Asha Bani, Dar es Salaam
Ikiwa zimebaki siku nne za katazo la serikali la kutokomeza mifuko ya platiki (rambo) vikundi mbalimbali vya ujasiriamali vimeanza kutumia fursa hiyo kwa kutengeneza mifuko ya karatasi.
Kampuni ya Guru Planet iliyopo Tabata jijini Dar es Salaam, leo Jumatatu Mei 27 iliwakusanya wajasiriamali na kuwafundisha namna ya kutengeneza mifuko hiyo kwa kutumia mikono kwa lengo la kusambaza madukani na sehemu mbalimbali za biashara.
Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Nickson Martin, amesema lengo ni kuwafanya wajasiriamali kujiari lakini pia kuendana na kasi ya kuacha kutumia mifuko hiyo ya plastiki.
“Hapa wajasiriamali wengi baada kuona tangazo wamejitokeza na kuanza kujifunza kutengeneza mifuko hiyo, tunamshukuru Mungu kwa hilo ila asilimia 90 ni kina mama na 10 kina baba kwa pamoja wataanza kupata masoko yaliyowazunguka mitaani mwao ili kuendana na kasi ya katazo,” amesema.
Aidha, Martin amesema anaamini soko ni kubwa mno hivyo kila mmoja ajira hii imeanzia pale alipo na pia anaamini watafanikiwa.
Kwa upande wake mwalimu wa mafunzo ya kutengeneza mifuko hiyo, Bilhuda Mohamed amesema soko ni kubwa na huduma hiyo imeanzia Dar es Salaam lakini pia lengo kufika mikoani kote.
Baadhi ya wajasiriamali waliopata mafunzo hayo, akiwamo Ester Sinduka (70), amesema alilisikia tangazo akiwa mkoani Mwanza na alipopata fursa ya kuja jijini Dar es Salaam akaona ni vyema kujifunza ili akawafundishe wajukuu zake jinsi ya kutengeneza mifuko hiyo.