BRIGHITER MASAKI
Watanzania wametakiwa waimarishe ushirikiano, upendo na undugu miongoni mwao pia waepuke kuchochea mifarakano na matukio ya kigaidi kwa kisingizio cha dini.
Mwenyekiti wa Taasisi ya kidini ya Imamu Bukhari, Sheikh Khalifa Khamisi amesema hayo alipokuwa akitambulisha kitabu chake cha Wahabi kinachoeleza chanzo cha ugaidi na mauaji ambacho kitazinduliwa kesho jijini Dar es Salaam.
Shekh Khamisi ameamua kutunga kitabu hicho ili kuonya wanaotumia dini kujenga mifarakano na kueneza chuki katika jamii.
“Nimeamua kueleza haya kupitia kitabu changu, jamii naihasa iepuke viongozi wa dini wanaotumia mgongo wa dini zao kueneza chuki kwa maslai yao,” ameeleza Shekh Khamisi.
Kitabu hicho kinatarajiwa kuzinduliwa katika ofisi za Makao Makuu ya taasisi hiyo iliyopo Magomeni Ndungumbo, jijini Dar es Salaam ambapo uzinduzi huo utaambatana na tukio maalum la iftari.