BAADA ya kuhudhuria matamasha mbalimbali na kuona faida yake, mwanamuziki wa muziki wa taarabu, Isha Mashauzi, amesema kuna haja ya wadau wa taarabu kuandaa tamasha la muziki huo ili kuutangaza kimataifa.
“Matamasha ni muhimu, kuna mambo mengi tunajifunza na pia hatuwezi kualikwa waimbaji wote wa taarabu katika matamasha hayo, lakini kama kukiwa na tamasha la taarabu kubwa kama yalivyo matamasha mengine makubwa yanayofanyika nchini itasaidia kututangaza wasanii wake na muziki wetu wa taarabu kimataifa kupitia wasanii tutakaowaalika katika tamasha hilo,” alieleza Isha.
Isha usiku wa kuamkia jana alitumbuiza katika tamasha la Karibu Music Festival, lililofanyika katika uwanja wa Mwanakarenge, uliopo Bagamoyo, mkoani Pwani.
Tamasha hilo lilihitimishwa na mkali wa muziki na bongo fleva kutoka kundi la Wanaume Halisi, Juma Nature, kwa shoo kali akiwa na wasanii wa kundi hilo, akiwemo aliyejiengua katika kundi hilo, Rich One.
Ingawa mvua ilikuwa changamoto kubwa, lakini tamasha hilo lilihitimishwa vema huku wadau mbalimbali wa muziki wakipongeza waandaaji kwa kujipanga vema, huku wakiwataka waongeze juhudi zaidi na kuleta wasanii wenye majina makubwa kutoka nje na ndani ya nchi ili washiriki katika tamasha hilo.