29.9 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

Hakimu: Wananchi wengi hawana elimu kesi za uhujumu uchumi

Na KULWA MZEE

-DAR ES SALAAM

HAKIMU Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Kelvin Mhina, amesema wananchi wengi bado hawana elimu ya kutosha juu ya kesi za uhujumu uchumi.

Amesema wananchi wengi wamekuwa hawaelewi kwanini kesi hizo zinaahirishwa mara kwa mara na upelelezi kuchukua muda mrefu.

Mhina alisema hayo alipokuwa akizungumza kwenye mahojiano maalumu juu ya elimu kwa umma inayotolewa katika mahakama zote nchini.

Alisema mahakama ilianza kutoa elimu kwa umma tangu Agosti mwaka jana lengo likiwa kutoa elimu na kusikiliza changamoto zinazowakabili wananchi.

“Kila mahakama ina siku yake ya kutoa elimu kwa umma, hapa Kisutu tunatoa elimu kila Jumanne, kikubwa ni elimu kuhusu sheria, kuna shida kubwa katika kesi za uhujumu uchumi.

“Kesi za uhujumu uchumi zimekuwa changamoto, wananchi hawajui kwanini upelelezi unachelewa kukamilika, hawaelewi kwanini zinaahirishwa mara kwa mara, hawaelewi kwamba kesi zipi Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kuzisikiliza.

“Tumekuwa tukitoa elimu katika maeneo yote hayo ikiwemo kuwafahamisha kwamba kesi za uhujumu uchumi Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kuzisikiliza, mahakama yenye mamlaka ni Mahakama Kuu, tunawaeleza pia upelelezi wake unachukua muda mrefu.

“Wananchi wanaelewa sasa hivi tofauti na kipindi cha nyuma ambacho hapakuwa na utaratibu wa kutoa elimu, waliopata elimu hawaulizi tena maswali kuhusu kuahirishwa kwa kesi za aina hiyo, ikitokea mwananchi ameuliza ni yule aliyefika kwa mara ya kwanza,” alisema.

Alisema wanaekeza wananchi jinsi ya kufungua kesi za madai, taratibu za kupata dhamana na wananchi baada ya kuelewa wanaridhishwa na huduma zinazotolewa na mahakama hiyo.

Mwananchi Moses Thomas aliyefika mahakamani kusikiliza kesi ya ndugu yake, alipohojiwa kuhusu elimu inayotolewa mahakamani hapo, alisema ameelewa utaratibu huo kwa sababu hajui sheria.

“Utaratibu ni mzuri, wengine hatujui sheria, nilikuwa sielewi kwanini kesi inatajwa  haiendelei, tumeelimishwa kwamba kesi za uhujumu uchumi upelelezi wake unachukua muda mrefu na mahakama hii haina mamlaka ya kuzisikiliza,” alisema.

Magadalena Mkumbi akizungumzia elimu wanayopewa, alisema kafika mahakamani kusikiliza kesi ya mtoto wa kaka yake.

“Nimeambiwa kesi yake ya uhujumu uchumi, yuko gerezani tangu Aprili mwaka 2018, kesi haisikilizwi wala nini, amekaa ndani sana, ni kama anaadhibiwa, Serikali iangalie yenyewe kama upelelezi haujakamilika wamwachie awe nje ili afanye kazi nyingine pamoja na kuhudumia nyumbani,” alisema Magdalena.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles