NA BADI MCHOMOLO
HATIMAYE timu ya Liverpool imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya usiku wa kuamkia jana baada ya kuwachapa wapinzani wao Tottenham mabao 2-0 huko nchini Hispania kwenye uwanja wa Wanda Metropolitano.
Fainali hiyo ilikuwa inasubiliwa kwa hamu kubwa sana hasa kwa mashabiki wa soka nchini Uingereza kwa kuwa ni mara ya kwanza kwa timu za nchini hiyo kutinga fainali kwa pamoja katika kipindi cha miaka kadhaa iliopita.
Kutokana na ubora ambao Liverpool wameuonesha kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita pamoja na msimu huu, idadi kubwa ya mashabiki walikuwa na imani kubwa ya timu hiyo kuweza kutwaa ubingwa.
Kikosi hicho cha kocha Jurgen Klopp kilipewa nafasi kubwa baada ya kufanya maajabu ya kuwaondoa wababe wa Kombe hilo Barcelona yenye mchezaji bora duniani Lionel Messi, katika nusu fainali.
Nusu fainali ya kwanza Barcelona wakiwa kwenye uwanja wa nyumbani walifanikiwa kushinda mabao 3-0 dhidi ya Liverpool, lakini mchezo wa marudiano ulishangaza wengi pale Anfiled ambapo Barcelona ilikubali kichapo cha mabao 4-0 na kufungashiwa virago.
Mbali na Liverpool kufika fainali, lakini wapo wengi ambao walikuwa hawana imani na Liverpool huku wakidai kuwa Klopp ana mkosi na michezo ya fainali, mikosi hiyo ilianzia wakati anaifundisha timu ya Borussia Dortmund miaka kadhaa iliopita.
Juzi ilikuwa fainali yake ya saba kwenye michuano mikubwa ya soka duniani, huku kabla ya mchezo huo tayari alikuwa amepoteza fainali zote sita kwenye fainali za michuano mbalimbali Ulaya.
Borussia Dortmund
Akiwa na timu ya Dortmund mwaka 2013, aliweza kuifikisha klabu hiyo katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini alipokea kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya wapinzani wake nchini Ujerumani, Bayern Munich.
Mwaka uliofuata 2014, aliweza kuifisha Dortmund katika fainali ya Kombe la Ujerumani (German Cup), lakini bado alikubali kichapo kingine kutoka kwa Bayern Munich cha mabao 2-0.
Mwaka 2015, aliweza kufika tena fainali ya German Cup na kukubali kichapo cha mabao 3-1, safari hiyo walikutana na wapinzani wao Wolfsburg.
Liverpool
Baada ya kumalizika kwa msimu huo, Klopp aliondoka na kwenda kujiunga na timu ya Liverpool, makali yake yakaja kuanza kuonekana msimu uliofuata baada ya kujiunga na timu hiyo, hivyo aliweza kuipeleka timu hiyo katika fainali ya Kombe la Carabao, lakini ilikubali kichapo cha mabao 3-1 dhidi ya Manchester City kwa mikwaju ya penalti baada ya mchezo huo kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Liverpool ilipoteza mchezo huo huku ikitajwa kuwa ni klabu ya nchini Uingereza ambayo inaongoza kwa kutwaa Kombe hilo, ikiwa imechukua mara nane, wakati huo Manchester City wakichukua mara sita.
Mwaka huo huo, Klopp aliweza kuipeleka fainali timu hiyo kwenye michuano ya Kombe la Europa ambapo walikutana na Sevilla, lakini kikosi hicho cha Klopp kilikubali kufungwa mabao 3-1.
Mwaka jana Liverpool iliweza kumaliza nafasi ya nne kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini iliweza kufika fainali katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Klopp alikuwa na lengo la kuweka historia katika fainali hiyo baada ya kushindwa kufanya vizuri mwaka 2013 akiwa na Dortmund.
Lakini mwaka jana walikutana na timu bora kwenye fainali hizo ambayo imeweka historia ya kuchukua mara tatu mfululizo, hao ni Real Madrid.
Liverpool wakiwa na safu bora ya ushambuliaji, ilikubali kichapo cha mabao 3-1 dhidi ya Real Madrid. Kutokana na hali hiyo Klopp alitajwa kuwa ni kocha mwenye mikosi kwa kuwa hana bahati na michezo ya fainali.
Hivyo fainali ya juzi ingezidi kumuweka pabaya hasa kwenye mitandao ya kijamii hasa kwenye suala hilo la mikosi. Lakini Mungu alikuwa upande wake na Liverpool kwa ujumla bila ya kujali ubora ambao ulioneshwa na Tottenham, lakini Liverpool waliweza kutwaa ubingwa huo kwa ushindi wa mabao 2-0.
Liverpool hawakuwa na kiwango kizuri, lakini Tottenham walikuwa vizuri zaidi bila ya kujali kupoteza mchezo huo. Tottenham walipiga jumla ya mabao 16, wakati huo Liverpool wakipiga 14, mashuti yaliyolenga lango yalikuwa nane kwa Tottenham, lakini yalikuwa matatu kwa Liverpool.
Katika suala la kumiliki mpira liliongozwa na Tottenham ambao walimiliki kwa asilimia 65, wakati huo Liverpool wakimiliki kwa asilimia 35. Tottenham hadi mchezo unamalizika walipiga jumla ya pasi 510, wakati huo Liverpool wakipiga pasi 272.
Lakini hadi dakika 90 zinamalizika kikosi hicho cha Klopp kiliweza kuibuka na ubingwa huo wa kihistoria kwa kocha huyo. Kilichowapoteza Tottenham ni kutumia muda mwingi kucheza mpira katika eneo lao, lakini walikuja kuamka tayari muda ulikuwa sio rafiki kwao.
Ingekuwa dhambi kubwa kwa Liverpool kukosa taji msimu huu huku ikiwa imemaliza nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu England kwa tofauti ya pointi moja dhidi ya Manchester City ambao wametwaa ubingwa, lakini ingekuwa mkosi mkubwa kwa Klopp kuendelea kufanya vibaya katika mchezo ya fainali.