MWANDISHI WETU-DODOMA
MBUNGE wa Mlimba, Suzan Kiwanga (Chadema), ameeleza sababu za kuangua kilio bungeni wakati akichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wiki iliyopita.
Akizungumza na MTANZANIA katika viwanja vya Bunge jana, Kiwanga alisema alilazimika kulia kutokana na ubovu wa barabara ya Mlimba hadi mpakani wa Mkoa wa Njombe, eneo la Lwamote.
“Barabara hiyo ina hali mbaya mno na katika kipindi hiki cha mvua, mabasi ya abiria yanayojaribu kwenda kule yanakaa njiani kwa zaidi ya siku tatu huku abiria wengine wakiwa ni wagonjwa, watoto na wazee.
“Hivi ninavyoongea, hata kijiko kilichokwenda kukwamua magari yaliyokwama na kusawazisha baadhi ya maeneo kwenye barabara hiyo, kimezama kabisa.
“Pia, kuna basi lilikwama kwa siku tatu, wananchi wanataabika na nilipokuwa nazungumzia suala hilo, nilijikuta ninatoa machozi.
“Kuna hatari watu wengine wanaweza kupata magonjwa ya mshtuko kama presha na hata kufia njiani kwa sababu kama kijiko kinazama, unategemea nini kwa mabasi ya kawaida.
“Ubovu wa barabara hiyo unaathiri masuala mtambuka yakiwamo masuala ya kiuchumi na kijamii ikizingatiwa wananchi walio wengi wanaoishi maeneo hayo ni wakulima na wazalishaji wakubwa wa mazao mbalimbali kama vile mpunga, ndizi, ufuta, kakao, mahindi pamoja na miti kwa ajili ya kulinda mazingira,” alisema Kiwanga.
Pamoja na hayo, mbunge huyo alimshukuru waziri mwenye dhamana ya ujenzi kwa kuwa aliahidi kutatua kero hiyo ya muda mrefu ambapo tayari upembuzi yakinifu ulikwishafanyika tangu 2017 kwa ajili ya kuijenga kwa kiwango cha lami kuanzia Ifakara hadi Kihansi.