TEHERAN,Iran
RAIS Hassan Rouhani, amesema kwamba taifa hili linakabiliwana shinikizo kubwa la kimataifa kutokana na vikwazo ambavyo limewekewa na Marekani na washirika wake.
Akizungumza jana mjini hapa, kiongozi huyo alisema kuwa kuendelea kuwekewa vikwazo hivyo na Marekani kumesababisha hali mbaya kiuchumi kuliko hata iliyotokea wakati wa vita na majirani zake Irak iliyodumu kuanzia mwaka 1980 hadi 1988.
Kauli ya kiongozi huyo imekuja wakati hali ya sintofahamu ikiwa inazidi kuongezeka, baada ya wiki iliyopita Marekani kupeleka na ndege na meli za kivitaka katika ukanda wa Ghuba.
Katika hotiba yake hiyo Rais Rouhani,ambaye anakabiliwa na shinikizo la kisiasa nchini alitoa wito wa kuwapo umoja kisiasa ili kuvishinda vikwazo hivyo.
“Wakati wa vita hatakuwa na matatizo katika benki zetu, mauzo ama ununuzi wa mafuta na tulikuwa na kikwazo kimoja cha kununua silaha,”Rais Rouhani aliwaambia wanaharakati wa kisiasa mjini hapa.
“Shinikizo la maadui ni vita ambavyo haijawahi kutokea katika historia ya mapinduzi yetu ya Kiislam.Lakini siwezi kukata tamaa na nina matumaini makubwa kwa siku zijazo na kuamini kwamba tunaweza kusonga mbele katika hali hii ngumu tukiwa tu umoja,” aliongeza rais huyo.
Kuongezeka kwa mvutano huo kati ya Marekani na Iran kumezua pia maswali kuhusu mustakabari juu ya siku zijazo kuhusu mkataba kihistoria wa nyuklia uliosainiwa mwaka 2015 kati ya nchi hii na nchi wanachama watano wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Ujerumani.
Mwaka jana Rais wa Marekani,Donald Trump mwaka jana alipitisha upya kuendelea kwa vikwazo ilivyowekewa nchi hii na pia inaonesha wazi Iran inaweza pia kuanza shughuli za nyuklia kama washirika wengine wataungana kutekeleza vikwazo hivyo vya Marekani.