Damian Masyenene, Mwanza
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Kilimo kuzipitia taarifa za Vyama vya Msingi vya Ushirika nchini (Amcos) juu ya makato ya fedha vinayopata kwenye mauzo ya pamba.
Majaliwa ametoa agizo hilo jana Jumanne Mei 29, jijini Mwanza kwenye mkutano wa dharura uliowakutanisha wadau wa sekta ndogo ya pamba nchini wakiwamo wabunge, wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri za wilaya zinazolima zao pamba.
Hatua hiyo inatokana na vyama hivyo hupokea makato ya Sh 50 kwa kila kilo moja ya pamba inayouzwa na wakulima lakini bado hakuna taarifa sahihi za matumizi ya fedha zao, huku Amcos nyingi zikiwa hazina hata maghala ya kuifadhia mazao hayo na kusababisha wakulima kukosa soko.
“Wizara inaendelea na utaratibu wa kukutanisha wanunuzi wa mazao ya biashara kwa ajili ya kusaidia mazao ambayo serikali iliamua yawe ya kibiashara.
“Naagiza Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Bodi ya Pamba, kujiridhisha na kupitia usahihi wa matumizi ya fedha zinazopokelewa na Amcos kwenye mauzo ya pamba,” amesema.