Leonard Mang’oha-Dar es Salaam
MWANASHERIA Mkuu wa Serikali (AG), Dk. Aderladus Kilangi, amesema Serikali imewasilisha katika Mahakama ya Rufani kusudio la kukata rufaa kupinga hukumu ya Mahakama Kuu kuwazuia wakurugenzi (DEDs) kusimamia uchaguzi kwa niaba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Mei 10, mwaka huu, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, katika hukumu yake iliyotolewa na jopo la majaji watatu, Dk. Atuganile Ngwala, Dk. Benhajj Masoud na Firmin Matogolo ilibatilisha kifungu cha 7(1) cha Sheria ya Uchaguzi kinachoipa mamlaka NEC kuwateua wakurugenzi wa majiji, manispaa na miji kuwa wasimamizi wa uchaguzi.
Pia ilibatilisha kifungu cha 7(3) kinachoipa NEC mamlaka ya kuteua mtu yeyote miongoni mwa watumishi wa umma kuwa msimamizi wa uchaguzi.
Katika hukumu hiyo, mahakama ilisema vifungu hivyo ni kinyume cha Katiba ya nchi ikibainisha kuwa wakurugenzi hao huteuliwa na rais aliyeko madarakani, ambaye hutokana na chama tawala na kwamba wengine ni wanachama wa chama cha mamlaka inayowateua jambo ambalo huathiri utendaji wao katika kutenda haki.
Pia ilisema sheria haijaweka ulinzi kwa NEC kumteua mtumishi yeyote wa umma kuhakikisha kuwa anakuwa huru katika kutekeleza majukumu yake.
Uamuzi huo wa Mahakama Kuu umetokana na kesi iliyofunguliwa na mashirika kadhaa ya wanaharakati kupitia kwa mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Bob Wangwe, akitetewa na Wakili Fatma Karume.
Jana katika mkutano na waandishi wa habari, Dk. Kilangi alisema tayari Serikali kupitia kwa Wakili Mkuu wa Serikali (SG) imewasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa kupinga hukumu hiyo.
Dk. Kilangi alisema hata hivyo kuwepo kwa hukumu hiyo hakutaweza kuathiri chaguzi nyingine zijazo zikiwemo za marudio, kwani baada tu ya kuwasilisha taarifa hiyo ya kusudio la kukata rufaa utekelezaji wa hukumu hiyo husimama, hadi pale rufaa ya Serikali itakapoamriwa.
Alisema katika shauri lililokuwa Mahakama Kuu, Serikali ilipinga madai ya walalamikaji kuwa hayakuwa ya msingi
“Kwenye maelezo ya utetezi, Serikali kupitia Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ilitoa hoja zifuatazo: Kuhusu kifungu cha 6(1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi sura ya 343 kinachompoa mamlaka Rais aliyekuwepo madarakani kuteua Mkurugenzi wa Uchaguzi kutoka katika utumishi wa umma, Serikali ilieleza kuwa kifungu hicho hakikinzani na ibara ya 21(1), 21(2) na 26(1) ya Katiba.
“Katiba ya Jamhuri na Sheria ya Taifa ya Uchaguzi imeweka misingi na utaratibu wa uteuzi wa Mkurugenzi wa Uchaguzi na kuwa mkurugenzi huyo atatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa masharti yaliyomo kwenye Katiba, sheria ya uchaguzi na kanuni zinazoongoza uchaguzi.
“Kuhusu kifungu cha 7(1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi kinachowataka wakurugenzi wa majiji, manispaa, miji na halmashauri za wilaya kusimamia chaguzi kwa madai kuwa kifungu hicho kinakinzana za ibara ya 21(1), 21(2) na 26(1), Serikali ilieleza kuwa Katiba kama sheria mama imetoa fursa kwa Bunge kutunga sheria mbalimbali na kwamba uteuzi wa mkurugenzi wa uchaguzi unaofanywa na Rais unazingatia sheria za nchi,” ilieleza taarifa hiyo.
Awali kesi hiyo ilikuwa inasikilizwa na jopo la majaji watatu, wakiongozwa na aliyekua Jaji Kiongozi, Ferdinand Wambari, ambaye kwa sasa amehamishiwa Mahakama ya Rufaa, Jaji Rehema Sameji, ambaye pia yupo Mahakama ya Rufaa na Jaji Temba aliyestaafu.
HUKUMU ILIVYOKUWA
Akisoma hukumu hiyo wiki iliyopita, Jaji Atuganile Ngwala, alisema kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi, kifungu namba 7(1) na 7(3) ni batili kwa sababu kinatoa nafasi kwa wateule wa Rais ambao pia si waajiriwa wa NEC kusimamia uchaguzi.
Alisema kifungu cha 7(1) kinasema kuwa kila Mkurugenzi wa Jiji, Manispaa na Halmashauri anaweza kusimamia uchaguzi wakati viongozi hao ni wateule wa Rais na si waajiriwa wa NEC wakati Katiba inasema NEC inapaswa kuwa huru na haki.
Jaji Ngwala alisema kutokana na hali hiyo, kifungu hicho kinakinzana na Katiba mama ambayo inasimamia nchi.
Alisema lakini pia kifungu cha 7(3) kinasema kuwa NEC inaweza kuteua mtu yeyote kuwa msimamizi wa uchaguzi bila ya kuainisha ni mtu wa aina gani.
Jaji Ngwala alisema lakini Katiba inasema kuwa mtu yeyote aliyekuwa msimamizi wa uchaguzi hapaswi kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa.
Alisema kutokana na vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapo na upande wa waleta maombi, vimeonyesha pasi na shaka kuwa wasimamizi wa uchaguzi wana masilahi na wateule wao.
Kutokana na hali hiyo, alisema mahakama imeona kuwa vifungu hivyo ni batili na kwamba havifai kutumika wakati wa kusimamia uchaguzi.
“Mahakama imebatilisha vifungu vya Sheria ya Uchaguzi namba 7(1) na 7(3) kutokana na NEC kuteua wakurugenzi wa Jiji, halmashauri na manispaa kuwa wasimamizi wa uchaguzi wakati ni wateule wa Rais na si waajiriwa wa NEC,” alisema Jaji Ngwala.