NA WINFRIDA MTOI-DAR ES SALAAM
KLABU ya Yanga imetangaza nafasi mbalimbali za kazi katika klabu hiyo, zikiwamo za katibu mkuu na mkurugenzi wa mashindano.
Tangu kuvurugika kwa uongozi katika klabu hiyo kwa viongozi wa juu kujiuzuru, nafasi ya Katibu mkuu ilikuwa inakaimiwa na Omar Kaya, baada ya Charles Mkwasa kuachia ngazi.
Katika tangazo la ajira lililotolewa jana na klabu hiyo, nafasi nyingine za kazi zilizotangazwa ni mkurugenzi wa benchi la ufundi na mkurugenzi wa fedha na utawala.
Ajira nyingine ni mkurugenzi wa makoso, mauzo na matukio, mkurugenzi wa sheria na uwanachama, pamoja na tenda ya usambazaji wa bidhaa za klabu hiyo.
Kati ya sifa zinazohitajika kwa waombaji wa nafasi hizo ni pamoja na elimu ya kuanzia shahada ya kwanza, pamoja na uozoefu katika sekta ya michezo na kazi anayohitaji.
Katika nafasi ya katibu mkuu, anahitajika mtu mwenye uelewa wa mchezo wa soka kitaifa na kimataifa, pamoja na uozoefu usiopungua miaka saba na kuhudhuria kozi za utawala zilizotolewa na Shirikisho La Soka La Kimataifa(FIFA).
Uongozi mpya wa klabu hiyo chini mwenyekiti Mshindo Msola na Msaidizi wake, Frederick Mwakalebela, umekuwa ukianika mikakati mbalimbali yenye lengo la kuirejesha katika chati, baada ya kushindwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania bara kwa msimu miwili mfululizo.
Wakati uongozi huo mpya ukizidi kujidhatiti, juzi Shirikisho la Soka Afrika(Caf)lilithibitisha Tanzania kuwalikishwa na timu nne katika michuano ijayo ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.
Kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu Tanzania Bara, zilizofanyiwa marekebisho, Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania( TFF), baada ya kupatikana nafasi nne, timu za Tanzania zitakazowakilisha kwenye mashindano hayo ni Simba, Yanga, ambazo zitashiriki Ligi ya Mabingwa, wakati KMC na Azam FC zitashiriki Kombe la Shirikisho.
KMC itaiwakilisha Tanzania Kombe la Shirikisho, kwa mujibu wa kanuni hiyo ambayo inatamka, kama timu iliyomaliza nafasi ta tatu itakuwa ndio bingwa wa Kombe la TFF, basi mshindi wanne atapata nafasi ya kucheza Kombe la Shirikisho.
Kwa mujibu wa kanuni hizo, bingwa wa Kombe la TFF, ambaye kwa msimu huu ni Azam atawakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho.