27.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Mtazamo mpya zao la kahawa

• TaCRI kuzalisha miche chotara ya kahawa milioni 23
• TCB kukuza soko la ndani kwa kuongeza matumizi
• Kuongeza maeneo mapya kilimo cha kahawa

Shermarx Ngahemera

ZAO la kahawa ndio lilikuwa linaongoza kwa kipato nchini na kufanya maeneo lililokuwa linalimwa kuwa mbele kwa maendeleo ya uchumi, elimu na huduma za jamii chini ya wananchi wenyewe. Ndio zao lililoinua Mikoa ya Kilimanjaro, Mbeya (Rungwe), Ruvuma (Mbinga) na Kagera na watu wake kuwa na maono ya maendeleo endelevu kabla ya maeneo mingine.


Hitaji la masoko ya kuuzia kahawa hiyo mikoa hiyo ilipata kuwa na vyama vya ushirika imara na tajiri kuliko sehemu nyingine hadi pale pamba ilipoanza kulimwa kwa wingi ukanda wa ziwa Victoria na kuanza kuonesha makali yake kwa kukuza kipato cha wakulima wake kupitia chama cha Ushirika wa Nyanza Cooperative Federation na baadaye Union(VCU)


Hata hivyo haikuwa rahisi kunyang’anya uongozi wa maendeleo kwa mikoa hiyo kwani pamba ni zao la msimu (seasonal) wakati kahawa au buni ni zao la kudumu na endelevu ukilipanda linaendelea kutoa mazao bila kupanda tena kwa miaka mingi. Kiuchumi ni kwamba ni zao ‘aggregative’ yaani linaendelea kuongeza kipato kwa kazi rahisi kwa kila mwaka unaoongezeka.


Kahawa ni kinywaji chenye watumiaji wengi kote duniani. Kinywaji hiki kinashikilia nafasi ya pili kwa wingi wa watumiaji baada ya maji duniani kote na kibiashara, ni bidhaa namba mbili duniani inayoongoza kwa mauzo baada ya mafuta ya petroli na madawa ya kulevya ambayo ni marafuku kisheria

Hata hivyo hali imeanza kugeuka miaka ya karibuni kwa kahawa kuongezeka magonjwa, mimea na ardhi nayo kuchoka na kidunia uzalishaji umekuwa mwingi kuliko hitaji na hivyo bei kuanguka na kufanya faida kupungua huku gharama za uzalishaji kupanda kila uchao kutokana na mahitaji makubwa ya mbolea, madawa, gharama za ughani, ada na tozo mbalimbali za Mamlaka.


Mbaya zaidi ubadhirifu umetamalaki vyama vya ushirika kwa wizi, hadaa na ukosefu wa uaminifu. Vyama vya Ushirika vya Kilimanjaro, Mbeya, Ruvuma na Kagera hivi sasa ni vivuli vya hali yao ya zamani na kufanya serikali kuingilia kati mara kwa mara kunusuru hali bila mafanikio ya kutosha kwani wengi wamezoea vya kunyonga na hivyo vya kuchinja hawaviwezi kwa kutopea kwenye wizi na ulanguzi.


Baadhi ya watumiaji wa kinywaji cha Nuru Coffee chap chap wakifurahia kinywaji hicho
 


Utafiti kutoa majibu
Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TaCRI), inaendeleza mikakati ya kuzalisha na kupanda miche ya kahawa chotara yenye tija kwa wakulima.
Mkurugenzi Mtendaji wa TaCRI, Dk. Deusdediti Kilambo, alisema mjini Hai (Moshi)kwamba uzalishaji wa miche utafanyika sambamba na utoaji wa mafunzo juu ya kanuni bora za kilimo cha kahawa ili kuongeza uzalishaji na ubora wa zao hilo.


“Inakadiriwa kuwa jumla ya miche milioni sita ya aina bora ya chotara, itazalishwa na kusambazwa kwa wakulima na takribani zaidi ya miche milioni 584, imetumika kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Januari hadi Desemba mwaka juzi, 2018.”

Anasema TaCRI kwa kushirikiana na wadau na Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), wameweka mikakati ya miaka mitatu kuanzia mwaka 2019 hadi 2022 kwa ajili ya kuzalisha miche zaidi ya milioni 23 bora na kuisambaza kwa wakulima.

Isitoshe TaCRI imetoa aina 19 za kahawa aina ya arabika na robusta ambazo hazishambuliwi na magonjwa ya chulebuni (CBD) au coffee bery disease na kutu ya majani, alisema Dk. Kilambo.

Naye Mtafiti Mkuu wa Kitengo cha Usambazaji wa Teknolojia na Mafunzo, Dk. Jeremiah Magesa, alisema wakulima pamoja na maofisa ugani wameshapatiwa mafunzo juu ya kuzingatia kanuni bora za kilimo ili kuongeza uzalishaji na utunzaji wa mibuni tangu inapokuwa shambani.

“Kwa kuzingatia hili, ni muhimu kwa uzalishaji na usambazaji wa miche aina bora ya kahawa sambamba na usambazaji wa mbolea kwa wakulima watakaopanda miche chotara.

“Pia, lazima mashamba ya wakulima yakarabatiwe ili kuongeza uzalishaji na tija kutoka gramu 300 za sasa na angalau kufikia gramu 500 kwa mti mmoja wa kahawa,” alisema Dk. Magesa.
Kwa kuzingatia upatikanaji wa taarifa na ukweli ni kwamba sisi ni sisi tutatumia hali ya chama cha Ushirika Kilimanjaro (KNCU) kama wakilishi wa hali ya ushirika na kahawa nchini .


Matatizo ya kupatikana masoko na mikopo KNCU kulifanyika juhudi ya kutumia mpangilio wa Stakabadhi Ghalani kama dhamana kwa Mikopo kwa wakulima wa Kahawa Kilimanjaro na mwanzoni ulifanikiwa na kuifanya serikali itumie mpango huo nchi nzima na haswa kwenye zao la korosho.

Pamoja na ukweli huo, kwa siku za hivi karibuni zao hilo limeanza kupoteza hadhi yake kutokana na changamoto kadha wa kadha ikiwamo wananchi kulipa kisogo kwa kile kinachodaiwa kupanda kwa gharama za uendeshaji na kushuka kwa bei ya zao hilo sokoni.

Kwa mujibu wa takwimu za TCB, uzalishaji wa zao hilo umekuwa ukipanda na kushuka katika misimu saba iliyopita mithili ya homa ya malaria.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya kahawa nchini (TCB), Primus Kimaryo anasema uzalishaji wa kahawa mwaka 2017/2018 ulitarajiwa kushuka hadi kufikia tani 43,000 bila kufafanua.

Changamoto kubwa ni upatikanaji wa mikopo yenye masharti nafuu kutokana na mabenki mengi kujiendesha kibiashara zaidi.
KNCU ililazimika kuanzisha benki yake ya ushirika kwa jina la KCBL na 1994 kabla ya mwaka 1995 kupata leseni ya Benki Kuu ya kutoa huduma za kibenki ambako
mwaka uliofuata yaani 1996 huduma za kibenki zilianza rasmi na kusitishwa kwa kufilisika mwaka 2018.

Aliyekuwa Meneja Mkuu wa Benki hiyo, Joseph Kingazi aliwahi kusema benki hiyo inao wanahisa 245 ambao ni vyama vya ushirika wa mazao (AMCOS), vyama
vya ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) pamoja na watu binafsi wapatao 307; sasa ni historia.

Kulegalega uzalishaji kahawa

Ingawa kahawa ni mojawapo ya zao mkakati nchini ambapo serikali inafanya juhudi za kila aina kuongeza uzalishaji wake ili kuongeza pato la taifa kwa mauzo ya nje ya nchi, mengine yakiwa pamba, chai, korosho na tumbaku.
Lakini ni kiasi kidogo sana cha kahawa kinatumika nchini kwa kiasi kisichozidi asilimia 10 ya uzalishaji.

Kutokana na ukweli huo zao hili mara nyingi hukumbwa na kukosekana na bei ya uhakika kwani hutegemea soko la nje ya nchi ambako nchi hii haina sauti kubwa kwani ni mzalishaji mdogo kwenye kundi la wazalishaji ingawa kahawa yake ni ya ubora wa juu na kupendwa sana.

Ethiopia imekuwa imara kwenye soko la zao la kahawa kwani wananchi wake wengi wanakunywa kahawa na hivyo kuzuia bei kuanguka na hivyo nchi kuweza kuwa na chapa yake yenyewe ya uhakika (brand).

Kwa mujibu wa TCB, wakulima walitarajiwa kuzalisha tani 60,000 mwaka 2018/2019, kutoka tani 41,679 mwaka 2017/18. Hivi kufanya Utabiri wa uzalishaji wa kahawa kuwa utaongezeka kwa tani 18,000 mwaka huu 2019 ingawa utabiri mwingi wa awali haujawahi kupatia makisio yake na kuleta shaka kuwa zao hili linavushwa kwenda nje kimagendo haswa kutokea mkoani Kagera na Kilimanjaro. Ushahidi upo kwa kesi nyingi polisi na takwimu za zao kutokuwa sawa.


Kimsingi hali ya zao ni mbaya kwani wachezaji wengi wamekwisha kata tamaa juu ya hatima yake na kuchukulia kudidimia kwake kama ni hali ya kawaida kutokana na changamoto nyingi zilizopo na watu kukataa kubadilika.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji TCB Kimaryo, Uzalishaji duni wa mazao ni kigezo tosha cha kudidimia kwani kihistoria kuanguka uzalishaji katika miaka mitatu iliyopita mfululizo na hivyo kudai miche mipya.

Hali nzuri ya hewa
Hali ya hewa mwaka huu ni nzuri ingawa mwaka jana kulifuata ukame hivi basi mfumo mpya wa kukusanya na kuuza kahawa unatarajiwa kuboresha hali hiyo na kufanya ongezeko ingawa changamoto zake za kimasoko na utawala nazo zinaongezeka.


Ripoti iliyotumwa kwenye tovuti ya TCB inaonyesha kuwa ikiwa kiwango cha uzalishaji wa 2018/19 kitafikia, itakuwa kama ile ya 2015/16.
Inaonekana kuwa tatizo la upotevu kutokana magendo ni kubwa kwani kule Bukoba kahawa nyingi inatoroshwa na kwenda kuuzwa Uganda wakati Kilimanjaro hutoroshea kahawa yake kwenda Kenya na ile ya Kigoma huvushwa kimagendo kwenda Burundi na Kongo na kuacha nchi ikitegemea kahawa kutoka Wilaya ya Mbinga na hivyo kupungua nguvu kwenye soko la Afrika Mashariki.


Magendo yanaimarisha zaidi masoko ya nchi za jiranizinazotuzunguka; isitoshe kahawa nyingi, inauzwa bado ikiwa shambani, yaani kahawa mbichi kwenye mpango unaoitwa ‘buturo’ ambao ni biashara haramu kiserikali.


Bei ndogo kahawa
Bei ya kahawa duniani imepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na mavuno ya ziada (bumper ) katika nchi kubwa zinazozalisha, ikiwamo Brazil, Vietnam, Angola na Columbia kwa mujibu wa Bei ya Bidhaa ya Dunia ya Mwaka uliochapishwa na BoT.


Uchunguzi wake kiuchumi Septemba 2018 ulionyesha kuwa bei ya bidhaa za kila mwaka kwa kahawa ya Robusta iliongezeka kwa asilimia 31.6 wakati ule wa Arabica ulipungua kwa asilimia 16.0. Mifuko ya kahawa 36,010 ilitolewa katika mnada wa Kahawa Moshi mnamo Novemba 1, 2018 na mifuko ya kilo 28,305 ilinunuliwa, kulingana na TCB.


Bei ya wastani katika mnada Moshi ilikuwa chini ya Dola 5.38 / 50 kilo kwa Arabika Baridi ikilinganishwa na mnada wa mwisho uliofanyika Oktoba 25, 2018.

Kuongeza unywaji kahawa
Watunga chapa wengi wanafanya juhudi ya kuchanganya (blending) ili kupata hisia mpya kwenye kahawa ili kuongeza idadi mpya ya wanywaji na watumiaji kahawa kwa kuwapa kinywaji kipya na inaanza kuleta mafanikio chanya kwenye soko ingawa bado ni kidogo na hivyo soko hilo linahitaji kulelewa.

TCB imeshindwa kuimarisha maduka ya kunywa kahawa (coffee shops) nchini na kubakia na duka moja tu pale Extelcoms mtaa wa Samora.
Ukiachia kahawa asilia kizazi cha sasa hutaka zaidi kahawa ya mara moja (instant coffee) na ikiwezekana ni ile iliyochanganywa na maziwa na vionjo kama karafuu, hiliki, tangawizi au mdalasini na hivyo kupata ladha mpya. Ajabu hoteli kubwa zote wanauza kahawa ya nje na sio ya Tanzania!
Kati ya wajasiriamali waliochipukia kuziba ombwe yuko Nuru Coffee Chapchap na AfriCafe Three in One na hivyo kuingiza ladha mpya ya kizazi kipya cha wanywaji kahawa.

Wataalamu wa masula ya afya wamekuwa wakiwashauri watu kutumia kinywaji cha kahawa kutokana na faida nyingi wanazoweza kuzipata.
Matumizi ya kahawa nchini bado yapo chini sana na kwa mujibu wa Bodi ya Kahawa Tanzania ni asilimia saba tu ya kahawa inayozalishwa hapa ndiyo inatumika nchini.


Mkurugenzi wa kampuni ya Dar es Salaam Merchant Group, Rayton Kwembe ambao ni wasambazaji wa kinywaji cha Nuru Coffee chap chap. Tofauti na kahawa ya kawaida ambayo imezoeleka, Nuru Coffee imekuja na ubunifu wa aina yake ikiwa na vitu vitatu ndani yake.

Mkurugenzi huyo anasema, “Nuru coffee chapchap ni kinywaji kipya nchini Tanzania chenye mchanganyiko wa viungo vitatu yaani kahawa, maziwa, na sukari ndani ya pakiti moja.


Alipoulizwa ni nini kilichowafanya kuja na wazo la kuwa na kinywaji chenye vitu vitatu kwa pamoja alisema “maisha yamebadilika na mambo mengi yanakwenda kwa kasi.
Faida unywaji kahawa
Mkurugenzi huyo anadai watanzania watumie kahawa kutokana na umuhimu wake kwa afya zao na kukuza uchumi wao kwa kuacha kunywa pombe.


“Kahawa ina faida kubwa mwilini kwani huburudisha mwili, huchangamsha (wakati wowote hujisikia furaha), kufikiri kwa haraka na kutosahau, huongeza uwezo wa ufahamu kiakili.

Pia hupunguza uwezekano wa kupata magonjwa mbalimbali kama saratani, kisukari, kusahau, kupunguza unene na msongo wa mawazo,” aliongeza kuwa kahawa inapunguza kupata Kisukari, Diabetes Type 2 kwa maelezo ya Utafiti uliofanya na The American Chemical Society unaonyesha kuwa watu wanaokunywa vikombe 4 na zaidi kwa siku, wanapunguza uwezekano wa kupata kisukari kwa asilimia 50.


Rayton anasema kahawa inachangamsha mwili na ubongo kwa kufanya mzunguko mzuri wa damu hivyo husaidia usafirishwaji wa hewa ya oxygen mwilini na kwenye ubongo.


Inaimarisha uwezo wa kufikiri
Kwa kuwa kahawa inaongeza msukumo wa damu inasaidia ufanyaji kazi mzuri wa ubongo hivyo ni rahisi kufanya vitu kiumakini zaidi kwa kuimarisha afya ya ubongo, kutokusumbuliwa na usahaulifu na kuimarisha uwezo wa kufikiri pia.


Katika maeneo wanayolima kahawa zao hilo hutishiwa na mbogamboga, parachichi, matunda, vanilla na ndizi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles