29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Njombe wageukia mauaji ya wazee, ndugu kubakana

ELIZABETH KILINDI-NJOMBE

Wakati zaidi ya watoto 10 wakiuawa mkoani hapa kutokana na imani za kishirikina, sasa mauaji hayo yamehamia kwa wazee.

Tangu Desemba mwaka jana, watoto takribani 10 wakiwamo watatu wa familia moja, waliripotiwa kuuawa kwa imani za kishirikina huku mauaji hayo yakihusishwa na imani za kishirikina.

Jana akiwa mkoani Njombe, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Simon Sirro, alikemea mauaji hayo aliyosema lazima yaishe huku akigusia namna ambavyo vitendo hivyo vimehamia kwa wazee.

Pia alisema Mkoa wa Njombe umekuwa na matukio mengi ya ubakaji ambayo pia yanahusisha ndugu.

 Sirro alisema watapambana usiku na mchana kuhakikisha wanamaliza mauaji hayo yanayosabishwa na imani za kishirikina.

 “Tuna shida bado ya matukio ya mauaji na nimetoa maelekezo kwamba lazima haya tuyamalize, wale wanaoyafanya kwa imani za kishirikina, wanaoyafanya kwa ugomvi wa mashamba na wale wanaoyafanya kwa ulevi, waache kwa sababu wataishia gerezani.

“Kuna tukio juzi lilitokea kwa sababu ya imani za kishirikina, mtu amekamatwa mzee mzima amekatwa kichwa na kupasuliwapasuliwa, ni mambo ya kishamba yaliyopitwa na wakati.

“Kwa hiyo nimeelekeza timu zetu maalumu za upelelezi kuhakikisha yule anayefanya mauaji anapatikana, lakini sio kupatikana tu, nasema siku zote kama unaua kwa upanga na wewe utauawa kwa upanga.

“Tumeona kuna shida iko Njombe na tunasema tutakuja kwa nguvu zote kuhakikisha haya matatizo yanapungua na yatapungua kwelikweli.

“Naomba wana-Njombe watuelewe hilo kwa sababu unapopunguza kuna watu wataumia na wataumia kwa mujibu wa sheria kwa sababu wanatulazimisha tufanye hivyo.

“Haiwezekani mkoa mmoja Njombe kila siku mauaji, watu hawataki kuacha na sisi vyombo vya ulinzi na usalama tupo,” alisema IGP Sirro.

Mbali na mauaji, alisema mkoa huo pia una matukio mengi ya ubakaji ambayo yakifika mahakamani hubainika kuwa yamehusisha ndugu.

‘’Pili tumeona kuna makosa ya kubaka ni mengi, nimeelekeza waende kutoa elimu kuanzia mashuleni, vyuoni ili kueleza madhara ya kubaka. Lakini mbaya zaidi kesi ikienda mahakamani inaonekana makosa mengi ya kubaka yanashirikisha ndugu.

“Nimesema biashara ya ndugu haipo, wewe kama umefanya kosa la jinai ni kosa la jinai wale lazima waende kutoa ushahidi ili tuwafunge.

“Kwahiyo wale wanaofanya mambo ya kubaka wakisema ni ndugu yake, ukifanya kosa suala la undugu halipo, ukifanya kosa umefanya kosa dhidi ya Jamhuri kwa hiyo unapobaka ujue anayekushtaki ni Jamhuri na tutakushughulikia kwa mujibu wa sheria zilizopo.

“Kwahiyo niwaombe ndugu zangu wana-Njombe haya mambo ya ujinga wa zamani tuachane nao, watu wanabadilika kwa sababu mwisho wa siku unapobaka utafungwa maisha au miaka 30.

 “Kama mtu anataka kuingia kwenye mstari mpeleke kwenye mstari, awe analia anapiga kelele mlete kwenye mstari kwa sababu kama wewe unataka kuua wenzako unategemea nini? Unatoa uhai wa mwenzako ili wewe uendelee kuishi, sisi tutakuchukua vizuri tutakupeleka na wewe utaenda kunyongwa,” alisema.

Aidha Sirro alisema Jeshi la Polisi limejipanga vizuri katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kwamba wananchi wasiwe na hofu na wale wachache watakaoleta vurugu watapambana nao.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Ruth Msafiri, akizungumza katika Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, alisema suala la mauaji sasa liwe basi.

“Madiwani na watendaji naomba tukashirikiane tuseme mauaji sasa basi, mnipe taarifa, kama kuna tukio lolote litatokea nitawaweka ndani hata kijiji kizima, msiniulize ‘lockup’ nitatoa wapi, itapatikana tu. Inasikitisha sana watu wanauawa kinyama,” alisema Ruth.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles