kuitafuta saini ya kocha wa Bayern Munich, Pep Guardiola.
“Kila siku ninasoma habari mbalimbali juu ya klabu ya Chelsea kumfukuza kocha wake, Mourinho, ila sishangai kuona habari hizo kwa kuwa hata klabu ya Manchester United na klabu yangu zipo habari zinasema kuwa tupo hatarini kufukuzwa kazi kama tusipofanya vizuri.
“Kila siku mambo yanabadilika, lakini kwa upande wangu sielewi kwa nini wamiliki wa klabu wanakosa uvumilivu hali ya klabu yao ikiwa mbaya, ila kama ningekuwa namiliki timu, kocha ningempa mkataba wa miaka mitatu halafu nitaangalia baada ya hapo kama kutakuwa na uwezekano wa kuendelea nayo.
“Miaka saba iliyopita klabu nyingi za nchini England zilikuwa na uvumilivu na makocha wao, lakini kwa sasa hali hiyo inaonekana kubadilika, hii sio kwa makocha vijana tu, ila ni makocha wote,” alisema Pellegrini.