KHARTOUM – SudanÂ
WAKATI taarifa mpya zikieleza kuwa watu takribani 30 waliuawa juzi baada ya Jeshi nchini Sudan kushambulia waandamanaji, viongozi wa kijeshi wamesema wanaondoa makubaliano yaliyokuwepo awali na kuruhusu uchaguzi ufanyike ndani ya miezi tisa.
Taarifa hiyo imekuja wakati jeshi likijikuta likikemewa vikali na mataifa mbalimbali duniani kutokana na uamuzi wake wa kushambulia waandamanaji katika mji wa Khartoum, ambako imeripotiwa watu takribani 30 wameuawa akiwemo mtoto wa miaka minane huku idadi ya waliopoteza maisha ikitarajiwa kuongezeka.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres ametaka uchunguzi ufanyike akisema ameshtushwa na ripoti kuwa maafisa walifyatua risasi hospitalini.
Mashambulizi hayo ya sasa yameibuka baada ya Jeshi ya kuwapo kwa makubaliano ya miaka ya mitatu ya kipindi cha mpito ndipo uchaguzi ufanyike.
Kiongozi wa Baraza la Mpito la Kijeshi (TMC) ambalo limekuwa likiongoza nchi tangu Rais Omar Al Bashir aondolewa kwa mapinduzi madarakani Aprili mwaka huu, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, alisema katika taarifa yake iliyorushwa kupitia televisheni ya Taifa kuwa wamekubaliana “kusitisha mazugumzo na Alliance for Freedom and Change na kuondoa yote waliyokubaliana”.
Aliongeza kuwa uchaguzi utafanyika ndani ya miezi tisa na utakuwa chini ya waangalizi wa kikanda na kimataifa.
Akizungumza na Shirika la Utangazaji la Uingereza la BBC, mchambuzi na Balozi wa zamani wa Uingereza nchini Sudan, Rosalind Marsden alisema uchaguzi huo wa ghafla unaweza kutengeneza njia ya kuurudisha uongozi wa zamani madarakani.
” Hakika pia kuna hatari ya vurugu kuendelea,” alisema.
Baada ya jeshi kuua raia, viongozi walioongoza vuguvugu la kutaka utawala wa kiraia kuongoza nchi hiyo, wamesema wamesitisha mawasiliano na serikali ya mpito ya kijeshi (TMC) na kufanya mgomo.
Vikosi vya usalama vilifika maeneo ambayo watu walikua wakiandamana, mapema Jumatatu na sauti za risasi zilisikika kwenye picha za video.
Katika taarifa yake iliyosomwa kwa njia ya televisheni ya taifa, Jeshi limeeleza masikitiko yake kwa namna hali inavyozidi kuwa mbaya na kusema kuwa operesheni ilikua imewalenga wanaotia dosari hali ya usalama wa nchi.
Jeshi limesema limekuwepo kwa ajili ya kulinda raia.
Awali, wanaharakati wamesema vikosi vya usalama waliizunguka hospitali moja mjini Khartoum na kufyatulia risasi hospitali nyingine.
Kamati Kuu ya madaktari wa Sudan, walio karibu na waandamanaji wamesema mbali a watu 30 waliouawa akiwemo mtoto wa miaka minane mamia ya watu wamejeruhiwa huku idadi ikitarajiwa kuongezeka.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amezitaka mamlaka za Sudan kufanya uchunguzi na kuchukua hatua dhidi ya wale waliohusika.
Pia amelaani matumizi ya nguvu kuwatawanya waandamanaji, na kushtushwa na ripoti kuwa vikosi vya usalama kufyatua risasi kwenye hospitali.
Shirika la habari la Sudan limesema mwendesha mashtaka ameunda kamatai kufanyia uchunguzi matukio hayo.
Waandamanaji wamekua wakipiga kambi nje ya jengo la makao makuu ya jeshi tangu Aprili 6 mwaka huu, siku tano kabla ya kuangushwa kwa utawala wa Bashir.
Kabla ya uamuzi wa sasa wa uchaguzi mwezi uliopita, waandaaji na majenerali watawala walikubaliana kuhusu muundo wa serikali mpya na muda wa mpito wa miaka mitatu kuelekea kwenye utawala wa kiraia.