Na BENJAMIN MASESE
-MWANZA
UTOTO umetwajwa moja ya sababu ya kuzorotesha elimu jijini Mwanza ambapo kwa mwaka 2017/18, wanafunzi 2,646 wa shule za msingi wameacha masomo kwa sababu mbalimbali wakiwamo 103 waliopata mimba.
Hayo yalielezwa na Ofisa Elimu wa Mkoa wa Mwanza, Michael Ligola, wakati akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya elimu mkoa katika kikao cha wadau wa elimu.
Ligola alisema kwa mujibu wa takwimu za elimu kuanzia mwaka 2016 hadi 2018, Mkoa wa Mwanza umeendelea kushuka katika nafasi za kitaifa kwenye matokeo ya mtihani wa darasa la saba.
Alisema mwaka 2016 Mkoa wa Mwanza ulishika nafasi ya sita katika matokeo ya darasa la saba na mwaka 2017 ulishika nafasi nane na kurejea katika nafasi ya sita mwaka jana.
Ligola alisema kwa shule za sekondari, Mkoa wa Mwanza ulishika nafasi ya sita mwaka 2016, tano mwaka 2017 na mwaka jana nafasi ya 13.
“ Takwimu zinaonyesha tatizo la wanafunzi kukatisha masomo na kuacha shule limeendelea kuwepo, hasa kwa shule za msingi.
“Wanafunzi 2,646 wametajwa kutoendelea na masomo kwa sababu mbalimbali wakiwamo 103 waliopata mimba, wengine wakiacha shule kwa sababu ya magonjwa, utoro, vifo na utovu wa nidhamu,” alisema.
Awali akifungua kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela aliwataka wadau kutambua kuwa kipimo cha elimu ni mtihani, hivyo kushuka kwa nafasi ya mkoa kitaifa kwa matokeo ya mtihani wa shule za msingi na sekondari ni kiashiria kuwa ubora wa elimu kimkoa unashuka.
“Nawaomba wadau wote wa elimu kuepuka kuleta siasa kwenye mjadala wa elimu na badala yake tung’amue changamoto zinazotufanya tuporomoke kitaaluma, nawataka wasimamizi wa elimu mkoa kufanya mapitio, usimamizi na mijadala juu ya maazimio ya wadau katika kutimiza majukumu na uwajibikaji.
“Nawatahadharisha wadau na wasimamizi wa elimu Mkoa wa Mwanza kuepuka visingizio, tambueni mapinduzi ya viwanda yanategemea elimu, hivyo misingi ya elimu ikiwa dhaifu mapinduzi ya sayansi na teknolojia hayawezi kufanikiwa,” alisema.