LONDON, Uingereza
IDADI ya wanaougua magonjwa yanayoambukizwa kwa njia ya ngono inaongezeka nchini Uingereza.
Mwaka 2018 kulikuwa na watu 447,694 waliobainika kwa mara ya kwanza kuwa na maradhi hayo, kiwango hicho kikiwa ni sawa na ongezeko la asilimi tano juu ya idadi ya mwaka 2017 ambapo watu 422,147 ndio waliopatikana na magonjwa hayo kwa mara ya kwanza.
Ugonjwa kisonono ndio unaoonekana kuwaandama zaidi Waingereza- kwa asilimia 26 sawa na wagonjwa 56,259 , idadi hiyo ikiwa ni kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa tangu mwaka 1978.
Kulikuwa na kesi 7,541 za kaswende – idadi hiyo ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia tano katika mwaka 2017.
Makundi yanatajwa kuwa katika hatari zaidi ni vijana pamoja na wanaume wanaofanya ngono na wanaume wenzao.
Inaelezwa kuwa ugonjwa unaosababisha maumivu wakati wa kukojoa au kutokwa usaha katika uume na uke (chlamydia) uliwakumba watu 218,095 , ukichukua asilimia 49 ya kesi zote mpya za magonjwa ya ngono yaliyoripotiwa.
Ugonjwa wa ‘genital warts’ unaosababisha uvimbe sehemu za siri uliwakumba watu 57,318, ukichukua asilimia 13 ya magonjwa yanayoambukizwa kwa njia ya ngono.
Kisonono uliwakumba watu 6,259 sawa na asilimia 13 ya magonjwa yanayoambukizwa kwa ngono.
Maradhi yanayosababishwa na bakteria na kusababisha maambukizi kwenye uke, njia ya choo na kinywani ulichukua asilimia nane ya magonjwa ya zinaa , zikiripotiwa kesi mpya 33,867.
Kwa upande wa kesi za Kaswende zimeongezeka kwa miaka mingi miongoni mwa wanaume na wanawake, licha ya onyo la mara kwa mara kutolewa na madaktari wa umma juu ya hatari za kufanya ngono bila kinga.
Bakteria wa ugonjwa huo husambazwa kutoka mtu mmoja hadi mwingine kupitia ngono bila kinga.
Wataalamu wanaeleza kuwa vimelea wa ugonjwa wa kisonono
huenezwi kwa busu, kukumbatia, au viti vya choo au hata kwa kushirikiana taulo au bafu.
Baadhi ya huwa hawana dalili lakini wanaweza kuambukiza wapenzi wao wanapofanya tendo la ngono.
Matabibu wanasema unaweza kutibiwa na dawa za maambukizi (antibiotics), ingawa kumekuwa na ripoti za hivi karibuni zinazosema kuwa imekuwa vigumu kwa baadhi ya watu kutibiwa katika kile wataalamu wanakiita “Super -gonorrhea” ambayo huwa sugu na kushindwa kutibiwa kwa dawa za kawaida.
Watu wenye dalili zozote za kisonono au wanaotokwa na maji maji ya kijani kwenye uke au uume au kusikia maumivu wanapokwenda haja ndogo – wanashauriwa kuwatembelea madaktari bingwa wa uzazi au kliniki ya magonjywa yatokanayo na ngono kwa ajili ya kufanyiwa vipimo.
Ugonjwa wa kisonono husababisha matatizo ya muda mrefu ya kiafya ikiwemo kushindwa kupata ujauzito miongoni mwa wanawake.
Daktari Olwen Williams, ambaye ni rais wa shirikisho la huduma za magonjywa ya zinaa na Ukimwi nchini Uingereza anasema kiwango cha mambukizi ya magonjwa yanayosambazwa kwa njia ya ngono kinatisha.
“Miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia kwa bahati mbaya kukatwa kwa ufadhili wa huduma za afya ya ngono , na hivyo kukwamisha uwezo wetu wa kukabiliana changamoto katika kipindi hiki kigumu ,” alisema.
” Kuendelea kuongezeka kwa magonjwa ya kisonono na kaswende ni jambo linalopaswa kupewa kipaumbele kama dharura ya kiafya ,vinginevyo jambo hili linaweza kusababisha madhara makubwa kwa maisha bora ya watu wengi na mfumo mzima wa afya .”
BBC