NA ABDUCADO EMMANUEL, DAR ES SALAAM
KOCHA Mkuu wa timu ya Azam, Stewart Hall, amesema mchezo wao ujao dhidi ya JKT Ruvu unaotarajia kufanyika Alhamisi hii kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam utakuwa mgumu na kudai watakamiwa vilivyo na mshambuliaji Gaudence Mwaikimba.
Hall amesema hiyo inatokana na mshambuliaji huyo kuwahi kukipiga Azam FC kwa misimu mitatu kabla kutemwa msimu huu na kujiunga na JKT Ruvu.
“Kuna wachezaji wa Azam kama Mwaikimba atakayepambana vikali kutuonyesha kuwa bado yumo na ana mapenzi na Azam FC, hivyo itakuwa ni mechi ngumu,” alisema Hall, wakati akizungumza na MTANZANIA.
Mwingereza huyo alisema ugumu mwingine wa mchezo huo unatokana na Uwanja wa Karume ambao ni wa nyasi bandia kutokuwa na ubora ule wa mwanzo, hasa ardhi yake.
Aliongeza kuwa, mpaka sasa kikosi chake kipo safi, baada ya wachezaji waliokuwa na majeraha madogo, Farid Maliki, Michael Balou, Aishi Manula, walioukosa mchezo uliopita dhidi ya Ndanda FC kuanza mazoezi kwa ajili ya kuivaa JKT Ruvu.
Wakati Azam FC ikishika nafasi ya pili kwa pointi 19 kwenye msimamo wa ligi sawa na vinara Yanga, JKT Ruvu yenyewe inapumulia mashine kutokana na kujikusanyia jumla ya pointi mbili tu mpaka sasa katika mechi nane, huku ikiwa haijashinda mchezo hata mmoja.