25.8 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Dk Gwajima: Simamieni huduma za afya

Mwandishi Wetu- Njombe

SERIKALI imezitaka timu za uendeshaji huduma za afya za mikoa kuelekeza nguvu zaidi na muda zaidi katika kusimamia  shughuli zote za utoaji wa huduma bora za afya katika mikoa yao, badala ya kutumia nguvu na muda mwingi kukaa ofisini au kuwa safarini.

Agizo hilo limetolewa   jana mjini Njombe na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), anayeshughulikia afya, Dk. Dorothy Gwajima wakati akizungumza na timu ya uendeshaji huduma za afya ya mkoa wa Njombe.

Alisema jukumu kubwa la timu za usimamizi huduma za afya mikoa ni kuhakikisha kuwa timu za usimamizi huduma za afya halmashauri zinaimarisha usimamizi wa timu za uendeshaji huduma za vituo husika ili, zihakikishe huduma zinatolewa kwa ubora stahiki.

kupitia ufuatiliaji wa kina, timu za usimamizi wa afya mkoa na halmashauri  zinapaswa kupata mwenendo wa huduma kutoka vituo vyote na maeneo yote ya huduma za afya jamii kisha,  kufanya uchambuzi wa takwimu na taarifa hizo na kuzijadili ili, kutoa ushauri, mapendekezo, maelekezo ya kuwesha kuwa na mipango stahiki inayojibu hoja husika kwa wakati.

Alizikumbusha timu zote za usimamizi huduma za afya za mikoa na halmashauri kuwa, huduma za afya zinazotolewa katika vituo na katika ngazi ya jamii zina uhusiano wa moja kwa moja na umakini wa utendaji wa timu za afya za mikoa na halmashauri hivyo, watambue kuwa, wanalo jukumu kubwa la kuelekeza nguvu na muda wa kutosha katika kufuatilia utoaji wa huduma husika badala ya kutumia muda mwingi kukaa ofisini na kusafiri hata safari ambazo wanaweza kuwakilishwa.

Hivyo, amesema kipimo cha ubora, umahiri na tija ya utendaji wa timu za afya mkoa na timu za afya za halmashauri ni ubora wa huduma zinazotolewa ngazi ya vituo vya afya na siyo vinginevyo.

Kuhusu  upatikanaji wa huduma, Dk. Gwajima alisema imeendelea kuinua ubora wa huduma za afya kwa kujikita katika kuboresha maeneo mengi na baadhi yake ni ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya na kuongeza bajeti ya dawa.

Hivyo, jukumu la timu za usimamizi huduma za afya ni kufanya ufuatiliaji na usimamizi wa kina ili, juhudi hizi zizidi kuzaa matunda makubwa zaidi na kuondoa kero zinazoepukika hususan, matukio ya kukosekana kwa dawa yatokanayo na kutozingatia taratibu za manunuzi ya umma na tabia za baadhi ya watoa huduma kutumia dawa hizo bila kuzingatia Mwongozo wa Matibabu.

Alisema, tabia zinazokwamisha juhudi za Serikali zinachangiwa na baadhi ya timu za usimamizi huduma za afya mikoa na halmashauri kutoweka nguvu na muda wa kutosha katika kufuatilia mwenendo wa utoaji huduma katika vituo husika.

Alimtaka  Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Njombe, Dk.Thomas Ndailo kuongeza kasi ya kutimiza malengo ya kujenga kituo cha afya kwenye eneo lenye nafasi.

Dkt. Gwajima amesema, ana imani kuwa, watoa huduma walioko vituoni watafanya vizuri zaidi iwapo, timu za usimamizi huduma za afya mikoa na halmashauri zitaelekeza nguvu na muda wa kutosha katika kufuatilia utekelezaji unaofanyika katika vituo hivi, kuchambua takwimu na taarifa, kujadili, na kushauri na kuelekeza na siyo vinginevyo.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dk. Bumi Mwamasage aliahidi kusimamia kwa nguvu zote yote yaliyo elekezwa na kuhakikisha kuna uwajibikaji mkubwa zaidi wa timu zote za usimamizi huduma za afya katika halmashauri zote.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles