25.6 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Mke wa Gwajima: Namjua mume wangu kuliko yeyote

ELIZABETH HOMBO Na  LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM

SIKU moja baada ya kusambaa picha na video ya ngono ikionyesha sura ya Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, akiwa faragha na mwanamke ambaye hajafahamika, mke wa kiongozi huyo wa dini, Grace amesema anamfahamu mume wake kuliko mtu yeyote.

Mke huyo wa Gwajima alitoa kauli hiyo jana mara baada ya mumewe kumaliza kutoa ufafanuzi wa video hiyo kwa waandishi wa habari, ambapo baadaye waumini wake waliokuwepo katika mkutano huo walisikika wakisema; “tunataka mama naye azungumze”.

Baada ya kelele hizo za waumini, Askofu Gwajima alimtaka mke wake asimame ili waumini hao wasikie chochote kutoka kwake.

Kutokana na hilo, Grace alisema anafahamu ukweli wa video hiyo na kamwe haiwezi kumyumbisha mume wake kwa maelezo kuwa anamfahamu vyema mumewe.

“Mimi ni jasiri kama simba, ukweli naufahamu, namfahamu mume wangu na kumwamini na ukweli huo hakuna mtu anayeweza kuubadilisha.

“Nipo pamoja na mume wangu na nitasimama na yeye. Mungu akiwa upande wetu hakuna atakayeweza kuwa juu yetu,”alisema Grace huku mamia ya waumini wa kanisa hilo wakishangilia na kupiga vigelegele.

Awali, Askofu Gwajima ambaye aliambatana na baadhi ya maaskofu wa madhehebu mbalimbali, alisema video hiyo imetengenezwa na mahasimu wake kwa lengo la kumchafua na kumnyamazisha.

Pamoja na mambo mengine, pia aliihusisha video hiyo na Uchaguzi Mkuu wa 2020 akisema watu wamedhamiria kumchafua na kumnyamazisha, lakini kamwe hatarudi nyuma.   

“Mahali ambapo napaswa kusema, lazima niseme watu wakijaribu kuleta matukio ili nisiseme tena nitasema na safari hii itakuwa kali kuliko ile ya zamani. Na utajua kwamba Mungu yupo.

“Kwa hiyo hizi image zinajaribu kuleta wasichana mbalimbali ninaomba kila mtu atumie akili yake kwamba ni mwanaume gani mwenye hadhi kubwa akarecord mwenyewe kitendo cha kujamiiana halafu mkono wake ni mkubwa wa baunsa ananyoosha mkono anarecord, hakuna mtu mjinga wa aina hiyo duniani.

“Haiwezekani mwili uwe wa mwingine kichwa kiwe cha mwingine, ukiangalia tu kwamba ameweka image mbili ya kwanza picha za familia ambayo niko kifua wazi…nimepiga picha za familia nyingi za namna hiyo mfano mojawapo ni hii (anaonyesha picha aliyopiga kifua wazi akiwa na mkewe na watoto).

“Image zinazotumika ni za familia sasa ninajua uchaguzi unakuja ni mwaka kesho, watu wana wasiwasi kwamba huyu bwana anaweza kuwa na nguvu za kutupasua vipande vipande, hivyo tumpunguzie sauti yake kabla mwaka kesho haujafika sasa hampunguzii sauti mtu hapa.

“Isipokuwa ulichosaidia umewathibitishia watu kwamba mimi ni mwanaume kamili kwamba tendo la ndoa naweza kufanya sawa sawa, kwa sababu kila mwanaume mwenye akili timamu huwa ana viungo kamili ana mtu wake huwa wanakutana kufanya tendo la ndoa tofauti huwa wanafanya chumbani.

“Shida ni kwamba vitu hivi vinafanywa kwa siri chumbani sasa mtu akivibeba kwa ajili ya kumdhalilisha akabadilisha akaweka bandia hapo ndipo haiwezi kukubalika,”alisema Askofu Gwajima.

 “Kwanza nilishangaa kusikia kuwa Gwajima ameitwa polisi saa tano, mimi ninajiuliza kama mtu umepata ajali, umegongwa na gari ukakatika mguu wewe uliyekatika mguu ndiyo unatakiwa uende uripoti polisi jambo hili wala halina maana yoyote.

“Tayari nimechukua RB a na kuwaambia TCRA (Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania) wamtafute mtu anayejiita Original huko Instagram maana ndiye alianza kuisambaza hapa ndio nitajua ile sheria ya mtandao inafanya kazi kwa sababu siwezi kuchafuliwa mimi sheria ya mtandao isifanye kazi halafu akichafuliwa mwingine sheria ifanye kazi itawezekanaje mtu anichafue halafu asipatikane.

“Kila silaha itakayofanyika juu yangu haitafanikiwa. Nitasema kuliko nilivyosema zamani nitasema zaidi ya hapo na sio kwamba najiandaa kufa, sifi  naongea kwa ujasiri, hafi mtu, halogwi mtu wala hatekwi mtu.

“Nimeona kuliko kukaa kimya kwa sababu  nilishamfuatilia aliye nyuma ya mambo hayo, ninamuonya asipofanya inavyotakiwa kufanya nitaanza kumgawia vitu vyake Jumapili hii, narudisha Jumapili zile ambazo watu walikusanyika hapa.

“Mtapata updates naifanyia kazi na nimekaribia mwishoni nitaeleza ni nani na kwanini na aliyefanya haya yupo hapa Tanzania na ni yule yule ambaye anatakiwa asagwe sagwe vipande vipande na atapotea mara nyingine tena. 

“Unajua kwenye nchi hii kuna mambo yanaendelea yenye lengo mbaya na nchi, mfano mlimsikia Rais anashangaa Mohamed Dewji alivyotekwa akaja akapatikana na waliomteka wakaacha silaha na gari halafu inaishia hapo hapo na ni kimya mpaka leo.

“Lazima tuelewe kuna matukio yanafanywa na mtu anayeongoza watu na inakuja kuonekana serikali ya Tanzania ndio inafanya haya lakini kuna individuals kuna baadhi ya watu wajinga, wapuuzi wanachafua taswira ya nchi,”alisema kiongozi huyo dini.

Alisema Jumapili ya wiki hii patachimbika kanisani kwake, endapo aliyetengeneza video hiyo hatafanya inavyotakiwa afanye.

Polisi yaanza uchunguzi

Akizungumzia video hiyo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema jeshi hilo kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) wameanza uchunguzi wa picha na video ya ngono inayosambaa kwenye mitando ya kijamii inayodaiwa kuwa ni ya Askofu Josephat Gwajima.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana Kamanda Mambosasa alisema Mei 7, mwaka huu video na picha za ngono zinazodhaniwa kuwa ni za Askofu Gwajima zilisambazwa katika mitandao ya kijamii zikimwonesha akifanya ngono na mwanamke asiyefahamika. “Jeshi la Polisi limeanza uchunguzi wa picha na video hiyo ya ngono mara moja na linapenda kuwataarifu wananchi kuwa Gwajima sio mtuhumiwa bali ni mwathirika wa tukio hilo, kwani jambo hili linaweza kufanywa na mtu yeyote kwa nia wa kumuharibia heshima yake kwa jamii na waumini wake,” alisema Mambosasa

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles