Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam
SHAHIDI wa Jamhuri Mashaka Duma katika kesi ya uchochezi inayomkabili, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, amedai yeye ni shabiki mzuri wa mwanasiasa huyo, anampenda, anaposikia sauti yake anafurahi na anafurahi anapomwona kwenye Televisheni.
Duma amedai alipomsikia Zitto, akizungumzia mauaji ya Kigoma Uvinza aliamini na kuwachukia Polisi.
Aliyasema hayo leo asubuhi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka shahidi alidai roho yake imetulia baada kutoa hisia zake mahakamani kwamba analichukia Jeshi la Polisi kwa kitendo wanachodaiwa kukifanya Uvinza Kigoma.
Shahidi mwingine, Shabani Hamisi, amedai kitendo cha Tundu Lissu kushambuliwa kwa risasi na hajawahi kukamatwa mtu kuhusiana na tukio hilo, kilimfanya aamini maneno ya mshtakiwa kuwa Kigoma Uvinza kuna watu waliuwawa.
Anadai Polisi walipokuwa wakipita na gari lao Manzese walikuwa wakizomewa kwamba wauaji hao.
Akihojiwa na Wakili wa utetezi, Peter Kibatala kuhusu watu waliokamatwa kwa kuzomea Polisi, alidai hakuna aliyekamatwa.
Shahidi huyo alidai kuwa aliiangalia YouTube akiwa Kimara Korogwe, Dar es Salaam. Kesi itaendelea kesho saa tatu asubuhi.
Awali aliposomewa maelezo ya awali, Zitto alikana kwamba Oktoba 28,2018 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za makao makuu ya chama cha ACT Wazalendo, alitoa maneno ya uchochezi kwa nia ya kuleta chuki miongoni mwa wananchi wa Tanzania dhidi ya Jeshi la polisi.
Zitto alikana maneno ambayo anadaiwa kuyasema kuwa “watu ambao walikuwa ni majeruhi katika tukio la mapambano baina ya wananchi na polisi, wakiwa wamekwenda hospitali kupata matibabu katika kituo cha afya cha Nguruka, polisi wakapata taarifa kuwa kuna watu wanne wamekwenda hospitali kituo cha afya Nguruka kupata Matibabu wakawafuata kule wakawaua.
Jamhuri inadai maneno hayo yalikuwa ni maneno ya uchochezi yenye kuleta hisia ya hofu na chuki.
Mshtakiwa anadaiwa kutoa maneno kwamba ‘lakini tumefuatilia kwa kina jambo hili , taarifa ambazo tumezipata kutoka kijijini Mpeta Nguruka, Uvinza ni mbaya ni taarifa ambazo zinaonesha wananchi wengi sana wameuwawa na jeshi la polisi, pamoja na kwamba Afande Sirro wamekwenda kule, halijatoa taarifa yoyote kuhusu wananchi….kama hawa wanyantuzu walivamia eneo la Ranchi, kuna taratibu za kisheria za kuchukua na si kuwauwa, wananchi wengi sana wamekufa’.
Inadaiwa Zitto katika mkutano huo huo alitoa waraka kwa umma ikiwa na maneno ya kichochezi kwa nia ya kuleta chuki kwa Watanzania dhidi ya Polisi.
Pia Zitto anadaiwa alitoa maneno yafuatayo ‘Tumekuwa tukifuatilia kwa kina yanayojri yote huko Uvinza …tunasikitika kusema kuwa taarifa tunazozipata kutoka Uvinza zinaogofya mno, kwani tunaambiwa kuwa wananchi zaidi ya 100 wa kabila la Wanyantuzu wamepoteza maisha kwa kupigwa risasi na polisi, wengine wakisemwa kuuawa hata wakiwa kwenye matibabu hospitalini baada ya kujeruhiwa kwenye purukushani na polisi.