23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Kilimanjaro, Arusha zazizima

Na Upendo Mosha-Hai

WANANCHI wa mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, jana walijitokeza kwa mamia kuupokea mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Dk. Reginald Mengi, ulipowasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na kuusindikiza hadi walayani Hai.

Mara baada ya kuwasili kwa mwili huo katika uwanja huo saa 3:40 asubuhi, ulipokewa na viongozi mbalimbali wa kiserikali, dini na mamia ya wananchi.

Msafara uliokua umebeba mwili wa marehemu uliondoka uwanjani hapo saa 4:15 na ulipita katika barabara ya Moshi/Arusha mpaka ulipofikishwa katika Kijiji cha Mkweseko wilayani Hai.

Baadhi ya wafanyabiashara walifunga biashara zao ili kupata kuaangalia mwili huo ukipita huku mamia ya wananchi wakiwa wamesima pembeni mwa barabara na wengine wakiwa wamebeba majani ya masale wakiyapunga kuonyesha ishara ya kuaga.

Katika baadhi ya maeneo, wananchi  walitandika  kanga barabarani ili gari lenye mwili lipite juu yake.

Pia kulikuwa na baadhi ya wananchi waliokuwa wakishinikiza jeneza hilo litolewe kwenye gari na walibebe kwa mikono jambo ambalo hawakufanikiwa kutokana na kudhibitiwa na polisi.

Msafara huo wakati ukipita maeneo ya Kia, Bomang’ombe na Kwasadala, wananchi walikuwa wakitaka kuusimamisha lakini ulipofika Kijiji cha Nkwarungo, ulisimamishwa ili kupunguza magari yaliyokuwa kwenye msafara huo.

FAMILIA YAELEZEA RATIBA YA MAZISHI

Mkuu wa itifaki wa familia ya Dk Mengi, Wilfred Mushi, alisema ratiba ya awali ilibadilika kutoka ibada iliyokuwa ikitarajiwa kufanyika Machame na kuhamishiwa usharika wa Moshi Mjini katika Kanisala la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).

“Ibada ya mazishi ya mpendwa wetu tulitarajia kuifanyia Machame lakini tumepokea maombi mengi kwa wanachi wa Mkoa wa Kilimanjaro wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa Anna Mgwhira wakitaka tuhamishie Moshi Mjini kutokana na ukubwa wa eneo jambo ambalo familia imekubali”alisema

Kutokana na hali hiyo, alisema mwili utalala nyumbani kwa marehemu katika Kijiji cha Mkweseko ambapo leo utapelekwa kanisani Moshi Mjini kwaajili ya ibada kisha  utapelekwa katika Kijiji cha Nkuu Sinde Kata ya Machame alipozaliwa ambapo ndipo atakapozikwa.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa, anatarajiwa kuongoza wananchi watakaoaga mwili huo leo.

Majaliwa kuongoza maziko

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Annah Mgwhira, alisema pamoja na Waziri Mkuu, pia Spika wa Bunge Job Ndugai, mabalozi, mawaziri wa kuu wastaafu, mawaziri wa wizara mbalimbali, wabunge, wakuu wa mikoa na wilaya na viongozi was dini no viongozi watakao hudhuria mazishi hayo.

“Kuhusu suala la kiusalama kama mkoa tumejipanga kupokea viongozi wote na tunawahakikishia usalama was kutosha lakini wanachi nap wasiwe na hofu serikali inatarajia jambo hili litamalizika kwa utulivu na amani”alisema.

Ndoto za Mengi Kilimanjaro

Akizungumzia masuala ya uwekezaji, Mgwhira alisema, Dk. Mengi alipanga kufungua mashamba ya zao la Parachichi na kiwanda kipya cha Sukari.

Alisema kuufunguliwa kwa mashamba hayo na kiwanda hicho kulikua na matarajio ya kutoa ajira za watu zaidi ya 5,000 ambao pia ingekuwa ni frusa  ya kuinua uchumi wa mkoa wa Kilimanjaro na taifa kwa ujumla.

”Kama mkoa bado tuna matumaini na familia ya Dk Mengi kwamba wanauwezo wa kuendeleza wazo hilo ambalo tulishaanza kulikulifanyia kazi kama mkoa” alisema.

Alisema mara kadhaa alikua akifanya mazungumzo na Dk Mengi ambaye alisema anahitaji angalau Ekari kati ya 2,000 hadi 5,000 ambazo ni maalum kwa ajili ya vijana kupata kazi kwa takribani watu 3,000.

alisema mipango mingine ilikuwa ni kufungua kiwanda cha sukari eneo la Machine tools ambacho kingetoa ajira za watu wasiopungua 2000.

Alisema Dk Mengi hakuwa mtu wa kujivuna licha ya kuonekana ni tajiri na mwenye hadhi kubwa ndani na nje ya nchi.

Dkt. Mengi alifariki dunia alfajiri ya Mei 2, akiwa kwenye matibabu huko Dubai, Falme za Kiarabu.

Juzi Rais John Magufuli akiwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine wa Serikali, waliongoza maelfu ya wananchi kutoa heshima za mwisho wakati wa shughuli za kuaga mwili huo katika ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Salaam.

Hadi mauti yanamfika, Dk. Mengi alikuwa Mwenyekiti wa Wamiliki wa Vyombo Vya Habari Tanzania (MOAT). Pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (Tanzania Private Sector Foundation – TPSF).

Baadhi ya nyandhifa ambazo Dk. Mengi aliwahi kushika ni pamoja na Kamishna wa kamati inayoshughulikia mishahara (Salary Review Commission); Mwenyekiti wa Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi Tanzania (NBAA); Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mazingira Tanzania (NEMC); Mwenyekiti wa vyombo vya habari vya Jumuia ya Madola Tanzania (Chairman of the Tanzania Chapter-Commonwealth Press Union-CPU); Kamishna wa TACAIDS na Mwenyekiti wa Baraza la Biashara la Afrika Mashariki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles