NA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM
TIMU ya Yanga imeonekana kuingiwa mchecheto kuelekea mchezo ujao dhidi ya Mwadui, baada ya kuondoka na wachezaji wote wa kikosi hicho hata wale waliokuwa majeruhi.
Mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wanaelekea mkoani Shinyanga leo kwa ajili ya mchezo huo muhimu utakaofanyika Uwanja wa Kambarage keshokutwa, huku wakiwa wamepania kuibuka na ushindi.
Mmoja ya wachezaji aliyekuwa majeruhi na anaondoka na kikosi hicho ni kiungo Salum Telela, huku wengine Mbuyu Twite na Kelvin Yondani wakiwa wameanza kufanya mazoezi mepesi.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Ofisa Habari wa timu hiyo, Jerry Muro, alisema wameamua kuondoka na jeshi zima kutokana na timu hiyo kukabiliwa na michezo miwili ikiwa mkoani humo, mwingine ukiwa ni dhidi ya Kagera Sugar utakaofanyika Oktoba 31, mwaka huu.
“Hatumbakizi mchezaji hata mmoja, wote wataondoka na timu hata waliokuwa na majeruhi, kwani huenda hali zao zikaimarika wakiwa huko na hata kama wapo watakaoukosa mchezo huu na Mwadui basi watapata nafasi ya kucheza mchezo unaofuata, kwani bado tuna muda mrefu,” alisema.
Muro aliongeza kuwa mkakati wao wa ushindi upo palepale, kwani malengo yao ni ya kupata ushindi kwa kila mchezo, hivyo kila mchezo ni muhimu kwao.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa mgumu sana, hasa kutokana na mwenendo mzuri wa timu hizo mbili, Yanga ikiwa kileleni kwa pointi 19 itataka kushinda ili kumkimbia Azam FC inayolingana nayo kwa pointi, wote wakiwa hawajapoteza mechi yoyote mpaka sasa.
Mwadui, inayonolewa na kocha mzoefu wa ligi hiyo, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, ipo katika nafasi ya sita kwenye msimamo ikiwa na pointi 14, ambapo haijapoteza mchezo wowote mechi zake tano zilizopita.