Na Ibrahim Yassin
-Momba
KATIBU Tawala wa Wilaya ya Momba mkoani Songwe, David Kafulila, ameipongeza Halmashauri ya Mji wa Tunduma kwa ukusanyaji mzuri wa mapato huku akiiponda ile ya Momba ambayo imekuwa ya mwisho kitaifa kwa ukusanyaji mapato.
Kafulila aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani katika halmashauri ya Tunduma.
Alisema vikao vya Baraza la Madiwani Tunduma vimekuwa na mijadala mikali kuliko halmashauri zote na sasa imekusanya vizuri mapato huku akiwataka waendelee na kuvuka lengo kwani mji huo ni wa kibiashara kutokana na kupakana na nchi zaidi ya tano.
Alisema asilimia 71 ya mizigo inayovushwa bandari ya Dar es Salaam kutoka nchi za Ulaya, Asia na Amerika hupita hapo hivyo endapo watendaji na madiwani wataongeza ubunifu mapato yataongezeka mara dufu na kuufanya mpaka huyo kuwa na umuhimu mkubwa kwa Taifa hili.
“Hongereni sana madiwani na watendaji kwa makusanyo mazuri, Tunduma ni kama Singapore ya Tanzania, mmepata hati safi na mnaongoza kimkoa kwa makusanyo ya mapato, lakini bado mna kazi kubwa kuhakikisha mnavuka malengo na kuwa wa kwanza kitaifa,” alisema Kafulila.
Alisema Tunduma kwa robo hii imekusanya zaidi ya asilimia 79 wakati Halmashauri ya Momba imekusanya asilimia 31 na imekuwa ya mwisho kitaifa.
Zaidi alisema Halmashauri ya Momba imekuwa ikishika mkia mara kwa mara na hali hiyo imetokana na makusanyo yao kutoingizwa kwenye mfumo.
Ally Mwafongo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Tunduma, alisema wameupokea ushauri huo na kusisitiza kuwa wapo tayari kuongeza mshikamano na ushirikiano ili wavuke lengo la ukusanyaji mapato na kuwa wa kwanza kitaifa katika ukusanyaji.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Momba, Adrian Jungu, alipotafutwa kwa njia ya simu kuzungumzia sababu ya kuwa wa mwisho kitaifa kwa ukusanyaji mapato simu yake haikupatikana.
Mathew Chikoti, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Momba, alikiri kushika mkia lakini alisema kabla ya kumaliza mwaka huu wa fedha watajitahidi kufikisha asilimia 100 ili waondokane na aibu hiyo.
Uongozi wa Halmashauri ya Momba umekuwa ukilalamikiwa kwa utendaji usioridhisha baada ya kutowalipa posho za mwezi kwa zaidi miezi ya 15 madiwani hali iliyozua mgogoro kati ya Mkurugenzi Adrian Jungu na madiwani.
Licha ya uongozi wa CCM kuingilia kati lakini bado madiwani hao hawajalipwa.