27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Wachambuzi wafunguka uteuzi wa Taifa Stars

ZAINAB IDDY -DAR ES SALAAM

WIKI iliyopita kocha wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Emmanuel Amunike, alitaja kikosi cha awali cha wachezaji 39, kwa ajili ya maandalizi ya fainali za Afrika (Afcon), zitakazofanyika nchini Misri kuanzia Juni 21 hadi Julai 19.

Mbali ya fainali hizo, kikosi hicho kitajiandaa na mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Misri, utakaochezwa Juni 13, mwaka huu Uwanja wa Borg El Arab, jijini Alexandria.

Akizungumzia wakati akitangaza kikosi hicho, Amunike, alisema pia amelenga kuwaandaa wachezaji aliowaita kwa ajili ya fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (Chan).

Afcon, Stars imepangwa Kundi C pamoja na jirani zao Kenya, Algeria na Senegal, wakati Misri ambao ni wenyeji wapo Kundi A pamoja na Zimbabwe, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Kundi B linaundwa na Burundi, Madagascar, Guinea na Nigeria.

Kundi D lina Namibia, Afrika Kusini, Ivory Coast na Morocco, wakati Kundi E, imo Angola, Mauritania, Mali na Tunisia huku Kundi F likiwa na Guinea Bessau, Benin, Ghana na mabingwa watetezi, Cameroon.

Ikumbukwe Taifa Stars imefuzu Afcon baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye Kundi L na kukusanya pointi zake nane, nyuma ya Uganda iliyoongoza kwa pointi 13, Lesotho iliyomaliza nafasi ya tatu na pointi sita na Cape Verde iliyokamata nafasi nne na pointi tano.

Tanzania itashiriki Afcon kwa mara ya pili tu katika historia, baada ya mwaka 1980 ilipofanyika nchini Nigeria ambako ilipangwa Kundi A pamoja na wenyeji Nigeria, Misri na Ivory Coast na kushika mkia.

Katika michuano ya mwaka 1980, Taifa Stars ilifungwa mechi mbili, kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Nigeria na kichapo cha mabao 2-1 ilichokipata kwa Misri kabla ya kutoa sare ya 1-1 na Ivory Coast na kuishia raundi ya kwanza, michuano hiyo ilishirikisha timu nane.

Kwa upande wa Chan, Taifa Stars itaanzia nyumbani dhidi ya Sudan Julai 26 kabla ya kurudiana Agosti 2 na ikifuzu mtihani huo itamenyana na mshindi kati ya Kenya na Burundi.

Walioitwa kwa Afcon

Makipa: Aishi Manula (Simba SC), Metacha Mnata (Mbao FC), Suleiman Salula (Malindi SC) na Aaron Lulambo (Tanzania Prisons), wakati kwa upande wa mabeki wapo, Claryo Boniface (U20), Hassan Kessu (Nkana FC, Zambia), Vincent Philipo (Mbao FC) na Shomari Kapombe (Simba).

Wengine ni Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni (Simba SC), Kelvin Yondani, Gardiel Michael (Yanga SC), Abdi Banda (Baroka FC, Afrika Kusini), Ally Mtoni (Lipuli FC), David Mwantika, Aggrey Morris (Azam FC), Ally Ally (KMC) na Kennedy Wilson (Singida United).

Viungo  wapo Feisal Salum, Ibrahim Ajibu (Yanga SC), Himid Mao (Petrojet, Misri), Frank Domayo, Mudathir Yahya (Azam FC), Jonas Mkude (Simba SC), Shiza Kichuya (ENNPI, Misri), Simon Msuva (Difaa Hassan El-Jadidi Morocco), Farid Mussa (Tenerife, Hispania) na Freddy Tangalu (Lipuli FC).

Washambuliaji wapo Yahya Zayd (Ismailia, Misri), Shaaban Iddi Chilunda (Tenerife, Hispania), Rashid Mandawa (BDF, Botswana), Ayoub Lyanga (Coastal Union), Kassim Khamis (Kagera Sugar), Miraj Athumani (Lipuli FC), Kelvin John (Serengeti Boys), Adi Yussuf (Solihull Moors, England), John Bocco (Simba SC), Thomas Ulimwengu (JS Saoura, ALgeria) na Nahodha Mbwana Samatta (KRC Genk, Ubelgiji).

Makocha, wachambuzi wa soka wametoa maoni yao baada ya kikosi cha Taifa Stars kutangazwa.

Kennedy Mwaisabula ambaye ni kocha na mchambuzi wa soka nchini anasifu uteuzi lakini anasema kikosi hicho  kinahitaji muda wa kutosha wa kukaa  pamoja kabla ya kwenda kwenye mashindano.

“Kikosi hakijabadilika sana na kile cha siku zote kinachoonekana hapa wachezaji wengi wameitwa baada ya kelele zilizokuwa zikipigwa na watu mbalimbali.

“Kuna wachezaji hawakustahili kuwepo katika kikosi na huenda wameitwa kwa kuwa watu wengi walihitaji wawepo, lakini kwa kuwa kocha ndiye mtu wa mwisho na mwenye maamuzi hatuna budi kumpa ushirikiano kwa manufaa ya Tanzania,” anasema.

Kwa upande wa Ally Mayay ambaye ni mchezaji wa zamani wa Taifa Stars na mchambuzi anasema: “Kikosi  kilichoitwa ni kizuri kwa kuwa ndicho kilichotuwezesha kufika Afcon.

“Hivi sasa Stars inahitaji mechi nyingi za kirafiki ili kujiweka kiushindani tofauti na hapo tunaweza kuwa washiriki tu na si washindani.”

Amunike anenaKocha Amunike anasema anahitaji mechi mbili ngumu kwa ajili ya kukiandaa kikosi chake kuelekea kwenye michuano ya Afcon.

“Nahitaji michezo miwili migumu kwa ajili ya kuandaa kikosi kuelekea kwenye michuano ya Afcon ambayo tumeweza kufuzu, tupo tayari kupambana na kupata matokeo ila ni lazima tupate mechi mbili.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles