32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

JPM: subirini

Na WAANDISHI WETU DAR/MIKOANI

RAIS Dk. John Magufuli amewataka wafanyakazi kuendelea kuwa na subira katika suala la nyongeza ya mishahara kwani muda wake wa uongozi bado haujaisha.

Amesema angeweza kupandisha mishahara hata kwa Sh 5,000 lakini endapo tu atapandisha bidhaa zingeweza kupanda kwa bei ya juu.

Akizungumza jana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika Uwanja Sokoine mkoani Mbeya, alisema ataendelea kuboresha masilahi ya wafanyakazi na watumishi wengine kulingana na uwezo wa Serikali.

“Mwaka jana nilitoa ahadi kwamba kabla sijaondoka madarakani nitapandisha mishahara, lakini ni lazima tuelewe hadi sasa sijaondoka madarakani, uchumi wetu unakwenda vizuri na hatua tulizochukua zinawanufaisha wafanyakazi na Watanzania wote.

 “Naomba muamini kwamba subira yavuta heri, muda wangu bado haujaisha, ningeweza kusema naongeza mshahara hata kwa Sh 5,000 lakini kesho bidhaa zingepanda bei,” alisema Rais Magufuli.

Alisema kwa sasa Serikali imejielekeza kwenye miradi mikubwa ya maendeleo ambayo inawanufaisha wafanyakazi, wakulima, wafugaji, wavuvi na wafanyabiashara.

“Kupanga ni kuchagua, tungeweza kuchagua kwamba hakuna kuajiri tunaongezeana posho, ahadi yangu bado haijaisha, muda wangu wa utawala bado haujaisha na kwa mwelekeo unavyoenda na kwa miradi hii inayotekelezwa na kwa uchapakazi unaofanywa na wafanyakazi, wakulima, wafanyabiashara, tunaelekea kuzuri,” alisema.

Alisema gharama za kuendesha Serikali bado ziko juu kwani kila mwezi Sh bilioni 580 zinatumika kulipa mishahara, lakini bado kuna madeni ya mikopo, miradi ya maendeleo na matumizi mengine.

“Kiasi kidogo kinachobaki ndio tumekuwa tukijiuliza tukipeleke wapi na baada ya kutafakari kwa kina tuliona ni busara tutumie kukiwekeza kwenye miradi ya maendeleo itakayoongeza ajira nyingi za wafanyakazi na kukuza uchumi kwa nguvu kubwa zaidi,” alisema.

Alifafanua kuwa fedha nyingi zimekuwa zikitumika katika miradi ya ujenzi wa reli ya kisasa, barabara, ukarabati na ujenzi wa meli mpya katika maziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa, upanuzi wa bandari mbalimbali, upanuzi viwanja vya ndege 11 na ununuzi wa ndege mpya nane.

Hata hivyo alisema kutokana na Serikali kuwajali wafanyakazi, ndiyo maana aliamua kusitisha kikokotoo cha malipo ya pesheni kilichokuwa kinawaumiza.

Alimwagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, kuhakikisha bodi za mishahara zinakutana, lakini akatahadharisha vikao hivyo visiwe kichocheo cha kutumia vibaya fedha za Serikali.

“Binafsi sina tatizo na bodi za mishahara kukutana na sielewi kwanini hazikutani, hata wakitaka kukutana leo sina shida wala sina tatizo,” alisema.

Kuhusu kodi ya mishahara (PAYE) alisema bado wataendelea kujadiliana kwa watumishi wa ngazi nyingine.

“Kama tuliweza kushusha kutoka asilimia 11 hadi 9 kwa watumishi wa kima cha chini, bado tunaweza. Jambo la muhimu ni TUCTA na wafanyakazi kutambua kuwa Serikali ina sababu za msingi za kutofautisha viwango vya kodi,” alisema Rais Magufuli.

Alitoa wito kwa waajiri wote kuhakikisha wanazingatia sheria za kazi, ikiwamo ya usalama na afya mahala pa kazi, kutoa mikataba ya ajira na kuruhusu uwepo wa vyama vya wafanyakazi.

MADAI

Rais Magufuli alisema watumishi 505,985 wamelipwa Sh bilioni 72.8 na kati ya hizo Sh bilioni 37.2 zimelipwa kwa walimu 270,878 na Sh bilioni 35.7 zimelipwa kwa watumishi wengine 235,107.

Alisema pia Sh bilioni 75.5 zimelipwa kwa watumishi 50,386 na kati yao walimu 28,115 wamelipwa Sh bilioni 27.9 na Sh bilioni 9.5 zimelipwa kwa wastaafu 1,829 waliokuwa wakiidai Serikali kwa muda mrefu.

Hata hivyo alisema mwaka jana watumishi 118,989 walipandishwa madaraja kwa gharama ya Sh 29.5 na walimu 75,502 walilipwa Sh bilioni 16.3.

“Watumishi wengine wasio walimu 43,487 wamelipwa Sh bilioni 13.2 na mwaka ujao wa fedha tutapandisha madaraja watumishi 193,166,” alisema Rais Magufuli.

Alisema pia walilipa Sh bilioni 291.3 ambazo si madai ya misharaha yaliyokuwepo kwa zaidi ya miaka 10. 

Rais Magufuli alisema Sh trilioni 1.5 zimelipwa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii ambayo ilikuwa ikidaiwa Sh trilioni 1.6 kwa kushindwa kupeleka michango ya watumishi tangu mwaka 2012/2013.

Kuhusu watumishi wapya, alisema wameajiri 42,755 wanaolipwa Sh bilioni 25.8 na kwamba mwaka ujao wa fedha wamepanga kuajiri wengine wapya 45,000.

MABANGO

Maandamano ya wafanyakazi yaliambatana na ujumbe tofauti ambao ulijikita katika masuala ya utawala bora, masilahi bora kwa wafanyakazi na mishahara, jitihada za kujenga hospitali, vituo vya afya, mifuko ya plastiki, haki sawa kwa wote na uchumi wa viwanda.

Ujumbe mwingine ni Tanzania ya uchumi wa kati itajengwa na wafanyakazi, Tukitaka kuelimisha Tanzania ni lazima kuwaelimisha Watanzania, Tunaomba uondoe unyonge wetu kwa kutuongezea mishahara iendane na mabadiliko ya gharama za maisha.

Rais Magufuli alisema alivutiwa na baadhi ya mabango ya wafanyakazi hasa yaliyokuwa na ujumbe wa nyongeza ya mshahara, lakini akawataka wafanyakazi kuwa na subira.

“Nimesoma bango moja linasema ‘Tupandishe madaraja ili nasi tupande bombadier’. Limeandikwa kitaalamu kweli, nawapongeza sana,” alisema Rais Magufuli.

WAZIRI WA KAZI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu), Jenista, alisema wataendelea kushirikiana baina ya waajiri na wafanyakazi ili kupunguza migogoro na maandamano yasiyokuwa na tija.

Jenista alisema Serikali itaendelea kuwa pamoja na kuwatetea wafanyakazi kwa kuhakikisha wanafanya kazi wakiwa salama na kupata stahiki zao kwa mujibu wa taratibu na sheria za ajira.

Alisema wameondoa tozo mbalimbali zilizokuwa zikitolewa kwa kufuta baadhi ya faini zilizokuwa kikwazo kwa wafanyakazi.

“Tozo ya ushauri wa kitaalamu imeondolewa kwani ilikuwa ikitozwa kwa saa Sh 450,000 na ilikuwa ni gharama kubwa kwa waliokuwa wakipatiwa ushauri huo,” alisema.

Alisema baada ya kuondoa tozo hiyo wafanyakazi wameweza kujiunga hadi kufikia zaidi ya 8,000 kutoka 2,000.

“Tutaendelea kushirikiana na wafanyakazi kuhakikisha wanapata stahiki zote kutoka kwenye Serikali ili kuhakikisha kazi zinafanyika na watumishi waendelee kufanya kazi kwa moyo wote,” alisema Jenista.

TUCTA

Katibu Mkuu wa TUCTA, Dk. Yahya Msigwa, alisema miundo ya utumishi katika baadhi ya mashirika haijapitishwa na kuzuia nyongeza za mishahara kwa watumishi.

Kuhusu kodi kwenye mishahara alisema kiwango cha asilimia 9 hakijawagusa wafanyakazi wote kwani wanaouguswa ni wale wenye mishahara ya kuanzia Sh 170,000 hadi Sh 325,000.

Aliiomba Serikali kuhakikisha maeneo yote ya kazi yanakuwa bora na salama kwani kuna baadhi ya maeneo hayazingatii sheria ya usalama kazini.

Kuhusu watumishi wenye elimu ya darasa la saba, alisema baadhi ya watumishi kutoka Kituo cha Elimu Kibaha na Serikali za Mitaa walirudishwa kazini, lakini hadi sasa hawajalipwa mishahara na stahiki zao zilizokuwa zimesimamishwa.

“Tunaiomba Serikali watumishi wote wa darasa la saba waliokuwa wameajiriwa serikalini warudishwe kazini na kulipwa stahiki zao,” alisema Dk. Msigwa.

Tucta pia ilipendekeza ili kukuza uchumi na kuongeza fursa za ajira, kuongezwa bidii kwenye ujenzi wa viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana nchini.

Alimwomba Rais Magufuli kununua meli kubwa za mizigo kuwezesha mabaharia wa Tanzania kupata ajira na ikishindikana Serikali iingie mikataba na meli zinazoleta mizigo nchini.

Naye Rais wa Tucta, Tumaini Nyamhokya, aliiomba Serikali kiwango cha kodi cha tarakimu moja kiwanufaishe wafanyakazi wote badala ya kuwanufaisha wenye kima cha chini cha mshahara.

“Tunaomba suala hili litekelezwe mapema ili tunapoanza mwaka mpya wa fedha sisi wafanyakazi tuanze kupata unafuu wa makato ya kodi katika mishahara yetu,” alisema Nyamhokya.

Akizungumzia nyongeza ya mishahara alisema; “Mheshimiwa Rais tunaamini kipindi chako cha utawala bado kipo, lakini tunatamani hata ikiwezekana leo (jana) mishahara ipandishwe.”

ZANZIBAR

RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, alisema Serikali itaendelea kujadili mfumo wa kuongeza masilahi stahiki kwa wafanyakazi nchini.

Akizungumza katika madhimisho ya Mei Mosi yaliyofanyika katika ukumbi wa Dk. Ali Mohammed Shein, Tunguu, Wilaya ya Kusini Unguja, alisema haki za wafanyakazi haziwezi kupatikana kwa  kuandamana kama inavyofanyika katika nchi nyingine.

Alisema hatua ya wafanyakazi kudai haki au masilahi yao kwa kuandamana si suala zuri kwani haliwezi kuimarisha hali za wafanyakazi kupata masilahi yao.

“Nyote ni mashahidi kwamba Serikali ya Awamu ya Saba imefanya mambo makubwa kwa wafanyakazi, sina haja ya kusema nikaja kuambiwa najigamba,” alisema Dk. Shein.

Alisema Serikali imefanikiwa kupandisha kiwango cha chini cha mshahara hadi kufikia asilimia 100 na kwamba lengo ni kulinda wafanyakazi wake kwa kuzingatia sheria ya usalama kazini.

“Kwa kuzingatia haki za wafanyakazi nchini, Serikali imepitia upya sheria za kazi ili kutoa tija kwa wafanyakazi kwa masilahi yao ya kila siku,” alisema.

Waziri wa Kazi, Uwezeshaji Wazee, Wanawake na Watoto, Moridline Syrice Castico, alisema mwaka 2018/2019 wizara imetoa elimu ya sheria kwa wafanyakazi wa Unguja na Pemba ili kutambua wajibu wao.

Alisema Serikali itasimamia utekelezwaji wa agizo la Dk. Shein kwa taasisi binafsi za Serikali kuhakikisha wanatoa kiwango cha chini cha mshahara cha Sh 300,000.

SIMIYU

Shirikisho la Vyama wa Wafanyakazi (Tucta) Mkoa wa Simiyu, limesema ni dhahiri kuwa halmashuari zimeshindwa na zinalemewa na mzigo mkubwa wa kulipa wafanyakazi wanaotegemea makusanyo ya ndani.

Shirikisho hilo limesema kwa sasa ulipaji wa mishahara kwa kutegemea makusanyo ya ndani ni msiba kwa wafanyakazi kutokana na halmashauri nyingi kutokuwa na uwezo.

Akizungumza jana wakati wa sherehe za Mei Mosi zilizofanyikia wilayani Maswa, Katibu wa Tucta Mkoa wa Simiyu, Said Mselemu, alisema wafanyakazi wamekuwa hawalipwi kwa wakati na wengine hukaa kati ya miezi miwili hadi mitatu bila kulipwa.

“Ni wakati sasa wa Serikali kuangalia upya huu mfumo, halmashauri zinalemewa, hazina uwezo hata kidogo, wafanyakazi wanateseka sana, wanakaa miezi miwili hadi mitatu bila kulipwa,” alisema Mselemu.

Alisema Serikali Kuu imezinyang’anya vyanzo vingi vya mapato halmashauri huku ikiziachia na mzigo mkubwa wa kulipa mishahara wafanyakazi wake.

Alisema pia wafanyakazi wengi wameendelea kudai malimbikizo ya madeni ya likizo, mishahara, safari, pamoja na uhamisho ambayo yamedumu kwa muda mrefu.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka aliwataka wakuu wa wilaya, wakurugenzi na wakuu wa idara kwenda kwa wajasiriamali kutoa vitambulisho vya ujasiriamali.

Aliwataka viongozi hao kutowaachia watendaji wa vijiji na kata kugawa vitambulisho hivyo na badala yake watoke ofisini na kwenda wenyewe vijijini kugawa kwa ufasaha.

TABORA

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Agrey Mwanri, ametoa wiki moja kwa waajiri wote kuhakikisha wanawapa mikataba ya ajira watumishi wao vinginevyo atawachukulia hatua za kisheria.

Alitoa agizo hilo jana wakati wa sherehe za Mei Mosi zilizofanyika kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.

Aliziagiza kampuni binafsi zikiwemo zile za kigeni zinazofanya shughuli zake mkoani humo kutii sheria za nchi zinazohusu masuala ya ajira hata kwa wale wanaofanya kazi za muda kama vibarua.

Mwanri aliwaonya waajiri wote wanaokwepa kutoa mikataba kwa watumishi wao na kuahidi kuwachukulia hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kusitisha mikataba yao ya kufanya kazi mkoani humo.

Pia aliwaonya waajiri wa sekta binafsi wanaowakataza watumishi wao kujiunga na vyama vya wafanyakazi kwa lengo la kutaka kuwapunja stahiki zao.

Akijibu risala ya Tucta, Mwanri aliagiza kupelekewa orodha ya watumishi ambao hawajapewa zawadi zao ili aweze kuwabana waajiri.

Tucta katika risala yao iliyosomwa na Alex Byangwamu, walidai kuwa wakurugenzi na waajiri wengine wamekuwa wakitaja zawadi kwa watumishi wao na kujichukulia umaarufu kama waajiri bora, huku wakijua hawana uwezo wa kutoa.

Kulingana na Tucta, hadi kufikia Juni 2017 watumishi wa Idara ya Elimu wanaidai Serikali madeni yasiyo ya mishahara Sh bilioni 1.8.

Walisema kitendo cha kutolipwa kwa madeni hayo kinawavunja moyo walimu ukiachilia mbali hatua ya kusimamishwa kupandishwa madaraja na vyeo tangu mwaka 2017.

LINDI

Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi, aliwataka watumishi wote katika nafasi zao kutimiza wajibu wao katika kuiletea nchi maendeleo.

Zambi ambaye alikuwa mgeni rasmi katika sherehe za Mei Mosi mkoani humo, aliupongeza uongozi wa Wilaya ya Kilwa kwa kutoa zawadi nzuri kwa wafanyakazi wake.

Katika sherehe hizo wafanyakazi bora kutoka wilaya mbalimbali walipewa zawadi zao ambapo katika Wilaya ya Kilwa kila mtumishi bora alikabidhiwa fedha taslimu Sh 500,000 na mfanyakazi bora wa jumla akikabidhiwa Sh milioni moja.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Renatus Mchau, aliwaasa watumishi kufanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo ambayo kila mmoja katika nafasi yake amekabidhiwa.

“Nawapongeza wale wote mliokabidhiwa zawadi lakini mkumbuke kuwa kila mmoja ana wajibu wa kufanya kazi kwa bidii ili kuleta mabadiliko chanya katika halmashauri yetu,” alisema Mchau.

Habari hii imeandaliwa na Nora Damian na Andrew Msechu (Dar), Eliud Ngondo (Mbeya), Derick Milton (Simiyu), Khamis Sharif (Zanzibar) na Murugwa Thomas (Tabora).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles