Esther Mbussi, Mwanza
Mamlaka ya Bandari (TPA) kupitia Bandari ya Mwanza, iko katika mchakato wa kutekeleza miradi mbalimbali ya ikiwamo Bandari ya Chato ambayo itakamilika Juni mwaka 2020.
Miradi hiyo imelenga kuboresha bandari hiyo ikiwamo ujenzi wa gati la Ntama katika Bandari ya Sengerema.
Mbali na gati hiyo, pia Kuna ujenzi wa gati la Mwigobero katika Bandari ya Musoma ambao tayari umekamilika na umegarimu Sh milioni 605,036,150.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza leo Jumatano Juni 5, Kaimu Meneja wa Bandari ya Ziwa Victoria, Geofrey Lwesya, amesema ujenzi wa gati la Nyamirembe katika Bandari ya Chato, kwa sasa umefikia asilimia 40 ya utekelezaji wake.
“Sehemu ya kazi iliyobaki ni kumalizia ujenzi wa jengo la abiria, jengo la mizigo, uzio, vyoo, mnara wa tanki la maji na ujenzi wa mashine ya umeme na chumba cha walinzi.
“Mradi huu unatarajiwa kukamilika Juni 16, mwaka 2020 na utagharimu Sh bilioni 1.7,” amesema.