25.5 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

Nassib Fonabo: Michel Teló wa ‘nosa nosa’ amenionyesha njia

FONABONassib Fonabo: Michel Telo wa ‘nosa nosa’ amenionyesha njia

NA FESTO POLEA

NAJUA unajua kwamba mshindi wa kwanza wa shindano la vipaji la Bongo Star Search ni Kayumba Juma aliyekuwa akiwakilisha Mkoa wa Dar es Salaam na amenyakua kitita cha Sh milioni 50, lakini sidhani kama unajua wa pili na watatu wamepata nini?

Walichopata ni hiki, aliyeshika nafasi ya pili, Nassib Fonabo anayetokea Mkoa wa Shinyanga lakini katika shindano hilo aliwakilisha Mkoa wa Arusha alipata Sh milioni 10 huku mshindi wa tatu, Frida Amani aliyetoka Arusha naye aliambulia Sh milioni tano.

Tuachane na walichokipata ninachotaka kuonyesha ni namna ambavyo mshindi wa pili wa shindano hilo, Nassib Fonabo, alivyoweza kuimba kwa ustadi wimbo wa ‘nosa nosa’ wa mwanamuziki wa Kibrazil, Michel Telo na ulivyoweza kumuonyesha njia ya mafanikio kupitia muziki wake.

‘‘Nilikuwa nikitumia wimbo wa ‘Ai Se Eu Te Pego!’ nosa nosa’ wa Michel Telo kwa kuwa naamini ni wimbo mzuri, wenye ladha na vionjo vitamu kwa mimi muimbaji na wasikilizaji pia naamini umeonyesha kipaji changu kwa wote waliofuatilia shindano hilo,’’ anasimulia Fonabo akidai kwamba alijitahidi kuubadilisha na kuufanya wimbo huo kuwa wake ndiyo maana anaamini umeonyesha njia katika maisha yake ya muziki.

Wimbo huo ulianza kujulikana katika nchi 15 tangu uliporekodiwa kwake mwaka 2011, ulijulikana na nchi nyingi duniani baada ya mchezaji wa timu ya soka la Barcelona na timu ya Taifa ya Brazil, Neymar, mchezaji wa Kihispania, Marcelo Vieira na mchezaji bora wa dunia anayechezea Real Madrid na timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo pamoja na mchezaji wa Kipoland, Adrian Mierzejewski, kucheza wimbo huo na video yake kuangaliwa na watu zaidi ya milioni moja.

Wimbo huo uliandikwa na Sharon Acioly na Antonio Dyggs, uliimbwa kwa lugha ya Kireno na Kiingereza ulizidi kujulikana baada ya baadhi ya wachezaji wa Brazil akiwemo, Ailton kuuimba wimbo huo akiwa katika kipindi cha TV nchini Ujerumani.

Baada ya hapo wimbo huo ulizidi kupanda chati na kupendwa na watu wa nchi za Ulaya, Latin Amerika na Israel ambapo uliweza kushika nafasi za juu katika chati mbalimbali.

Mwaka 2011 wimbo huo ulichaguliwa kushindania tuzo za Latin Grammy, ukiwakilisha albamu bora wakati huo ulikuwa namba 11 katika chati za Ujerumani, namba 10 Austria na namba mbili inchini Switzerland.

Haya ni mahojiano na Nassib Fonabo kwa baadhi ya vitu anavyofanana na mwanamuziki Telo.

Mtanzania: Telo aliyezaliwa Januari 21, 1981 huko Medianeira, Parana, alianza kuimba katika kwaya ya shuleni kwao mwaka 1987 akiwa na miaka sita tu, wewe umezaliwa wapi?

Fanabo: Nimezaliwa Shinyanga, nilikutana na uchaguzi wa BSS nikiwa nasoma chuo katika Chuo cha Makumira jijini Arusha ambapo kwa sasa naendelea na masomo ya shahada ya muziki.

Mtanzania: Telo alipotimiza miaka 10 nyota yake ya muziki ilianza kuonyesha dira baada ya baba yake kumpa zawadi ya kifaa cha muziki na alipotimiza miaka 12 majirani na ndugu zake walimshauri aanzishe bendi kwa kuwa alikuwa akijua kupiga baadhi ya vyombo, wewe je, safari yako ya muziki ikoje?

Fonabo: Mimi nilianza muziki nikiwa mdogo ingawa mazingira ya maisha yangu yalikumbwa na changamoto nyingi ikiwemo baba yangu kutokupenda shughuli zangu za muziki kwa kuwa haukuwahi kuonyesha faida tangu nilipoanza ambapo alitaka niendelee kwenye masomo tu niachane na muziki.

Lakini mama yangu alinipa moyo na alikuwa msaada mkubwa kwangu, lakini masikitiko yake makubwa ni kwamba nilitamani kipindi hiki baba yangu angekuwepo naye ashuhudie na kuusikiliza muziki wangu kwa kuwa alikuwa akinikataza kutokana na kutoona faida yake.

Mtanzania: Mwaka 1997 akiwa na miaka hiyo 12, Telo alijiunga na bendi iliyokuwa ikipiga nyimbo za asili ya kibrazil iliyoitwa, Grupo Tradição, miaka mitano alijifunza kupiga gitaa na kinanda alipoweza alirekodi albamu kadhaa akishiriki kuimba, kuandika na kuweka vikorombwezo, muziki wako umetoka wapi na ulijifunza gitaa kwa muda gani?

Fonabo: Baba yangu alifariki nikiwa mwaka wa pili nikisoma muziki katika Chuo cha Sanaa Bagamoyo ambapo nimehitimu stashahada ya muziki.

Gitaa nilianza kujifunza mwaka 2000 hadi leo naona kama bado naendelea kujifunza kupiga kwa kuwa naamini sijamaliza mipigo yote.

Mtanzania: Telo aliachana na bendi mwaka 2008, akiwa ameachia albamu ya mwisho aliyoiita ‘Micareta Sertaneja 2’, albamu ambayo ilimuwezesha kuingia katika tuzo za Latin Grammy kupitia kipengele cha muziki wa Kibrazil, wewe umeshawahi kupiga na bendi?

Fonabo: Mimi ni mmoja wa waanzilishi wa bendi ya The Spirit yenye makazi yake Bagamoyo mkoani Pwani, bendi hiyo ina wanamuziki sita.

Bendi hiyo inafanya maonyesho mbalimbali ndani na nje ya nchi ambapo hivi karibuni wakati nilipokuwa kambini BSS wezangu walikuwa wakitumbuiza katika tamasha la Bagamoyo lililofanyika katika Chuo cha Sanaa Bagamoyo.

Mtanzania: Telo baada ya kuachana na muziki wa bendi aliamua kufanya muziki wake binafsi ambapo albamu yake ya kwanza ya ‘Balada Sertaneja’ aliitoa mwaka 2009 ukiwemo wimbo unaotamba dunia kwa sasa wa ‘Ei, Psiu! Beijo, Me Liga,’ wewe na kundi lako mmewahi kutoa albamu?

Fonabo: Hapana kwa sasa nipo chini ya uongozi wa Tip Top Connection na hata kushiriki shoo nyingine kama Tusker Projest Fame, siwezi kwa kuwa nipo chini ya uongozi mwingine ninaoamini utatangaza jina langu na kazi zangu zijazo, lakini pia nitaongeza kipato kupitia muziki wangu.

Mwaka 2010 mwanamuziki Telo alitoa albamu nyingine aliyoiita ‘Ao Vivo’ ambayo ilishinda tuzo ya dhahabu ikiwa na wimbo wa ‘Fugidinha’ uliokuwa ukishika namba moja katika chati za nyimbo 100 nchini Brazil.

Naamini mwanamuziki huyo mchanga anaweza kufikia mafanikio ya Michel Telo kwa kuwa njia walizopitia wakati wa kutafuta mwelekeo wa muziki bora zinafanana, tofauti yao kubwa ni mazingira na nchi wanakotoka na ukubwa wa muziki wao pamoja na lugha wanazotumia. Nikutakie mafanikio mema katika safari yako ya muziki, Nassib Fonabo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles