LONDON, ENGLAND
KOCHA wa Manchester City, Pep Guardiola, amesema vijana wa kocha wa Liverpool, Jurgen Kloop, ndio pekee wamekuwa wakimuumiza kichwa tangu atue Ligi Kuu England.
Manchester City ipo kwenye mbio za kuwania ubingwa msimu huu dhidi ya Liverpool ambayo nayo ipo kwenye mbio hizo ikiwa imebakiza michezo miwili.
Kocha huyo wa zamani wa Barcelona na Bayern Munich, kwa sasa analiwinda taji la nane la Ligi Kuu lakini anaamini Liverpool imekuwa mshindani mkubwa tangu awe kocha licha ya kukabiliana na ushindani dhidi ya Borussia Dortmund na Real Madrid.
“Katika Ligi Kuu nilizocheza Liverpool imekuwa ikionyesha ushindani mkubwa kwangu tangu kuanza kazi hii ya ukocha. Kila ligi ukishinda ni jambo zuri lakini pia kuna ugumu wake hata hivyo Liverpool imekuwa ya kipekee.
“Tumepambana vya kutosha lakini ni ngumu kupata pointi 100. Lakini ni jambo gumu kuwa kwenye kiwango kinachofanana kila msimu,” alisema Guardiola wakati akihojiwa na runinga ya Sky Sports.
Guardiola amepanga kushinda taji la Ligi Kuu England kwa mara ya pili mfululizo ambapo itakuwa mara ya kwanza katika historia ya klabu ya Manchester City.
“Baada ya msimu uliopita kutwaa taji wachezaji wangu nyota bado walikuwa na hamu ya kutwaa tena taji hili.
“Huu ni mchezo wa soka, watu wanaokuja Uwanja wa Etihad msimu huu si kwa ajili ya kukumbuka soka la kupendeza la msimu uliopita. Huko tulishamaliza.
“Msimu ujao pia hautakuwa sawa kama msimu huu. Kama nikikaa hapa na kukumbuka yaliyopita nitafukuzwa haraka sana.
“Klabu kubwa kama hii kila siku inawaza kubadili makocha kwa kuwa kila msimu inataka kushinda mataji,” alisema Guardiola.